Uchungu wa Papa Francisko waathirika wa ajali ya Novi Sad
Vatican News
Walikuwa ni wasafiri wanaosubiri au wafanyakazi wa kila siku katika usafiri, wameketi kwenye majukwaa yenye watu wengi, na wengine ndani wakinunua tiketi za treni. Karibu na adhuhuri, ghafla na ya kutisha, paa la zege juu ya mlango wa kuingilia lilianguka! Hivi ndivyo mkasa wa Novi Sad, nchini Serbia, ulivyotokea siku ya Ijumaa tarehe Mosi Novemba 2024, ambapo watu 14 waliangamia katika ajali hiyo pamoja na wengine watatu kujeruhiwa vibaya.
Ukaribu wa Papa kwa taifa la Serbia
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kupata taarifa hizo alitaka kuwa karibu na watu wa Serbia kwa kumwandikia telegramu Rais Aleksandar Vučić wa Jamhuri ya nchi hiyo ambapo anabainisha kwamba yuko karibu na taifa katika "wakati huu mgumu" na kwamba anaombea "hasa marehemu, familia zao zinazoomboleza na kwa wote waliojeruhiwa ”, huku akihakikisha ukaribu wake wa kiroho.
Maandamano na kukamatwa
Baadhi ya sehemu za kituo hicho zilikuwa zimefanyiwa ukarabati hivi karibuni kwa njia ya mwendo kasi, lakini paa hilo halikuathiriwa na kazi hizo. Siku chache baada ya mkasa huo, maelfu ya watu waliandamana huko Novi Sad na pia kulikuwa na maandamano na ghasia karibu na kituo hicho, jambo ambalo lilichochea hisia za polisi kufyatua mabomu ya machozi na kukamatwa kwa wengine. Kuanguka kwa paa hilo kulisababisha kujiuzulu kwa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi Goran Vesic.