Tafuta

Washirikishi wa Kongamano la Mfuko wa "Centesimus Annus Pro Pontefice": Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, Heshima na Haki Msingi za binadamu. Washirikishi wa Kongamano la Mfuko wa "Centesimus Annus Pro Pontefice": Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, Heshima na Haki Msingi za binadamu. 

Mfuko wa Centesimus Annus Pro Pontefice: Mafundisho Jamii ya Kanisa: Utu, Heshima na Haki Msingi

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, kwa washiriki wa Kongamano hili, Jumamosi tarehe 8 Oktoba 2022 amekazia kuhusu: Ukuaji wa uchumi unaozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu; Huruma na upendo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; umuhimu wa kazi kama kipimo cha utu na heshima ya binadamu na wongofu wa kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 5 Juni 1993. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huu ni kufanya upembuzi yakinifu, kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbalimbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa uwepo fungamani wa Kanisa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Mfuko huu unawajumuisha viongozi wa Kanisa Katoliki, wasomi na wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali. Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, kuanzia tarehe 6-8 Oktoba 2022 umekuwa ukifanya kongamano la Kimataifa, ambalo limenogeshwa na kauli mbiu “Ukuaji shirikishi wa uchumi, ili kutokomeza umaskini na kukuza maendeleo endelevu na amani.”

Washiriki wa kongamano la CAPP kwa Mwaka 2022
Washiriki wa kongamano la CAPP kwa Mwaka 2022

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, kwa washiriki wa Kongamano hili, Jumamosi tarehe 8 Oktoba 2022 amekazia kuhusu ukuaji wa uchumi unaozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu; Huruma na upendo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; umuhimu wa kazi kama kipimo cha utu na heshima ya binadamu na wongofu wa kweli. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mfuko wa “Centesimus Annus Pro Pontefice” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ni jukwaa muhimu sana linaloweza kuwasaidia watu wa Mungu kufahamu mambo msingi ya kiuchumi na kijamii mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa katika muktadha wa mazingira halisi ya binadamu. Ukuaji wa uchumi haina budi kuzingatia na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, Mfuko huu unayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, unawasaidia watu wa Mungu kuangalia ukuaji wa uchumi kwa jicho la tunu msingi za Kiinjili, kwa kuwapatia watu wote heshima yao bila kumdharau mtu awaye yote. Mfuko huu unapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kukazia huruma na upendo, tunu msingi zinazobubujika kutoka katika maisha na utume wa Kristo Yesu.

CAPP: Mafundisho Jamii ya Kanisa
CAPP: Mafundisho Jamii ya Kanisa

Uchafuzi mkubwa wa mazingira sanjari na athari za mabadiliko ya tabianchi ni chanzo kingine kikubwa kinachoendelea kuwatumbukiza watu katika umaskini wa hali na kipato. Kazi ni msingi wa maisha na utambulisho wa mwanadamu; ni sehemu ya makuzi na kichocheo cha maendeleo. Kutoa msaada wa fedha kwa maskini linapaswa kuwa ni suluhisho la muda katika kukidhi mahitaji msingi. Lakini maskini wanapaswa kupewa fursa ya kujijenga kiuchumi na kamwe maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasichukue nafasi ya nguvu kazi, hali inayoweza kupelekea migongano ya kijamii. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha mtandao wa mahusiano yenye kuaminiana, kutegemea heshima, kanuni na taratibu ambazo ni mambo muhimu sana katika ukuaji wa uchumi badala ya kulenga kupata faida kubwa kwa muda mfupi, jambo ambalo ni hatari kubwa. Rej. Laudato si n. 128. Jambo la msingi ni kudumisha misingi ya haki, usawa, utu na heshima ya binadamu, ili kuondokana na uwezekano wa kuzalisha maskini wapya ndani ya jamii. Viongozi wakuu sehemu za kazi, wawahudumie wafanyakazi wao kwa heshima na nidhamu, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu wamoja, licha ya tofauti zao za hali na kipato. Mwelekeo na mtazamo huu mpya unahitaji wongofu wa ndani, unaoheshimu utu wa binadamu, kwa kusimama kidete kupinga mashindano ya kiuchumi yasiyokuwa na mvuto wa mashiko na badala yake, yamekuwa ni chanzo cha kinzani, migogoro na vita. Utu na heshima ya binadamu ni nyenzo msingi katika ujenzi wa amani duniani.

Mafundisho Jamii ya Kanisa
08 October 2022, 14:59