Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVII ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu, chakula cha uzima wa milele. Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVII ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Kristo Yesu, chakula cha uzima wa milele. 

Kristo Yesu ni chemchemi ya ukarimu na upendo!

Mtume Paulo anawaalika wabatizwa wote katika umoja kwa mfano wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Fumbo la Ekaristi Takatifu katika Maandiko ya Mtume Paulo ni msingi wa umoja na mshikamano. Katika 1Kor. 10:17 anaandika hivi – kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi sote tulio wengi ni mwili mmoja, kwa maana sisi sote tunashiriki mkate mmoja.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Vatican.

Ndugu wapendwa katika mtandao wa Vatican News! Leo tunaanza kusoma somo la injili kutoka injili ya Yohani na somo hili huunganisha kwa karibu ekaristia na teolojia ya Kristo – Kristo ni nani.  Tulisikia jumapili iliyopita habari juu ya huruma kwa kundi la Mungu na haja ya kuwa na viongozi makini wa kuliongoza kundi sanjari na kuwapatia mahitaji yao msingi, yaani kwanza kabisa Neno la Mungu, mkate wa maisha ya uzima wa milele!   Jumapili ya XVII, Yesu anawalisha wenye njaa. Huu muujiza unakuwa sasa katekesi juu ya taalimungu ya Kristo Yesu, Mkate wa maisha ya uzima wa milele, chemchemi ya wema na ukarimu wa Mungu usiokuwa na mipaka.Yesu anaona kundi, wote wana njaa, anataka kuwapa chakula. Filipo anashtuka. Denari mia mbili hazitoshi kwa lo lote.

Filipo anawakilisha hali yetu ya kibinadamu, hasa wakati imani yetu ikiwa majaribuni. Hasa tunapotaka kutatua mambo peke yetu.  Hata Andrea pia – ni nini hii kwa watu wote hawa? Hata hivyo imani ya Andrea inavuka ile mipaka ya kibinadamu. Anamwona mtoto mwenye mikate mitano na samaki wawili. Anamwonesha Yesu, akitambua kuwa anaweza kufanya muujiza. Nabii Elisha naye anaonesha wasiwasi huo katika somo la kwanza – nitawekaje kiasi hiki kwa watu mia moja? Katika somo hili la kwanza twasikia habari ya chakula kwa ajili ya rafiki zake Elisha. Njaa inatajwa, na hii inaandaa njia kuonesha jinsi Mungu anavyowalisha na kuwaokoa watu wake. Aidha kinachozingatiwa hapa ni kile chakula cha kiroho zaidi ya chakula cha kimwili.

Anachofanya Yesu leo, kuwapa chakula wenye njaa ni mwaliko wa kuvuka mipaka yetu, wasiwasi zetu n.k. na kutupeleka kuamini katika miujiza ya Mungu. Mara nyingi mazingira na namna ya kutatua matatizo huweza kuonekana kama kikwazo – je hata mimi ninaweza kufanya hivyo? Yesu anatualika leo kuona kuwa inawezekana. Yesu anamuuliza Filipo tutanunua wapi mikate (Yoh. 6:5)? Yesu alijua vizuri mipaka ya kibinadamu ya Filipo. Mitume waliona shaka. Je itawezekana? Yesu anawaalika na kutualika pia leo kufanya kitu (Yoh. 6:6 – Yesu alijua wazi atakalofanya) na kadiri iwezekanavyo kuwapa chakula, kutumia kile kilichopo, tukiwa na imani katika uweza wake. Hakika hapa yahitajika ukomavu wa kiimani. Peke yetu hatuwezi kufanya lo lote. Andrea alitambua uwezo wa Yesu na anamtambulisha kwake mtoto mwenye mikate mitano na samaki wawili.

Hatuna budi sasa sisi tunaosikia Neno hili siku ya leo kuona mahitaji halisi ya taifa la Mungu. Kwanza kujua ni ipi njaa ya kweli ya ulimwengu. Dunia yetu na watu wake wanahitaji nini leo. Hata mimi binafsi – ninahitaji nini? Na pia ninaweza kufanya nini? Na baada ya kujua hatuna budi kuona namna ya kuimaliza njaa hii. Je tutaishia tu kulalamika bila kufanya kitu? Mara nyingi hata tunacholalamikia hatukijui vizuri. Hatuna budi kutafakarishwa na mwanafalsafa Socrates anayetuambia – mtu ambaye hana tafakari ya maisha yake hafai kuishi. Ni sawa na mtu mfu.

Tunamshukuru Mungu kwamba, mwanae Yesu Kristo anakuwa meza ya chakula na kutuliza njaa yetu. Anajitoa mtu mzima. Ila katika upendo wake kwetu anatualika kushikiriki katika kuwa na kitu. Angalia katika harusi ya Kana – divai ilitengenezwa toka mabirika yaliyojazwa maji na wale watu. Kutoka katika kitu fulani Yesu anafanya kitu kizuri zaidi. Ni wajibu wa mitume na sisi pia  kuandaa mazingira ambayo Yesu anaingilia kati. Hata katika injili ya leo tunona Andrea anamtambua mtoto mwenye kitu. Muujiza ni tendo la pekee na lisilokuwa la kawaida analofanya Mungu na sisi kwa ajili yetu. Katika Mt. 9:29 tunasoma neno hili – akawagusa macho, akasema, mtendewe mlivyosadiki. Kabla ya hapo wale waliokuwa vipofu waliomba huruma yake na Yesu anawauliza je mnasadiki kwamba naweza kufanya hayo? Utayari wao na imani yao inawaponya.

Tutafakarishwe na mfano wa mama aliyekuwa amelemaa miguu baada ya ajali ya gari. Akawa hawezi tena kutumia miguu yake bila magongo. Akiwa anapika jikoni chuba cha chini, akagundua kuwa chumba cha juu alikomlaza mwanawe kimeshika moto. Alichofanya ni kusahau ulemavu wake, akaweza kupanda darini bila magongo na kumwokoa mtoto wake aliyekuwa katika hatari ya kufa.  Na tunaambiwa kuwa tangu siku hiyo alipona na ulemavu wake. Ndicho anachofanya Yesu leo, kujitoa mzima na kuzima njaa ya watu wale. Nasi hatuna budi kufanya hivi.

Upendo huu maana yake ni nini kwetu? Huu ni ufunuo wa Kristo na fumbo lake. Mitume na watu walikuwa bado hawajamwelewa Kristo. Ila katika muujiza huu anajifunua kama mwokozi na zaidi tunaona anachofanya kikifanana na alichofanya katika karamu ya mwisho.  Alama hii ni mwaliko katika kumtambua Kristo na uweza wake, wa ukuu wake wa wokovu na mwaliko wa kukutana naye katika neno lake na katika ekaristia. Kundi linamtafuta, wana njaa, naye anawalisha. Anaona mahitaji ya watu na kutenda

Hii dhamira ya Kiekaristi inatawala masomo yetu ya leo na jumapili nne zifuatazo. Tunashangaa kuona jinsi mkate huu unavyoshibisha wenye njaa. Ukipokelewa kwa imani, hulisha imani yetu, kwamba anayeshiriki ekaristi takatifu aweza kusema anapata kile alichohitaji. Ni nini zaidi kimebaki? Hatuna budi kumshukuru Mungu.  Katika somo la pili, Mtume Paulo anawaalika wabatizwa wote katika umoja kwa mfano wa fumbo la utatu mtakatifu. Ekaristia katika roho ya mtume Paulo ni msingi wa umoja na mshikamano. Katika 1Kor. 10:17 anaandika hivi – kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi sote tulio wengi ni mwili mmoja, kwa maana sisi sote tunashiriki mkate mmoja.

Tumsifu Yesu Kristo.

 

26 July 2018, 15:50