Papa Francisko aelezea ukaribu na watu wa Chad kwa shambulio la kigaidi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana Ijumaa tarehe Mosi Novemba 2024, ikiwa ni Siku Kuu ya Watakatifu Wote, Baba Mtakatifu, ameelezea uchungu wake katika Nchi ya Bara la Afrika. Papa amesema “Ninaeleza ukaribu wangu kwa watu wa Chad, hususan kwa familia za wahanga wa shambulio kubwa la kigaidi siku chache zilizopita, pamoja na wale walioathiriwa na mafuriko.
Kimbunga DANA nchini Hispania
“Na kuhusu majanga haya ya mazingira, tunaomba kwa ajili ya wakazi wa peninsula ya Iberia, "hasa jumuiya ya Valencia, iliyozidiwa na dhoruba ya ‘DANA: kwa ajili ya marehemu na wapendwa wao, na kwa familia zote zilizoharibiwa. Bwana awasaidie wanaoteseka na wale wanaotoa msaada. Tunatoa ukaribu wetu kwa watu wa Valencia.”
Salamu kwa mahujaji
Papa Francisko ametoa salamu mbali mbali: “Nawasalimu nyote kwa upendo, mahujaji kutoka nchi mbalimbali, familia, vikundi vya parokia, vyama na vikundi vya shule. Hasa waamini wanaotoka Rignac (Ufaransa).”
Mbio za Watakatifu
Papa Francisko akikumbusha tukio la 'Mbio za Watakatifu' amesema: “Na ninawasalimu washiriki katika "Mbio za Watakatifu", iliyoandaliwa na Mfuko wa Utume wa Don Bosco. Wapendwa, mwaka huu pia unatukumbusha kwamba maisha ya Kikristo ni mbio, lakini si kama ulimwengu unavyokimbia, la! Ni mbio za moyo wa upendo! Na asante kwa msaada wenu katika kujenga kituo cha michezo nchini Ukraine.”
Kuombea amani nchi za Vita
Papa Francisko kama kawaida yake hakusahu sehemu zenye vita: “Tunasali kwa ajili ya Ukraine inayoteswa, tunasali kwa ajili ya Palestina, Israel, Lebanon, Myanmar, Sudan Kusini, na kwa ajili ya watu wote wanaoteseka kutokana na vita. Kaka na dada, vita daima ni kushindwa, daima! Na ni jambo la kudharauliwa, kwa sababu ni ushindi wa uwongo, mtu anatafuta maslahi ya juu kwa ajili yake mwenyewe na uharibifu wa juu kwa adui, kukanyaga maisha ya binadamu, mazingira, miundombinu, kila kitu; na wote wamefunikwa na uwongo. Na wasio na hatia wanateseka! Ninafikiria wanawake na watoto 153 waliouawa katika siku za hivi karibuni huko Gaza.”
Kumbukumbu ya Siku ya Watakatifu
Papa Francisko akikumbuka kumbukizi la walioaga dunia, ifanyikayo kila tarehe 2 Novemba ya kila mwaka amesema “Kesho itakuwa kumbukumbu ya kila mwaka ya waamini wote waliofariki. Wanaoweza kwa siku hizi wanakwenda kusali kwenye makaburi ya wapendwa wao. Kesho asubuhi mimi pia nitakwenda kuadhimisha Misa katika Makaburi ya Laurentina huko Roma. Tusisahau: Ekaristi ni sala kuu na yenye ufanisi zaidi kwa ajili ya roho za marehemu.” Hatimaye Baba Mtakatifu amesema “Nawatakia wote sherehe njema katika usindikizwaji wa Watakatifu. Ninawasalimu nyote, vijana kike na kiume wa Parokia ya Maria Mkingiwa. Na tafadhali msisahau kuniombea. Likizo njema! Mlo mwema, mchana mwema na kwaheri ya kukuona!