Kard.Krajewski:Nchi Takatifu inaomba amani ya kudumu na ya dhati
Vatican News
Nilitumwa hapa katika Nchi Takatifu na Baba Mtakatifu kumwakilisha katika maeneo haya ya Biblia, ambapo Wakristo wanaomba amani. Nilitumwa kusali pamoja nao kwa niaba ya Papa. Ndivyo Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo alivyosema akiwa karibu kufikia mwisho wa utume wake, na kueleza maana ya siku hizi za ziara hiyo alizotumia pamoja na wale wanaoteseka kati ya Yerusalemu, Bethlehemu na Nazareti. Alibainisha akiwa katika mji wa mwisho ambapo tarehe 26 Desemba 2023 Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha kumbu kumbu kifodini cha Mtakatifu Stefano na ambako kuna jumuiya kubwa ya Kikristo.
Ombi la amani
Kutoka Yerusalemu hadi Nazareti, kama kilomita 200 hivi Kardinali Krajewski, alikwenda kwenye Basilica ya Kupashwa Habari pamoja na paroko wa Gaza ambapo walikuwa na wakati wa sala ya kimya. Kwa mujibu wa Kardinali Krajewski alisimulia juu ya sala ya kunong'ona na ya kutoka moyoni kwa ajili ya kuomba amani, iliyounganishwa na ya Papa Francisko na Wakristo ulimwenguni kote. Sala ambayo kisha ilikuwa mwili kwa kuwa sauti katika adhimisho la Misa Takatifu na katika sala ya Malaika wa Bwana. Kwa upande wake alisema “ni maombi yaliyoongozwa pamoja na watawa na Wakristo wa madhehebu mengine.” Kisha alifanya ziara yake kwa baadhi ya jumuiya za kitawa kama vile watawa wa Familia Takatifu ya Nazareti na Fatebenefratelli, mapadre wa Shirika la Hosptiali wa Mtakatifu Yohane wa Mungu, wanaosimamia hospitali kubwa katika mji wa Yesu.
Haki na amani
Alasiri ya tarehe 26 Desemba alifanya maombi katika Mlima wa Heri kwenye mwambao wa Ziwa Tiberia kama msingi wake. Hapa kulikuwa na tafakari iliyoakisi Mahubiri ya Yesu ya Mlimani hasa yasemayo: “Heri wapatanishi ....” Kwa mujibu wa Kardinali Krajewski alieleza kuwa: “hapo tuliomba amani kwa maneno haya: 'Ee Mungu umefunua kwamba wapatanishi wataitwa watoto wako'. Tulimwomba Mungu: atujaalie kuitafuta hiyo haki ambayo inaweza tu kutuhakikishia amani thabiti na ya kweli. Tazama, tuliomba amani hii: imara na ya kweli. Sio tu kusitisha mapigano bali kuweka amani mioyoni mwetu na kati yetu. Ardhi ya Gaza inahitaji amani.”
Kadhalika Mjumbe wa Papa katika Nchi Takatifu alifanya mkutano na watawa wamisionari wa upendo huko Yerusalemu kwa kushiriki mateso ya watawa watatu walioko Ukanda wa Gaza na ambao hawawezi kupata habari. Jioni hiyo ya tarehe 26 Desemba Kardinali Krajewski alianza safari ya kurejea mjini Vatican akiwa na uhakika, baada ya safari hyoi, kwamba sala ni pumzi ya roho kama vile Papa Francisko alivyosema mara kadhaa. Nafsi inayoteseka leo kutokana na vita ambavyo vinaharibu ulimwengu na ambayo, kama Papa alikumbuka katika siku za hivi karibuni, husababisha taabu na njaa. Sala kwa ajili ya Yesu, Mfalme wa Amani, inaweza kufanya mengi kubadili mioyo na hivyo kuingiza ubinadamu mpya.