Tafuta

Mei, Mosi 2024 Baba Mtakatifu Francisko amesema, Mama Kanisa anauanza Mwezi Mei uliotengwa kwa heshima na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Mei, Mosi 2024 Baba Mtakatifu Francisko amesema, Mama Kanisa anauanza Mwezi Mei uliotengwa kwa heshima na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mwezi Mei Ni Kwa Ajili ya Ibada na Heshima Kwa Bikira Maria

Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano ya maisha ya kiroho; Ni Sanduku la Agano Jipya, Mlango wa huruma ya Mungu; Nyota angavu ya asubuhi na Mama wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo makini cha upendeleo wa Mungu katika maisha yake, akamkinga na dhambi pamoja na mauti, ili aweze kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kuwasaidia waamini kumfuasa Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya katekesi yake, Jumatano Mei, Mosi 2024 amesema, Mama Kanisa anauanza Mwezi Mei uliotengwa kwa heshima na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ibada kwa Bikira Maria na Ibada ya huruma ya Mungu ni nyenzo muhimu sana katika hija ya kuutafuta na kuukumbatia utakatifu wa maisha pamoja na kuendelea kuwa wafuasi aminifu wa Kristo sanjari na mashuhuda wa huruma ya Mungu hapa duniani. Anawaalika waamini kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwasaidia kutambua na kuthamini dhamana na nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika ufuasi wao. Bikira Maria ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu, Mtumishi mwaminifu na mwalimu mkuu katika shule ya huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Ni nyota angavu inayowasindikiza waamini katika hija ya kumwendea Baba wa milele!

Mwezi Mei Umetengwa kwa ajili ya ibada na heshima kwa Bikira Maria
Mwezi Mei Umetengwa kwa ajili ya ibada na heshima kwa Bikira Maria

Bikira Maria ni mfano bora wa kuigwa katika mapambano ya maisha ya kiroho, kwani ni kielelezo cha Eva mpya, Sanduku la Agano, Mlango wa huruma ya Mungu na mbingu, Nyota angavu ya asubuhi na Mama wa mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo makini cha upendeleo wa Mungu katika maisha yake, akamkinga na dhambi pamoja na mauti, ili aweze kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kuwasaidia waamini kumfuasa Kristo kwa ujasiri na moyo mkuu. Huu ni mwaliko wa kuingia katika shule ya upendo inayoongozwa na kusimamiwa na Bikira Maria.

Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa
Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa

Hapa waamini wanapaswa kukubali kuona kwa jicho la imani: mateso na mahangaiko ya Bikira Maria tangu siku ile alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu hadi aliposimama chini ya Msalaba na kushuhudia Mwanaye mpendwa akiinamisha kichwa na kukata roho! Waamini wajitahidi kumchukua Bikira Maria katika maisha yao kwa kujiweka wakfu kwa Bikira Maria; kwa kusali na kutafakari Rozari ambayo kimsingi ni muhtasari wa Injili, yaani: maisha, utume na historia ya kazi nzima ya ukombozi na kwamba, hii ni Biblia ya waamini wa kawaida! Waamini wajenge na kudumisha Ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria pamoja na kufanya mapilizi kwa ajili ya dhambi za walimwengu. Ili kukuza na kudumisha moyo na ari ya Ibada kwa Bikira Maria kuna haja ya kujikita katika fadhila ya: imani, utii, unyenyekevu, huruma, uwajibikaji pamoja na kujiaminisha kwa Kristo Yesu!

Waamini wanaalikwa kuombea amani na utulivu duniani
Waamini wanaalikwa kuombea amani na utulivu duniani

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa ya Mei Mosi, 2024 kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia kwani kuna watu ambao wanaendelea kuteseka kutokana na vita na kwamba, vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu na wala hakuna mshindi wa vita. Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wa Mungu nchini Ukraine, Israeli, Palestina, Rohingya na Mynmar. Baba Mtakatifu anasema, watu wa Mungu wanahitaji amani ya kweli. Inasikitisha kuona kwamba, Mataifa mengi yanawekeza katika mchakato wa utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha, faida kubwa inayopatikana kwa mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu anasema, huu ni muda muafaka kwa ajili ya kuombea amani duniani, ili iweze kusonga mbele!

Mwezi wa Bikira Maria
02 May 2024, 12:19