Tafuta

Pauline Jaricot Mwanzilishi wa matendo ya Kimisionari Pauline Jaricot Mwanzilishi wa matendo ya Kimisionari 

Padre Nowak:kuongeza nguvu za kusaidia utume Ulimwenguni

Mfuko wa Kimataifa wa Mshikamano wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, unaofadhiliwa katika Siku ya Kimisionari Duniani,unawezesha utume,hata wale walio maskini na mbali zaidi duniani.Amesema hayo Katibu wa Baraza la Kipapa la Utume wa Kimisionari katika muktadha wa Siku ya kimisionari duniani 2023 inayoongozwa na kauli mbiu Mioyo inayowaka na miguu inayotembea.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Mfuko wa Mshikamano wa Kiulimwengu (Fus) wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni aina ya "tanki ya akiba" inayotuwezesha kusaidia utume wa kimisionari, hata wale walio maskini zaidi na walio mbali zaidi duniani. Shukrani kwa nyenzo hii, rasilimali zinaelekezwa kwa wahudumu wa kichungaji wa kila Kanisa ambao ni: makatekista, mapadre, shule, afya na wahudumu wa kijamii wanaopata huduma na msaada wa mkusanyo ambao kila Kanisa la mahalia linachangia kadiri ya upatikanaji wake kiuchumi, hata kama wakati mwingine "mchango  huo ni wa mfano tu, kama sarafu ya mjane katika Injili", alifafanua hayo Padre Tadeusz Jan Nowak, Katibu Mkuu wa Shirika la Kipapa la Kueneza Imani, akifafanua maana ya ukuu wa  mshikamano kati ya Makanisa ambayo shukrani kwa matoleo yaliyokusanywa kwa ajili ya Siku ya Wamisionari Duniani (WMD).

Mtandao wa ulimwengu unaoundwa na makanisa

“Kwa hakika ni mtandao wa kiulimwengu unaoundwa na Makanisa yote katika ushirika wa Kanisa zima alisema huku akielezea kuwa: mtandao wa sala, mafunzo, habari, kusaidiana, ili kufanya uinjilishaji uendelee duniani.” Mfuko wa Mshikamano wa Kiulimwengu unasambaza misaada kwa Makanisa mapya na katika maeneo ya uinjilishaji wa kwanza: haya ni takriban hali halisi 1,150 mahalia (kuanzia jimbo, majimbo kuu, vikariati na majimbo ya kitume, utume wa kisheria) ulioko Afrika, Asia, Visiwa vya Australia na katika baadhi ya Kanda za Amerika ya Kusini. “Mkusanyo uliofanywa katika hafla ya Siku ya Kimisionari Duniani ambayo inaadhimishwa katika kila jumuiya ya Kikristo ulimwenguni inatiririka katika Mfuko wa Ulimwengu  kwa mujibu wa  Padre Nowak.

Kuelewa nini maana ya kusaidia mahitaji ya utume

Katika kila parokia au jumuiya watu wanaosali, misa huadhimishwa na waamini wanaweza kutoa kitu cha kusaidia wamisionari duniani. Inazidi kuwa vigumu kuwaelewesha watu kwamba, mahitaji mazito ya Uinjilishaji, ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayazungumzia mara kwa mara, ni pia na juu ya mahitaji yote msingi ya kichungaji ya Makanisa katika hali zenye uhitaji mkubwa zaidi; yaani mafunzo ya waseminari, mapadre, makatekista wa dini, wa ndani, ujenzi na matengenezo ya maeneo ya ibada, seminari na miundo ya parokia, msaada kwa vyombo vya habari vya Kikatoliki vya mahali hapo (TV, radio na waandishi wa habari), utoaji wa vyombo vya usafiri (magari, au pikipiki, baiskeli, boti), msaada wa katekesi, mafundisho ya Kikatoliki, malezi ya Kikristo ya watoto na vijana".

Majimbo kama 940 yanahitajia msaada wa shughuli za kichungaji

Sehemu kubwa ya Mfuko huo hufikia majimbo yanayohitaji ruzuku ya kawaida: Majimbo 940 hupokea, kwa jumla ya karibu dola milioni 27 kwa mwaka. Ruzuku ya kawaida huwapa maaskofu fursa ya kuwa na kiasi kinachowawezesha kusaidia maendeleo ya jumuiya ya Kikristo na miundo ya kikanisa: kwa mfano fedha za petroli kuruhusu ziara za kichungaji kwa askofu, kununua Mashine ya kutoa kopi ili kusaidia mapadri wa majimbo ambayo hayana aina nyingine za usaidizi. Kwa hiyo "Tumekuwa tukipitia hali ya kushuka kwa muda - anahitimisha Padre Nowak - na kwa bahati mbaya kila mwaka mfuko unapungua: miaka kumi iliyopita kulikuwa na karibu dola milioni 140 za kusambazwa, mwaka huu nusu, 70 tu. Inabidi ujiulize kwa mfano, Majimbo ya  za Myanmar, Malawi, Bangladesh, Pakistan, Sri Lanka na nyinginezo zitapata wapi pesa za utume wao?”

Ujumbe wa Papa wa Siku ya Kimisionari 2023

Hayo yote ni katika fursa ya Siku ya Kimisionari Duniani itakayoadhimishwa tarehe 22 Oktoba 2023, ambapo Baba Mtakatifu Francisko alikuwa tayari ametoa ujumbe wake ukiongozwa na Kifungu cha Injili ya (Luka 24,13- 35) kisemacho mioyo inayowaka na miguu inayotembea. Ni kifungu kinachoeleza mitume wa Emau. Wanafunzi hao wawili walichanganyikiwa na kukatishwa tamaa, lakini kukutana na Kristo katika Neno na katika Mkate uliomegwa uliwasha ndani yao shauku ya kuanza tena kuelekea Yerusalemu na kutangaza kwamba Bwana amefufuka kweli. Katika simulizi ya Injili, tunafahamu mabadiliko ya wanafunzi kutoka kwa baadhi ya picha zinazodokeza: mioyo inayowaka kwa ajili ya Maandiko yaliyofafanuliwa na Yesu, macho yaliyofunguka katika kumtambua na, kama kilele, miguu katika mwendo. Kwa kutafakari mambo hayo matatu, yanayoonesha ratiba ya wanafunzi wamisionari, tunaweza kufanya upya bidii yetu ya kueneza injili katika ulimwengu wa leo……

Nyuso za mitume wa Emau zilionekana kukata tamaa

Kifungu cha kwanza ambacho Papa Francisko anaanza kuendeleaz ni Mioyo inayowaka kuwa “walipotufafanulia Maandiko walihisi hivyo”. Kwa njia hiyo Neno la Mungu huangaza na kubadilisha moyo katika utume. Wakiwa njiani kutoka Yerusalemu kwenda Emau, mioyo ya wanafunzi hao wawili ilikuwa na huzuni - kama ilivyokuwa dhahiri kutokana na kuonekana nyuso zao- kwa sababu ya kifo cha Yesu, ambaye walikuwa wamemwamini. Wakikabiliwa na kushindwa kwa Mwalimu aliyesulubiwa, tumaini lao kwamba Yeye ndiye Masihi liliporomoka. Na tazama, “walipokuwa wakizungumza na kujadiliana, Yesu mwenyewe akakaribia, akatembea pamoja nao” (mstari 15). Kama vile mwanzoni mwa wito wa wanafunzi, hata sasa wakati wa kuchanganyikiwa kwao, Bwana huchukua hatua ya kuwakaribia wanafunzi wake na kutembea pamoja nao. Katika rehema zake kuu, Yeye hachoki kuwa pamoja nasi, licha ya kasoro, mashaka, udhaifu wetu, licha ya huzuni na tamaa inayotuongoza kuwa “wajinga na wa polepole wa moyo” (mstari 25), watu wa imani haba.

Leo kama hapo awali Yesu yuko karibu na wanafunzi wake wamisionari

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakazia kusema kuwa Leo, kama vile wakati ule, Bwana mfufuka yuko karibu na wanafunzi wake wa kimisionari na anatembea pamoja nao, hasa wanapohisi wamepotea, wamekata tamaa, wanaogopa mbele ya fumbo la uovu linalowazunguka na kutaka kuwakosesha pumzi. Kwa hiyo, "tusikubali kunyang'anywa tumaini!" (Evangelii gaudium, 86). Bwana ni mkuu kuliko shida zetu, hasa tunapokutana nazo katika kutangaza Injili kwa ulimwengu, kwa sababu utume huu, hata hivyo, ni wake na sisi ni washirika wake wanyenyekevu, "watumishi wasiofaa" (rej Luka 17, 10). Ninadhihirisha ukaribu wangu katika Kristo kwa wamisionari wote ulimwenguni, hasa kwa wale wanaopitia wakati mgumu: Bwana mfufuka, yuko pamoja nanyi kila wakati na anaona ukarimu wenu na sadaka yenu  kwa utume wa uinjilishaji katika sehemu za mbali.  Sio siku zote za maisha zimejaa mwanga wa jua, lakini tukumbuke daima maneno ya Bwana Yesu kwa marafiki zake kabla ya mateso yake: "Ulimwenguni mna dhiki, lakini muwe na ujasiri: Mimi nimeushinda ulimwengu!"(Yh 16:33 ). Baada ya kuwasikiliza wale wanafunzi wawili walipokuwa njiani kuelekea Emau, Yesu aliyefufuka “akianza na Musa na manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu” (Lk 24:27 ). Na mioyo ya wanafunzi ikachangamka, wakaamini wao kwa wao: Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu alipokuwa akisema nasi njiani, alipotufafanulia Maandiko? (Mst. 32). Hakika, Yesu ndiye Neno lililo hai, ambalo peke yake linaweza kuufanya moyo kuwaka, kuangaza na kubadilika.

Tuwezeshe Utume wa Kimisionari
16 October 2023, 13:36