Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVI ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVI ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa 

Kristo Yesu ni mfano wa mchungaji mwema, anayeona, hurumia na kuamua kutenda kwa haraka!

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya XVI ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa ni mwaliko wa kuiga mfano wa Kristo Mchungaji mwema, aliyewaona watu wake, akawahurumia kwani walikuwa kama Kondoo wasiokuwa na mchungaji, akaamua kuwafundisha. Hiki ni kielelezo cha uaminifu, ulinzi na usalama, urafiki, sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Vatican.

Ndugu wapendwa, jumapili hii twaweza kuiita jumapili ya huruma kwa kundi. Ni mwaliko wa wajibu wa kikristo. Ni mwito wa kuwa tayari kuhudumia kikristo. Masomo yetu ya leo yanatuonesha hali hiyo. Katika somo la kwanza – tunasikia kuwa sababu ya viongozi wakatili, taifa la Mungu limepoteza dira. Ila mpango wa Mungu wa ukombozi ni tofauti kabisa na mpango wa mwanadamu. Hivyo Mungu anamtuma mjumbe wake mwaminifu, nabii Yeremia, kutangaza kwamba Mungu hataacha mpango wake wa mapendo na kwamba anawaandalia watu viongozi wapya. Nabii Yeremia alibaki mwaminifu kwa Mungu kuliko kuwafuata viongozi wabadhilifu. Sisi twaitwa kondoo kwa vile Mungu ni mchungaji na hapa kondoo wanapata maelezo sahihi na hupata nafuu ya ulinzi na maongozi ya Mungu. Uaminifu, ulinzi na urafiki ni alama za mchungaji  mwaminifu. Mpango huu ulikamilika kwa ujio wake Kristo.

Katika somo la pili, tunaona kuwa uwepo wa Kristo, huondoa migawanyiko yote ya kibinadamu. Paulo anajiita mtumwa wa Kristo. Katika Injili – twaona kuwa Yesu anataka kujitenga kidogo na watu ili apate muda wa kusali na kupumzika. Lakini watu wanamfuata. Jambo hili linamgusa sana. Kwa watu hawa wenye njaa na kiu ya ukweli, yeye anawapatia Neno la uzima. Yesu anaona kundi lenye njaa na kiu na anachukua uongozi wa hilo kundi na kuwafundisha, tena kwa mpangilio na kutuliza njaa na kuwapa ulinzi kamili. Mchungaji mwema yuko makini  na kufanya kazi yake kwa uaminifu.

Ndugu wapendwa, tunaona kuwa Mungu anajitoa kwa upendo na matokeo yake ni uzima. Na ikiwa watu wanajibu,  matokeo yake ni wokovu na uzima pia. Wale wanaoguswa na upendo huu, hutangaza huo wokovu. Ndicho alichofanya Yesu, alipowaaminisha utume na akawatuma ulimwenguni kwenda kuhubiri habari njema. Katika injili ya Marko ni mahali pekee hapa wale 12 wanaitwa mitume, yaani waliotumwa. Pengine pote wanaitwa wafuasi, yaani wanafunzi. Hivyo yule aliyetumwa anakuwa sehemu ya wokovu wa watu kwa kutangaza hiyo habari njema. Huu ndio wajibu wetu leo. Kuwa wachungaji wema kama alivyokuwa Kristo, mchungaji mwema. Hii itawezekana tu kama tutakaa pamoja na Kristo na kujazwa na roho wake.

Nabii Yeremia anatupa changamoto kubwa leo tunaposikia tena Neno la Mungu na kutafakari nafasi yetu katika kutangaza hiyo habari njema. Nabii Yeremia hakutishwa na viongozi dhalimu, ila alimtumainia Mungu na akakemea waziwazi maovu ya viongozi wabovu.  Bwana wetu Yesu Kristo anatupa changamoto kubwa zaidi leo kama wafuasi wake. Anatoka katika hali yake ya ubinafsi na kuwahurumia wahitaji. Tunapoangalia hali zetu, nchi yetu, ulimwengu wetu wa leo na hali zetu na mitindo yetu ya maisha tunajiuliza je tunatakiwa kufanya nini? Hatuna budi kujiuliza ni kipi kilio cha watu wetu leo? Ni kitu gani hasa tunahitaji kidini, kisiasa, kiuchumi, kimaadili n.k? Ni mambo gani ambayo tunatakiwa tuyape kipaumbele ili huruma ya Kristo ionekane wazi? Je tunajitenga na wenye shida na mahitaji zaidi yetu na kusema shauri yao? Yesu hakufanya hivyo. Watumishi waaminifu wa Mungu hubaki upande wa Mungu hata pale wanapojikuta katika mazingira magumu ya kutoa ushuhuda.

Upendo kwa Mungu na moyo wa ushuhuda huwafanya wajisahau katika mahitaji yao binafsi kama kupumzika na kujitoa kwa ajili ya wengine. Inaonekana wazi kuwa Yesu alichoka na anaona wafuasi wake wamechoka. Wanataka kujitenga ili wapumzike. Lakini mahitaji au njaa na kiu ya watu inakuwa kubwa na Yesu anawahurumia. Anawalisha Neno la uzima. Na anachofanya kinatuliza njaa yao. Wanapata wokovu na uzima. Yesu hatoi ziada bali anajitoa mwenyewe na anawataka wafuasi wake wafanye hivyo hivyo. Nasi tukafanye hivyo. Jambo la kufurahia hapa na kuwa ni changamoto kwetu sote ni kuwa Yesu anatuwajibisha sisi katika kutenda. Walipomwendea na kumlilia shida aliwambia watende.

Yesu anaona ndani yetu uwezo mkubwa na hapa hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutupa wajibu huo mkubwa. Ni dhamana imewekwa mbele yetu. Yesu anawaambia mitume wawape watu chakula. Tukitaka kuenzi neno hili la Mungu wakati wetu huu hatuna budi kufanya kama walivyofanya mitume. Walitimiza agizo lile la Yesu kwa matendo. Kardinali Manning anasema, utakatifu hupatikana katika kuyatenda yale ya kawaida katika hali isiyo ya kawaida.

Wageni katika Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo huko London wanaweza kusikia hata sauti ya mnongonezo inayofanywa au na mwongoza wageni au na mtu aliyenena neno fulani kwa sauti ndogo. Hii inawezekana kama ukiweka sikio lako ukutani, kwamba waweza kumsikia mtu anayeongea upande wa pili wa kanisa hata kama tamko likitoka kwa sauti ya chini kabisa. Wakati fulani fundi viatu alisikia akimwambia mchumba wake wa kike kuwa hataweza kumuoa kwa vile hakuwa na fedha ya kununua ngozi na biashara yake haikuwa inaenda vizuri. Yule binti alitoa machozi baada ya kusikia taarifa hiyo mbaya. 

Mtu mmoja aliyekuwa umbali wa mita 66 na aliyekuwa ameweka sikio lake ukutani, alisikia habari hiyo ya kusikitisha. Akaamua kutoa msaada ili kuokoa mapenzi ya vijana wale. Huyu mtu akaamua kumfuatilia yule kijana alipotoka pale kanisani na kufahamu mahali alipoishi. Huyu akanunua ngozi na kumtumia yule kijana lakini bila kujitambulisha. Yule kijana alifurahi sana na biashara yake ikaanza tena kushika kasi na akaweza kuoana na yule binti rafiki yake. Kwa muda mrefu alitaka kufahamu ile zawadi ilitoka kwa nani na ilichukua muda mpaka alipofanikiwa kufahamu kuwa ile zawadi ilitoka kwa waziri mkuu wa Uingereza William Gladstone. Sisi hatuna budi kujiuliza tunasikia nini kila siku, tunajua nini kuhusu wajibu wetu wa kikristo na pengine tumefanya kitu gani cha pekee mpaka sasa. Mungu anatuita daima tutende na nguvu hivyo imewekwa ndani yetu.

Tumsifu Yesu Kristo.

21 July 2018, 15:54