Tafuta

Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu.   (Vatican Media)

Papa Francisko: Maadhimisho ya Sinodi XVI ya Maaskofu: Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kupenda ni kuhudumia na kwamba, Kanisa linaitwa na kutumwa kumwabudu Mungu na Kanisa linapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma na bandari ya huruma ya Mungu; mwaliko kwa watu wa Mungu ni kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na la Kimisionari, tayari kumwabudu Mungu na kuwahudumia binadamu, kwa kutangaza na kushuhudia faraja pamoja na furaha ya Injili. Mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Awamu ya Kwanza Ngazi ya Kiulimwengu yalizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023 kwa Sala na Mkesha wa Kiekumene, tukio ambalo lilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Makanisa. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine, alikazia umuhimu wa kujenga utamaduni wa ukimya, ili kumsikiliza Roho Mtakatifu na kwamba, maadhimisho ya Sinodi ni fursa muhimu ya ujenzi wa umoja na udugu ndani ya Kanisa. Watu wa Mungu walisali pamoja na kusikiliza shuhuda za watu mbalimbali. Maadhimisho ya Sinodi ni muda muafaka kwa watu wa Mungu kujikita katika mageuzi yatakayosaidia mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kulitakasa Kanisa kutokana na mapungufu yake. Ukimya ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Ni muhimu hata katika mchakato wa ujenzi wa umoja miongoni mwa Wakristo, kwani sala ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene, ili wote wawe wamoja.

Sinodi ya Maaskofu: Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Sinodi ya Maaskofu: Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Makardinali wapya, Jumatano tarehe 4 Oktoba, 2023 Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Katika mahubiri yake aligusia changamoto alizokabiliana nazo Kristo Yesu katika maisha na utume wake, akainua macho yake mbinguni na kumshukuru Baba yake wa mbinguni kwa hekima na akili anayeona mema yaliyofichika, yanayokuwa, mbegu ya Neno la Mungu linalopokelewa kwa moyo mnyoofu, mwanga wa Ufalme wa Mungu unaoendelea kung’ara hata katikati ya usiku wa giza. Kumbe, mwono wa Kristo Yesu ni chemchemi ya baraka, ni jicho linalopokea changamoto na mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa lijenge utamaduni wa kuwasikiliza waamini walei katika utume wake
Kanisa lijenge utamaduni wa kuwasikiliza waamini walei katika utume wake

Dominika tarehe 29 Oktoba 2023, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Katika mahubiri yake amekazia kuhusu Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani, inayokita mizizi yake katika upendo na kuabudu; changamoto na mwaliko wa kupambana na malimwengu. Kupenda ni kuhudumia na kwamba, Kanisa linaitwa na kutumwa kumwabudu Mungu na Kanisa linapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma na bandari ya huruma ya Mungu; mwaliko kwa watu wa Mungu ni kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na la Kimisionari, tayari kumwabudu Mungu na kuwahudumia binadamu, kwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.  Baba Mtakatifu Francisko anasema, swali la Farisayo kwa Kristo Yesu katika Torati kuhusu Amri kuu ni endelevu hata kwa waamini wa nyakati hizi na kwamba, jibu la Kristo Yesu ni wazi: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” Mt 22: 37-40.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Umoja, Ushiriki na Utume
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Umoja, Ushiriki na Utume

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kupenda ni kumwabudu na kumtambua Mwenyezi Mungu kuwa ni Bwana na hivyo kumpatia nafasi ya kwanza kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeanza kuwapenda kwanza. Kuabudu ni tendo la kwanza la fadhila ya Kimungu. Kumwabudu Mungu ni kumkiri kama Mungu, Muumba na Mkombozi; Bwana na Msimamizi wa kila kitu kilichopo, kama Mapendo yasiyo na kifani, mapendo yenye huruma. Hii ni hija ya Kanisa katika historia na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa maana ya maisha ya mwanadamu, msingi wa furaha ya kweli, sababu ya matumaini na uhakika wa uhuru kwa waja wake. Upendo kadiri ya Maandiko Matakatifu ni kielelezo cha mapambano dhidi ya kuabudu miungu wa uwongo, kazi ya mikono ya wanadamu. Zina vinywa lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii. Rej. Zab 115-4-5. Mwenyezi Mungu yu hai daima, ingawa wakati mwingine, mwanadamu anakosa ufahamu wa Mungu, kiasi hata cha kujikatia tamaa, hali inayompelekea mwamini kuabudu miungu wa uwongo kwa kutaka Mwenyezi Mungu atende kadiri ya matakwa ya mwamini na hivyo kuufungia upendo wake mkuu kadiri ya mpango ya kibinadamu, kumbe waamini wanapaswa kumwabudu Mungu kwa mshangao.

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga Sinodi ya XVI ya Maaskofu

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupambana fika na miungu wa uwongo na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu; kwa kutaka kujikweza, kutafuta mafanikio ya chapuchapu, uchu wa mali na madaraka na wakati mwingine miungu wa uwongo wanajitokeza hata katika maisha ya kiroho, mawazo ya kidini na hata pengine ufanisi katika shughuli za kichungaji, yote haya yanaweza kumfanya mwamini kujitafuta mwenyewe badala ya kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafuta muda wa sala ili kumwabudu Kristo Yesu katika Tabernakulo. Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa kumwabudu Kristo Yesu katika ukimya, tafakari ya Neno la Mungu, ili aweze kuwatakasa na kuwatakatifuza; kuwaongoa na kuwapyaisha kwa moto wa Roho wake Mtakatifu! Baba Mtakatifu anasema, kupenda ni kumhudumia Mungu na jirani na hivyo kuondokana na uchoyo pamoja na ubinafsi na kwamba, mabadiliko ya kweli ndani ya Kanisa yanasimikwa katika kumwabudu Mungu na kuwapenda jirani. Kumbe, Kanisa halina budi kujikita katika kumwabudu Mungu na huduma kwa binadamu, tayari kuganga na kuponya madonda ya binadamu; huku akiwasindikiza wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii. Hawa ni wageni, wajane na watoto yatima. Huu ndiyo upendo uliojionesha kwa Mungu kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri na kwamba, ni kipimo hiki cha upendo anachowataka Waisraeli wakitumie kwa wale wote wanaoteseka, kunyanyaswa na kudhulumiwa.

Ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa ni muhimu sana
Ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa ni muhimu sana

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu amewakumbuka wahanga wa vita sehemu mbalimbali za dunia, wakimbizi na wahamiaji, maskini na wote wanaoelemewa na mzigo wa ugumu na changamoto za maisha; watu ambao wamelia kiasi kwamba, hawana tena machozi na wala sauti. Baba Mtakatifu anawaonya wale wote wanaojishughulisha na mitandao ya unyonyaji na dhuluma, kwani hii ni dhambi kubwa dhidi ya utu na udugu wa kibinadamu. Wafuasi wa Kristo Yesu, wanataka kupeleka chachu ya Injili kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wanyonge na wale wasiokuwa na sauti. Waamini wanaitwa kuota ndoto ya Kanisa linalowahudumiwa watu wote kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; Kanisa ambalo malango yake yako wazi; Kanisa ambalo kimsingi ni bandari ya huruma ya Mungu kwa wahitaji zaidi, ili kuwapokea na kuwaweka huru na mahali pa salama zaidi. Hii ni changamoto kwa waamini kuwasaidia na kuwaokoa wale wote wanaozama kwenye dimbwi la baa la umaskini, njaa na maradhi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa Ibada hii ya Misa Takatifu anahitimisha maadhimisho ya awamu ya kwanza ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaliyowasaidia Mababa wa Sinodi kujikita katika “mawasiliano katika Roho” ili kugundua ndani mwao uzuri wa udugu wa kibinadamu uliowawezesha kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kwa kutambua utajiri wa historia na mang’amuzi mbalimbali, kiasi cha kujizamisha katika kumsikiliza Roho Mtakatifu. Kwa leo si rahisi kuona matunda ya mchakato huu, lakini kwa siku za mbeleni, Kristo Yesu ataendelea kuwaongoza ili kujikita zaidi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na la Kimisionari, linalomwabudu Mungu na kuwahudumia binadamu katika ulimwengu mamboleo, tayari kutoka kutangaza na kushuhudia furaha na faraja ya Injili kwa watu wa Mataifa. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru Mababa wote wa Sinodi kwa safari ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ambayo imewawezesha kutembea kwa pamoja na kwamba, sasa wanaweza kukua katika kumwabudu Mungu na huduma kwa jirani.

Papa Misa Sinodi
29 October 2023, 15:19