Tafuta

Papa Francisko Dominika tarehe 5 Mei 2024, amewatumia salam na matashi mema, waamini wa Makanisa ya Kiorthodox na baadhi ya Makanisa yanayoadhimisha Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2024. Papa Francisko Dominika tarehe 5 Mei 2024, amewatumia salam na matashi mema, waamini wa Makanisa ya Kiorthodox na baadhi ya Makanisa yanayoadhimisha Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2024. 

Sherehe ya Pasaka ya Bwana Kwa Makanisa ya Kiorthodox 2024: Ukweli wa Imani

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika tarehe 5 Mei 2024, amewatumia salam na matashi mema, waamini wa Makanisa ya Kiorthodox na baadhi ya Makanisa yanayoadhimisha Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 5 Mei 2024 kadiri ya Kalenda ya Julian. Kristo Mfufuka awakirimie amani na furaha ya kweli. Awafariji wale wanaoteseka kutokana na vita na wanaokabiliana na majanga makubwa ya maisha. Pasaka ni Ukweli wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Dominika ya Pasaka, Kanisa linamshangilia Kristo Mfufuka kwa “Sekwensia ya Pasaka” yaani “Kristo Pasaka yetu aliyechinjwa sadaka, tumaini la watu wake amefufuka na amewatangulia mjini Galilaya. Kadiri ya Mapokeo, wakati wa Pasaka, watu wanasalimiana kwa maneno “Kristo Amefufuka”, ili kulitukuza Fumbo la imani ambalo ni chemchemi ya furaha na matumaini yanayowawajibisha waamini ili kushiriki kikamilifu katika utume wao ulimwenguni. Sherehe na mashangilio ya Pasaka ndani ya familia hayana budi kujikita katika hija na utume kwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka. Kwa njia ya Kerigma, Kanisa linainjilishwa, ili kuendelea kuinjilisha.

Pasaka ni fumbo letu la wokovu.
Pasaka ni fumbo letu la wokovu.

Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, wote wamehesabiwa haki, kwa vile wamefufuka katika Kristo Yesu, wanapaswa kuyatafuta na kuyaambata yale ya mbinguni, ushuhuda wa imani tendaji. Kwa wale waliozaliwa upya kwa kuuvua utu wao wa kale, wataweza kuhesabiwa haki mbele ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuondokana na unafiki katika maisha yao kwa kuishi na kutenda mema na pale wanapotumbukia dhambini, wawe na ujasiri wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili hatimaye, wao pia waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wale wanaoteseka na kudhalilishwa kwa utupu; wanaokosa mahitaji yao msingi, watu wanaoishi katika upweke na uvuli wa mauti. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kwa upya wa maisha ndani ya Kristo Yesu, Wakristo wanaweza kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini, alama ya maisha mapya na ufufuo. Wakristo wawe na ujasiri wa kumwachia Kristo Yesu, nafasi ili aweze kuosha na kutakasa macho ya imani, ili kuona na kutenda vyema, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Mfufuka.

Pasaka ya Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti
Pasaka ya Kristo ni kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti

Kwa kuishi vyema Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha ya Bikira Maria aliyefuatana na Mwanaye Mpendwa katika Njia yake ya Msalaba, akateseka sana pamoja naye hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba bila ya kumwonea aibu! Ni Mama ambaye, moyo wake ulisheheni furaha isiyokuwa na kipimo, kwa Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yawawezeshe waamini kushiriki kikamilifu ili waweze kupyaisha maisha yao! Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa Makanisa ya Kiothordox na baadhi ya Makanisa ya Mashariki, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Dominika tarehe 5 Mei 2024, amewatumia salam na matashi mema, waamini wa Makanisa ya Kiorthodox na baadhi ya Makanisa yanayoadhimisha Pasaka ya Bwana, Dominika tarehe 5 Mei 2024 kadiri ya Kalenda ya Julian. Kristo Mfufuka awakirimie amani na furaha ya kweli. Awafariji wale wanaoteseka kutokana na vita na wanaokabiliana na majanga makubwa ya maisha.

Pasaka ya Bwana kwa Makanisa ya Mashariki
Pasaka ya Bwana kwa Makanisa ya Mashariki

Kwa upande wake, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, katika Ujumbe wake kwa Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2024 anasema kwamba hii ni Sherehe ya: Imani, upendo, matumaini, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kumbe, Fumbo la Pasaka ni sababu na kiini cha imani, furaha na matumaini ya Wakristo hapa duniani kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake Kristo Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumkirimia maisha ya uzima wa milele, mwaliko wa kudumisha upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliweza kugeuza ubaya kuwa ni chemchemi ya historia ya wokovu kwa watu. Ufufuko wa wafu ni kiini cha imani ya Kanisa na kwamba, ubaya hauna neno la mwisho katika maisha ya binadamu na kwamba, Ufufuko kwa Kristo Yesu umewafungulia waamini maisha ya uzima wa milele. Imani katika Fumbo la Pasaka ni udhihirisho wa ndani zaidi na wa wazi wa uhuru wa waamini, kielezo cha kuzaliwa upya kwa neema. Kama ufufuko wa Kristo Yesu ulivyo wazi kwa Kanisa la Kiorthodox hii ni nafasi ya uhuru wa ukweli ambao ni msingi, njia na hatima ya maisha ya Kikristo. Ufufuko wa Kristo Yesu na kielelezo cha uhuru wa pamoja kama watoto wateule wa Mungu katika uzima wa milele wa Ufalme wa Baba, wa Mwana na wa Roho Mtakatifu.

Pasaka ya Bwana
06 May 2024, 14:22