Baba Mtakatifu Francisko akishiriki chakula cha usiku na maskini mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko akishiriki chakula cha usiku na maskini mjini Vatican. 

Ekaristi Takatifu ni shule ya upendo na ukarimu

Katika kiini cha adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kuna mkate na divai, ambavyo kwa maneno ya Kristo na kwa kumwita Roho Mtakatifu hugeuka kuwa Mwili na Damu ya Kristo. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati. Muujiza huu ni ishara ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre William Bahitwa. – Vatican.

UTANGULIZI: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu leo ikiwa ni Dominika ya 17 ya mwaka B wa Kanisa. Maandiko Matakatifu katika Jumapili ya leo yanaturudisha katika shule ya ukarimu, tuitafakari fadhila hii ianayoambatana na neema kubwa ya Mwenyezi Mungu kiasi cha kutenda maajabu, kutenda miujiza machoni petu pale tunapoiishi.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (2Waf. 4:42-44) Nabii Elisha analetewa matoleo ambayo ni mikate 20 ya shayiri na masuke mabichi ya ngano. Naye akiisha kupokea matoleo hayo anampa mtumishi wake na kumwambia awatayarishie watu mia moja wale. Mtumishi anashangaa kwa sababu chakula kile ni kidogo sana kwa idadi ya watu mia. Elisha kwa maneno ya Zaburi 132:15 anamwambia “watayarishie kwa kuwa Bwana anasema watakula na kusaza”. Na ndivyo ilivyokuwa.

Utume wa nabii Elisha, kama ulivyokuwa wa mtangulizi wake Eliya, ulikuwa ni wa kuamsha dhamiri ya waisraeli ambayo kwa kipindi hicho ilififishwa sana na imani kwa miungu Baali. Muujiza huu anaoufanya leo ni kuwafundisha waisraeli kuwa Mungu pekee ndiye anayeyashikilia maisha yao. Yeye ni mkarimu na anawafundisha wao pia kuwa wakarimu na kuwajali wahitaji. Hata kidogo kitolewacho kwa ukarimu na kinachotumiwa kwa mafaa ya wote huleta manufaa makubwa.

Somo la pili (Ef. 4:1-6) ni mahusia ya mtume Paulo kuhusu mwenendo uwapasao wakristo kadiri ya imani waliyonao. Anasisitiza juu ya fadhila za unyenyekevu, uvumilivu na kuchukuliana kwa upendo. Lengo ni kuuhifadhi umoja, umoja katika Roho Mtakatifu. Mtume Paulo anawaalika waamini katika jumuiya hiyo ya Efeso walinde umoja kwa sababu tayari imani yao ni moja na inawaleta pamoja, hali kadhalika tumaini lao ni moja katika umoja wa Utatu Mtakatifu. Mafundisho haya ya Mtume Paulo yanajijenga juu ya taalimungu yake kwa Kanisa, yaani Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo. Hali kadhalika jumuiya ya waamini ni mwili wa fumbo wa Kristo, nao ni mmoja japo una viungo vingi, vinavyotegemana na kukamilishana.

Injili (Yn. 6: 1-15) inaeleza muujiza ambao Yesu anaufanya. Anawashibisha watu zaidi ya 5000 kutoka mikate mitano na samaki wawili. Yesu mbele ya umati mkubwa, baada ya kuwa amewafundisha na kuwapa chakula cha roho, aliona pia hitaji la kuwashibisha kimwili. Yesu hashughulikii tu ustawi wa watu wake kiroho bali anashughulikia pia ustawi wao kimwili na ndiye aliyewafundisha kumwomba Mungu kwa ajili ya “mkate wa kila siku”. Yesu anaanza kwa kumuuliza Filipo mtume wake “tununue wapi mikate ili hawa wapate kula?” Naye Filipo anabaki katika hali ya kawaida bila kukumbuka aliyemuuliza swali ni nani na kwamba anao uwezo usio wa kawaida. Anatoa jibu kwa kuhurumia mfuko wao wa hazina akiona kwamba hata wakitoa fedha wao hazitafua dafu kwa idadi ile ya watu.

Katika mahangaiko hayo, mtume mwingine Andrea anaeleza kilichopo, mikate mitano ya shayiri na samaki wawili. Hata hivyo anaona ni kitu kidogo sana kwa idadi ya watu. Anasema “lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?” Kwa hakika vilikuwa ni kidogo kwa sababu kama aliyekuwa amebeba ni mtoto mdogo ni wazi isingekuwa mikubwa na hata samaki wasingekuwa wakubwa. Lakini pia haikuwa na ubora uliozoeleka. Waisraeli walikuwa wakulima wa ngano na mikate waliyokula ilikuwa ni ya ngano na si ya shayiri kama aliyokuwa nayo huyo mtoto. Hata hivyo Yesu anawaambia wawaketishe watu. Na kutoka mikate hiyo mitano na samaki wawili watu hao wakala hadi wakasaza na yakakusanywa mabaki vikapu kumi na viwili.

Mababa wa Kanisa kwa namna ya pekee Mwenyeheri Beda na Mtakatifu Agustino wanaona katika mikate mitano kiashirio cha vitabu vitano vya Musa, yaani Torati ambayo Yesu amekuja kuikamilisha. Samaki wawili ndio Maandiko ya Manabii na Zaburi yanayokamilishwa Yesu anapoyatwaa na kuyapa maana mpya, maana ya ukombozi. Mtakatifu Augustino anaongeza kuwa mitume wanapoitwaa mikate wanapoimega na kuwagawia watu ndio kuwafundisha kwa mamlaka ya Kristo na kama Kristo alivyoikamilisha. Muujiza huu pia ni kiashirio cha Fumbo la Ekaristi Takatifu, (Rej KKK 1335), Yesu anapotwaa mikate, anashukuru, anaimega na kuwapa wafuasi wake kwani ndivyo atakavyokuja kufanya anapoutoa mwili wake kama Sakramenti ya wokovu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, fadhila ya ukarimu ambayo kwayo leo tunaelekeza tafakari yetu, ni fadhila ambayo tunajifunza toka kwa Mungu mwenyewe. Mungu ndiye asili na chemichemi ya ukarimu.  Katika sura nyingi za ukarimu kati yetu binadamu, Maandiko ya leo yanatuonesha thamani ya kutoa kwa ajili ya wengine. Na hiyo ndiyo fadhila yenyewe ya ukarimu, yaani kutoka kilicho chako kwa ajili ya manufaa ya mwingine. Kutoa bila shuruti bali kwa upendo na kwa kujali ustawi wa mwingine. Kwa ukarimu mtu anaweza kutoa mali: fedha au vitu, lakini pia anaweza kujitolea mwenyewe muda wake, huduma yake na hata katika ulio wajibu wake kwenda zaidi ya wajibu akisukumwa na manufaa ya wale anaowatumikia.

Kitolewacho kwa ukarimu huongezewa neema ya Mungu. Na ni neema hii inayofanya ukarimu uonekane kama muujiza machoni petu. Ni kwa ukarimu Nabii Elisha alitwaa matoleo yaliyokuwa yake kama Nabii naye akayatoa kwa ajili ya watu ili watumie. Kwa neema ya Mungu inayoambatana daima na tendo la ukarimu, matoleo yale yakawatosha watu mia moja. Ni ukarimu huu uliomsukuma Yesu pia kuwaandalia chakula watu zaidi ya elfu tano kutoka mikate mitano na samaki wawili.

Kwa njia ya mitume wawili, Filipo na Andrea, Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanaleta pia mbele yetu tahadhari dhidi ya maadui wawili wa ukarimu. Adui wa kwanza ni kutanguliza hasara dhidi ya tendo la ukarimu. Filipo ndiye yule ambaye baada tu ya kuulizwa na Yesu aliwaza juu ya mfuko wao wa hazina, juu ya uchumi wao na kuona haiwezekani. Bila kubeza umuhimu wa  kulinda hazina binafsi tunaalikwa tukishinde kishawishi cha kuweka hasara kama kisingizio cha kutokuwa wakarimu. Kwa anayeishi kimahesabu na kupima kila kitu kimahesabu, kuwa mkarimu maana yake ni kugharimika na kufilisika. Maisha yenyewe yameonesha kuwa kinachoweza kumfilisi mtu sio ukarimu bali ni uchoyo na tamaa ya kujilimbikizia zaidi.

Adui mwingine wa ukarimu ni mtu kuona kuwa anacho kidogo sana kisichoweza kusaidia chochote. Ndivyo Maandiko Matakatifu yanavyomwonesha Andrea Mtume anayesema “mikate mitano na samaki wawili ni nini kwa watu wengi kama hawa?”  Katika hili aliwahi kutukumbusha Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa “ulimwenguni hakuna aliye maskini kiasi kwamba hana chochote cha kutoa kumsaidia mwingine na hakuna aliye tajiri kiasi ambacho hahitaji chochote kutoka kwa mwingine”. Daima kuna kinachoweza kufanyika, na kwa ukarimu neema ya Mungu hutenda maajabu.

Tuanze upya katika ukarimu; tuipokee changamoto ya kuishi kikarimu; tuelekeze upya mitazamo yetu katika ukarimu hata katika yale yaliyo madogo madogo kwa wahitaji wanaotuzunguka kila kukicha. Mt. Mama Tereza wa Kalkuta aliwahi kuambiwa kuwa utume wake wa kuwasaidia maskini na waliotupwa hautafika popote kwani watu hao ni wengi mno duniani na hawezi kuwafikia wote. Yeye alijibu kwa utulivu na tabasamu nitamsaidia yule mhitaji aliye karibu yako. Nasi pia hatuhitaji kuwatendea ukarimu dunia nzima bali yule aliye karibu yetu, ndiye “jirani yako”.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

28 July 2018, 08:29