Tafuta

Dr. Paulo Kishumba, Kaka yake Askofu mkuu Protase Rugambwa amefariki dunia tarehe 27 Oktoba 2021 Jijini Mwanza na Maziko yake ni 2 Novemba 2021. Dr. Paulo Kishumba, Kaka yake Askofu mkuu Protase Rugambwa amefariki dunia tarehe 27 Oktoba 2021 Jijini Mwanza na Maziko yake ni 2 Novemba 2021. 

Dr. Paulo Kishumba, Kaka yake Askofu Mkuu Protase Rugambwa Amefariki Dunia

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu anapenda kutoa salam za rambirambi kwa Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Askofu mstaafu wa Jimbo la Kigoma, Tanzania kwa kuondokewa na Kaka yake Dr. Paulo Kishumba aliyefariki dunia Jumatano tarehe 27 Oktoba 2021 Jijini Mwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kuhusu kifo na ufufuko wa mwili. Kanisa lina amini na kutumaini kwa uthabiti kabisa kama vile Kristo Yesu alivyoteswa, akafa na kweli kutoka wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Yesu Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho. Ufufuko wa waamini ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Neno mwili, linamwelezea mtu katika hali yake ya udhaifu yaani kifo! Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu akiwa ameungana na viongozi na wafanyakazi wa Baraza lake, anapenda kutuma salam za rambirambi kwa Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Askofu mstaafu wa Jimbo la Kigoma, Tanzania kwa kuondokewa na Kaka yake mkubwa Dr. Paulo Kishumba aliyefariki dunia Jumatano tarehe 27 Oktoba 2021 Jijini Mwanza, Tanzania kutokana na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu linapenda kuungana na Familia ya Askofu mkuu Protase Rugambwa katika kipindi hiki cha majonzi mazito. Linamwombea Marehemu Dr. Paulo Kishumba ambaye ameacha watoto sita aweze kupata huruma ya Mungu na apumzike kwa amani! Ibada ya Misa Takatifu na mazishi inatarajiwa kuadhimishwa Jumanne tarehe 2 Novemba 2021 Parokiani Nyaishozi, Jimbo Katoliki la Kayanga, Tanzania!

Itakumbukwa kwamba, Dr. Paulo Kishumba alizaliwa tarehe 26 Agosti 1957 na ni mtoto wa kwanza wa familia ya Ta Prosper Iholana na Ma Immaculata Pancras. Dr. Kashumba aliipenda na kuithamini sana kazi yake, kiasi cha kujitahidi kuwahudumia wagonjwa, kwa upendo. Katika maisha na utume wake, alimwona Mtakatifu Francisko wa Assisi kuwa ni mfano wake wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa na maskini. Karama ya Mtakatifu Francisko, tayari ilianza kuota mizizi katika familia kutokana n ana nyayo alizoacha Ta Prosper Iholana ambaye alikuwa pia ni Mfranciskani. Alifurahi kumwona mtoto wake Francisko akifuata malezi na majiundo ya Kipadre na kwa sasa yuko Seminari Kuu ya Ntungano, Jimbo Katoliki la Bukoba. Mwenyezi Mungu akipenda, siku moja, atawekwa wakfu kuwa Padre kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Wengi wanamkumbuka Mwalimu Grace Basimwaki Kishumba aliyefariki dunia tarehe 18 Mei 2020 na kumwachia watoto sita! Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaungana na familia nzima ya Askofu mkuu Protase Rugambwa, kuomboleza msiba huu mzito. Tunamwombea faraja, imani na matumaini Ma Immaculata Pancras ili katika uzee wake, aweze kuupokea msiba huu kwa moyo mkuu, akiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele! Amina!

Tanzia Dr Paulo
29 October 2021, 17:00