Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya wazee kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 23 Julai 2023 Maadhimisho ya Siku ya wazee kwa mwaka huu ni hapo Jumapili tarehe 23 Julai 2023  

Siku ya Wazee Duniani Tarehe 23 Julai 2023: Kauli Mbiu!

Papa Francisko anawaalika waamini kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani kwa Ibada ya Misa Takatifu na vijana wa kizazi kipya watumie fursa hii, kuwatembelea na kuwasaidia wazee katika maisha yao. Na wazee nao, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, wajisadake kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha ya kiroho kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Domika ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Dominika tarehe 23 Julai 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50. Maadhimisho haya yanafanyika siku chache tu kabla ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kuanzia tarehe 1 – 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria akaondoka kwa haraka” Lk 1:39. Kimsingi hii ni hija ya maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa waamini lakini hasa vijana wa kizazi kipya, kuguswa na moyo wa unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa wengine kama alivyofanya Bikira Maria kwa kumtembelea binamu yake Elizabeth. Safari hii ya Bikira Maria inafungua macho ya waamini ili kuangalia historia ya wokovu, kwa wanawake hawa wawili, wanavyopokea na kukumbatia upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao na inavyopenyeza katika historia ya mwanadamu na hivyo kumkirimia furaha ya Injili. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani kwa Ibada ya Misa Takatifu na vijana wa kizazi kipya watumie fursa hii, kuwatembelea na kuwasaidia wazee katika maisha yao. Na wazee nao, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, wajisadake kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea vijana wa kizazi kipya katika hija ya maisha ya kiroho kama sehemu ya ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya udugu wa kibinadamu katika ulimwengu mamboleo.

Siku ya wazee Duniani ipambwe kwa Ibada ya Misa Takatifu
Siku ya wazee Duniani ipambwe kwa Ibada ya Misa Takatifu

Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Hii ni ahadi ya uwepo endelevu na fungamani wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wito wa wazee duniani ni kulinda mapokeo, amana na utajiri wa jamii ili kuweza kuurithisha kwa kizazi kipya pamoja na kuwalinda vijana katika hija ya maisha yao hapa duniani ili wasijikwae, wakateleza na hatimaye kukengeuka! Wazee hata katika uzee wao, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi kieleweke kwa msaada na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Wazee na vijana wanahitajiana, ili kukamilishana katika hija ya maisha yao na hakuna mtu anayeweza kujiokoa peke yake. Baba Mtakatifu anawataka mababu, mabibi na wazee kujikita katika nguzo kuu tatu za maisha: Ndoto, Kumbukumbu na Sala kama kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kwa waja wake. Kwa bahati mbaya sana, wazee katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia wanaonekana kana kwamba, ulimwengu mamboleo si mahali pao tena, pengine ingewabidi kutafuta mahali pa kuishi.

Vijana na wazee washikamane
Vijana na wazee washikamane

Wazee ni watu wanaotelekezwa na ndugu na jamaa zao. Wananyimwa haki zao msingi na huduma muhimu kama vile afya; mara nyingi ni watu wanaoteseka sana kutokana na utamaduni wa kifo ambao unaendelea kuwanyemelea watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Wazee wamegeuzwa kuwa ni walezi wa wajukuu zao vijijini wakati watoto wao wenyewe “wanakula bata kwa mrija” huku wakiendelea kutesa kwa zamu.” Jambo hili ni hatari sana kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu. Wazee wengi hawakuwa na kipato cha kutosha, kiasi cha kuwawezesha kufurahia maisha ya uzeeni na hasa ikiwa kama wazee hawa walikuwa ni waadilifu. Kumbe, vijana wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na watoto, ndugu na jamaa ili kujenga uchumi wa kaya zao. Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kuthaminiwa mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kutetea, kulinda na kudumisha haki zao msingi. Kama sehemu ya maandalizi ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Wazee Duniani unaweza kutembelea katika Wavuti ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa anuani ifuatayo: (www.laityfamilylife.va).

Siku ya wazee Duniani

 

 

15 June 2023, 16:29