Shuhudieni upendo wa Mungu kwa njia ya ukarimu!
Na Padre Joseph Peter Mosha. - Vatican.
Dunia mamboleo inamwelekeza mwanadamu katika utetezi wa uchoyo wake. Sababu ya sumu ya ubinafsi na kujijali mwanadamu amekuwa stadi katika kutafuta maneno ambayo yatautetea uchoyo wake. Mambo haya hujionesha katika kujiridhisha kwa kujihudumia mambo ya msingi ambayo ni mahitaji ya kawaida ya mwanadamu; mfano maji, chakula, malazi na mavazi. Wengi wetu tunafunikwa na fikara za kibinadamu ambazo zinatetea kujitafutia mtu binafsi mahitaji haya kwa nafasi ya kwanza ndipo uinue macho yake na kumtazama mwingine. Wakati mwingine ubinafsi huu unatufikisha katika hatua ya kutaka hata mahitaji fulani ambayo hayahitajiki au kumpatia mtu ziada, na mmoja yupo tayari kutupa jalalani bila kumjali Lazaro anayeteseka pembeni yake. Tunu ya ukarimu inaharibiwa na ubinafsi wetu. Tunasahau kwamba hatua ya kwanza na muhimu katika ukarimu ni upendo kwa jirani.
Ukarimu unaojificha katika upendo ni tendo la kimungu. Hali hii haiangalii kile kinachotolewa bali ni moyo wa kushirikisha kile ulichonacho. Moyo wa kushirikisha ulichonacho kwa ukarimu inawezekana pale mmoja anapokuwa tayari kujifunua kwa wengine na hili linaelezewa katika upendo wa kimungu Agape. Ukarimu unaojifunua katika Upendo unachagizwa na uwepo wa Mungu na nguvu zake na pia ukarimu wake kwetu. Katika masomo ya leo hususani Somo la Kwanza na Injili hali hiyo inaonekana. Nabii Elisha aliamini katika ukarimu wa Mungu na hivyo kutumaini katika kuwashibisha watu wengi kwa chakula kidogo. Hali kadhalika na katika Injili Kristo alilisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano ya shayiri na samaki wawili.
Kinachotupatia fundisho ni uwepo wa Mungu katika ukarimu huo. Nabii Elisha aliamini katika uwezo wa Mungu kuwashibisha watu mia kwa mikate ishirini ya shayiri na masuke mabichi. Muujiza wa Mungu unatendeka kwa watu wote kutosheka. Kristo katika Injili “aliitwaa mikate, akashukuru akawagawia walioketi; na kadhalika wale samaki kwa kadiri walivyotaka”. Kitendo cha kushukuru Mungu tayari kilimkaribisha Mungu na kumfanya awe mwezeshaji wa kutosheleza wote. Ukaribisho wa Mungu katika tendo la ukarimu linamkaribisha ndugu yako na kuwa sehemu ya hitaji lake. Hili litamfanya mmoja kuona mahitaji yake ya msingi ni mahitaji ya watu wote na hivyo kumfunua kuweza kutafuta na kuwahudumia wote.
Mahitaji ambayo binafsi nayaona ni ya msingi na ya muhimu yapo pia kwa mwenzangu. Hali ya kutaka furaha, faraja na kushibishwa na hitaji la binadamu wote. Katika hali ya umoja mwanadamu atafanikiwa kuitatua hali hii kwani umoja huo utawashirikisha wote katika kutafuta suluhisho kwa wote. Methali ya lugha ya Kiswahili inatuambia “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu”. Kujitoa kwa ajili ya wengine kunawaridhisha wote kwani kila mmoja anapojitoa kwa ajili ya wengine kwa hakika sote tutashibishana. Kitendo cha ukarimu wa Kristo kinatufundisha hilo. Mmoja asidharau kipaji chake au kiwango alichonacho. Muhimu ni kujitoa katika hali ya ukarimu hapo Mungu atawezesha.
Kutumia vema vipawa tunavyopewa na Mungu ni tendo la shukrani kwake na hali hiyo inamkaribisha Mungu na kuwezesha kipawa chako kuwa faida ya wote. Neno Ekaristi lina maana ya shukrani. Hivyo ushiriki wetu wa Ekaristi Takatifu unatuunganisha na Kristo aliye chemchem ya shukrani zetu kwa Mungu. Chakula hiki ni kichocheo kwetu kwa ukarimu wetu ambao unatoka kwa Mungu. Ekaristi Takatifu inatuimarisha katika “diakonia”, yaani kuhudumiana sisi kwa sisi, na “koinonia”, yaani maisha ya umoja. Hivyo Ekaristi Takatifu ni zawadi kutoka mbinguni kwa ajili ya kustawisha ukarimu wetu kwa wenzetu.
Hali ya ubinafsi na uchoyo inachagizwa na kutokuwa na imani thabiti na utegemezi kwa Mungu. Mwanadamu anajidanganya katika kujihangaikia binafsi na kuwaacha wengine wakisumbuka lakini mara nyingi huishia katika hali ya msongo wa mawazo. Uzoefu unaonesha watu wengi wanaojifungia ndani ya mioyo yao wanakosa amani na wengine. Hii ni uthibitisho wa ukosefu wa hali ya kimungu ndani ya uchoyo na ubinafsi. Yeye anayesongwa na uchoyo na ubinafsi anaihasi hali yake halisi. Kwa asili Mungu amemwumba mwanadamu kushirikiana na wengine na kifungo cha huo ushirikiano ni Yeye mwenyewe. Mungu anatufumbulia katika fumbo la Utatu Mtakatifu sana haiba hiyo ya ushirikiano unaodadavuliwa na ushirikiano wa nafsi tatu za Mungu.
Mtume Paulo katika somo la pili anatupatia wito: “Mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa”. Wito wetu ambao tumepewa na mwenyezi Mungu ni kumjua yeye katika wenzetu, kumpenda yeye katika wenzetu, kumtumikia yeye katika wenzetu na mwisho kuungana naye juu mbinguni. Mtume Paulo anatupatia nyenzo akisema: mwenende “kwa unyenyekevu wote na upole”. Kinyume cha unyenyekevu na upole ni majigambo na ukatili. Ni hali ya mmoja kujitafuta umaarufu na nguvu; mwanadamu kutafutia umaarufu bila kuwa na huruma kwa wengine. Mtume Paulo anaendelea kutuambia: “Kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo”. Hali ya kuutambua udhaifu wa mwingine na kunuia kumuimarisha na kurudi katika hali njema. Hii ni hali inayosababishwa na upendo wa kimungu, upendo ambao unaangalia utu wa mtu na hadhi yake mbele ya Mungu bila kuambatanisha udhaifu unaofunika haiba hiyo. Hivyo katika hali hii bidii hufanyika kuuondoa udhaifu unaoifunika haiba njema ya ndugu yako.
Mtume Paulo anamalizia kwa kusema: “mkijitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani”. Umoja wa Roho Mtakatifu ndiyo unaviunganisha viumbe vyote na kuwafanya kitu kimoja. Umoja huu ndiyo chachu ya undugu wetu wa kikristo. Katika Roho Mtakatifu uwepo wa Mungu unakuwepo katikati yetu. Maagizo ya mtume ni kujenga umoja katika Roho Mtakatifu. Mungu awe chanzo cha umoja wetu. Kwa njia hiyo tunaihifadhi amani. Haya ndiyo maisha ya kikristo yanayoshuhudia uwepo wa Mungu katika jamii ya kikristo.
Jamii mambo leo inayoweka ukinzani katika uwepo wa Mungu unamgawa mwanadamu katika sehemu mbili na matokeo yake ni ukosefu wa amani. Imani na maisha ya kawaida vimetengwa. Yale mmoja anayoyasikia katika mazingira ya imani hayapati nafasi kati mazingira ya maisha ya kawaida. Unduminakuwili huu (duality) kwa mwanadamu una athari kubwa sana katika maisha yake kwani Mungu anakosa nafasi katika maisha ya kawaida ya mwanadamu. Kwa mantiki hiyo vigezo vya ukarimu wetu na upendo wetu kwa wenzetu vinapambwa na hisia za kidunia tu na aghalabu kuiona agape kati ya watu. Unakuwa ni upendo wa “nipe nikupe”. Namna hii ndiyo inatuhalalisha katika uchoyo na kuendelea kuleta mafarakano kati ya wanadamu. Kila nilichonacho ni changu na nitakupatia nitakavyo na kama kitanisaidia kunitukuza zaidi kibinadamu. Wewe kama huna utajijua mwenyewe.
Leo Kristo anatuambia “waketisheni watu” akitaka tuwapatie sisi chakula. Haya ni mahitaji ya wenzetu. Mungu ameweka vipaji mbalimbali ndani mwetu anataka tuwahudumie hao ambao tayari amewaketisha. Msukumo huo wa kiimani rohoni mwetu uonekane katika utendaji wetu wa kila siku kwa matendo yetu ya huruma. Tutambue kuwa ukarimu wa kweli unajifunua katika upendo thabiti.