
Papa Francisko:"Asante sana,Jubilei iwe na matunda tele"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Na kabla ya Baraka ya mwisho, yaani mwishoni mwa Misa, Baba Mtakatifu Dominika tarehe 6 Aprili 2025 alifika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro,mbele ya madhabahu na kutoa maneno machache akisema: “Dominika njema kwa wote. Asante sana.” Baadaye Baba Mtakatifu Francisko aliacha Uwanja huo na baadaye kusomwa kwa lugha mbali mbali, maneno ya shukrani ya Papa Francisko.
Maneno hayo yalikuwa yanabainisha kuwa Baba Mtakatifu Francisko amewasalimia kwa upendo wale wote walioshiriki katika maadhimisho haya na kuwashukuru kwa dhati kabisa sala iliyoinuliwa kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya afya yake, akitumaini kwamba, hija ya Jubilei hiyo itakuwa na matunda tele, amewapatia baraka za kitume, akiwapa wapendwa wao, wagonjwa na wanaoteseka, pamoja na waamini wote waliokusanyika leo. Vikundi vifuatavyo viliripoti uwepo wao katika hafla hiyo: kutoka Italia, Jimbo la Vittorio Veneto na Jimbo la Termoli-Larino. Pia kuna vikundi vya wamini kutoka Albania na Kroatia.