Makamu Rais wa Malawi Saulos Kalus Chilima alifariki dunia na wengine 9 kwa ajali ya ndege tarehe 10 Juni 2024. Makamu Rais wa Malawi Saulos Kalus Chilima alifariki dunia na wengine 9 kwa ajali ya ndege tarehe 10 Juni 2024. 

Malawi:Makamu Rais wa Malawi afariki kwa ajali ya Ndege

Rais wa nchi ya Malawi,Lazarus Chakwera,alitangaza juu ya kifo cha Makamu wake,Saulos Klaus Chilima,moja kwa moja kwenye TV kilichotokea tarehe 10 Juni 2024 kwa ajali ya ndege.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kufuatia na ajali iliyotokea nchini Malawi, Rais Lazarus Chakwera, wa Malaiwi alitangaza kifo cha Makamu wake, Saulos Klaus Chilima, moja kwa moja kwenye TV. Katika tangazo hilo alisema: "Ninasikitika kuwataarifu kwamba timu za uokoaji zilipata mabaki ya ndege hiyo msituni. Hakukuwa na walionusurika. Watu wote waliokuwemo kwenye ndege hiyo  walikufa papo hapo." Ndege aliyokuwa akisafiria Makamu Rais ilipoteza mawasiliano ya rada tarehe 10 Juni 2024 majira ya saa 3 asubuhi kwa saa za huko, ilipokuwa ikijiandaa kutua huko Mazuzu, kaskazini mwa Malawi.

Maombolezo nchini Malawi
Maombolezo nchini Malawi

Wadhibiti wa ndege walikuwa wamemshauri rubani kurejea Lilongwe, mji mkuu wa nchi hiyo, lakini alama za ndege hiyo zilipotea na baadaye ikapatikana ikiwa imeanguka msituni karibu na Mazuzu.Vikosi vya uokoaji vilitatizika kutafuta mabaki hayo kutokana na uoto mnene. Serikali ya Malawi ilikuwa imeomba Mataifa kadhaa msaada katika kumtafuta. Mbali na Makamu wa Rais, kwenye ndege hiyo kulikuwa na watu wengine 9 akiwemo mke wa zamani wa Rais wa zamani Bakili Muluzi. Mara baada ya kusikika taarifa za kifo cha Chilima, meseji za rambirambi zilitokea kwenye mitandao ya kijamii kutoka kwa baadhi ya mapadre wa Malawi ambao walimkumbuka kuwa ni Mkatoliki mwenye bidii.

Nyadhifa za Chilima

Saulos Klaus Chilima aliazaliwa tarehe 12 Februari 1973 na  alikuwa mchumi na mwanasiasa wa Malawi ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Malawi kuanzia 2014 hadi 2019 na tena kuanzia 2020 hadi kifo chake tarehe 10 Juni 2024. Chilima alichukua wadhifa wake tarehe 28 Juni 2020, na kushinda wengi pamoja na mgombea urais Lazarus Chakwera. Chilima pia aliwahi kuwa Waziri wa Mipango ya Uchumi na Maendeleo, pamoja na Mkuu wa Maboresho ya Sekta ya Umma, nafasi ambayo pia aliwahi kushika chini ya utawala wa rais wa zamani Peter Mutharika. Kabla ya kujiunga na siasa, Chilima alishika nyadhifa kuu za uongozi katika makampuni mbalimbali ya mataifa mbalimbali yakiwemo Unilever, Coca-Cola na Airtel Malawi, ambapo alipanda cheo hadi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu.

Watu wanaombeleza kifo cha makamu Rais wa Malawi
Watu wanaombeleza kifo cha makamu Rais wa Malawi

Mnamo tarehe 10 Juni 2024, ndege iliyokuwa imembeba Chilima na abiria wengine tisa ilianguka katika Hifadhi ya Msitu wa Chikangawa katika Wilaya ya Mzimba ilipopaa kutoka mji mkuu wa Malawi Lilongwe na haikutua katika eneo lililopangwa kufikia Uwanja wa Ndege wa Mzuzu. Ndege hiyo haikuweza kutua katika uwanja wa ndege kutokana na kutoonekana vizuri na iliamriwa kurejea Lilongwe kabla ya ajali hiyo. Tarehe 11 Juni 2024, Chilima na abiria wengine waliripotiwa kufariki baada ya mabaki ya ndege hiyo kupatikana.

12 June 2024, 10:30