Papa Francisko kwa watu wa kujitolea Vienna:sisi sote tunatajirishana
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 8 Novemba 2024 amekutana mjini Vatican na kikundi cha watu wa kujitolea na watu wasio na makazi maalum, (Begegnung im Zentrum) kutoka Vienna, nchini Austria ambapo katika hotuba yake amesema “Asante kufika kwenu. Kwa kawaida hukutana katika Makao makuu ya Askofu Mkuu huko Vienna - tafadhali mnifikishie salamu zangu kwa Kardinali Schönborn - leo nina furaha kuwakaribisha hapa.” Baba Mtakatifu amebainisha kwamba watoka katika nchi tofauti, “ninyi ni wa maungamo tofauti ya kidini, na kila mmoja wenu amekuwa na uzoefu wake wa maisha, wakati mwingine hata misukosuko mikubwa. Lakini kitu kimoja kinatuunganisha sisi sote: sisi ni kaka na dada, sisi ni watoto wa Baba mmoja. Hii inatuunganisha sote.”
Papa amefurahi sana kwamba “ukweli huu unakuwa dhahiri katika jumuiya yenu wakati mnasaidiana na, katika mikutano yenu, kushiriki kile ambacho kila mtu anaweza kutoa.” Kwa hakika, si kweli kwamba wengine wanatoa na wengine wanapokea tu: sisi sote ni watoaji na wapokeaji, sote tunahitajiana na tunaitwa kutajirishana. Na tukumbuke kwamba hii haitokei tu kupitia zawadi za kimwili, bali pia kupitia “tabasamu rahisi, ishara ya urafiki, sura ya kidugu, kusikiliza kwa dhati, huduma ya bure” (rej. Spes non confundit. Dikirii ya kutangaza Mwaka wa Jubilei, 18).
Kisha, Papa amesema “katika wakati huo, tunafanya kile ambacho Bwana alituambia tufanye, yaani, tupendane kama vile alivyotupenda sisi. Tunamshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi ya upendo wake, ambayo pia huja kwetu kupitia watu wema wanaotuzunguka.” Papa amekazia kusema kuwa “Bwana anatupenda kupita mipaka na magumu yote. Kila mmoja wetu ni wa kipekee machoni pake na kamwe hatusahau. Hebu tujaribu daima, kama kaka na dada, kufanya maisha yetu kuwa zawadi kwa wengine. Asante tena kwa mkutano huu na kwa yote mnayofanya pamoja. Ninawaombea, ninakubariki.” Kwa kuhitimisha, Baba Mtakatifu aliomba wote kusali kwa kimaya kwa dakika moja na baadaye kupngeza (Gott segne uns alle) yaani (Mungu atubariki sisi sote).