Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili
Padre William Bahitwa. - Vatican.
UTANGULIZI: Kanisa kwa tabia yake ni la kimisionari, ndivyo unavyofundisha Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika hati yake juu ya kazi za kimisioni za Kanisa (AG. 2). Asili ya tabia hii ya kimisionari ni Mungu Baba mwenyewe ambaye katika mpango wake wa ukombozi daima amewachagua watu, akawaita na kuwatuma. Ndivyo pia katika utimilifu wa nyakati alivyomtuma ulimwenguni Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Katika dominika hii ya 15 ya mwaka B wa Kanisa Maandiko Matakatifu yanatualika tuutafakari wito huu wa kimisionari katika Kanisa: namna ya kuendelea kuupokea, kuuishi na kuutekeleza katika nyakati zetu kadiri ya mpango wa Mungu wa wokovu kwa ulimwengu mzima.
Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Amo. 7:12-15) Kipindi cha nabii Amosi kilikuwa ni kipindi ambacho Israeli ilikuwa inafurahia ustawi na maendeleo ya kiuchumi. Lakini ustawi na maendeleo haya hayakwenda sawa na ustawi katika uchaji wa Mungu na katika maadili. Amosi anaitwa na kutumwa katika mazingira haya ili awarudishe wana wa Israeli katika uchaji safi kwa Mungu na maisha yenye adili. Katika kuhubiri haya, Amosi anapata upinzani kutoka kwa Amazia, aliyekuwa kuhani katika madhabahu ya mfalme, na kutoka kwa mfalme mwenyewe Yeroboamu.
Somo letu la kwanza leo linaanza hapa ambapo Amazia anamfukuza nabii Amosi. Amosi anajibu kwa kueleza chanzo cha utume wake wa unabii. Anasema hakuwa nabii wala hakuwa mwana wa nabii, ni Bwana aliyemtoa katika kazi yake ya ukulima akamwita awe nabii. Naye anaitekeleza kazi hiyo ya Bwana kwa kibali na mamlaka hayo aliyopewa naye. Ni wito wake unaompa mamlaka, sio elimu, sio mfumo, siyo wingi au uchache wa wafuasi, sio utajiri au umasikini bali ni wito kutoka kwa Mungu.
Somo la pili (Ef. 1:3-14) ni utenzi wa sifa na kumtukuza Mungu. utenzi huu unawezekana ulikuwa ni sala ya jumuiya alikohubiri Mtume Paulo, sala ya shukrani kwa Mungu kwa neema zake anazowajaliwa watu wake. Katika sala hii mwombaji anamshukuru Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Anashukuru Mungu Baba kwa upendo wake mkubwa na kwa kuwachagua wawe watu wake tangu hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu. Anamshukuru Mungu Mwana kwa sababu kwa njia yake amepata ukombozi na maondoleo ya dhambi. Anamshukuru Mungu Roho Mtakatifu kwa sababu amemtia muhuri wake na kumfanya mrithi katika milki ya Mungu kwa sifa na utukufu wa Mungu mwenyewe.
Somo hili linakuza sababu za mwanadamu kumshukuru Mungu maishani. Linaonesha ni mengi mangapi mwanadamu aliyonayo ya kumshukuru Mungu tena si katika yale ya kila siku ambayo huenda mwanadamu angeyatamani zaidi bali katika yale ya milele yanayogusa undani wa uwepo wake kama vile ukombozi, maondoleo ya dhambi na urithi wa ufalme wa Mungu.
Injili (Mk. 6: 7-13) Yesu anawatuma mitume wake kwenda kuhubiri. Anawatuma waende wawili wawili na anawapa masharti ya kufuata huko waendako ili waweze kutekeleza vema kilicho mbele yao. Katika masharti hayo anawazui kuchukua vitu vya njiani, anawazuia kubeba chakula na pesa na anawazuia kuhama hama kutoka nyumba moja hadi nyingine isipokuwa kama wanafukuzwa. Badala yake anachowapa ni uwezo dhidi ya pepo wachafu.
Anapowatuma katika jozi, wawili wawili, anawaonesha kuwa utume kwa tabia yake si kitu binafsi bali una tabia ya kijumuiya. Unahitaji daima kutekelezwa kwa kusindikizana, katika ushirikiano, katika kushirikishana na katika kuunganisha nguvu na karama ambazo Yeye mwenyewe anamjalia kila anayemtuma. Na tena japokuwa Yeye anamwita kila mmoja peke yake, daima anatuma kama jumuiya: “Enendeni”.
Anapowakataza kubeba vitu vya njiani: mkoba, kazu mbili, chakula na pesa kamwe hamaanishi kuwa vitu hivyo haviitajiki kwa anayetumwa. Kwa waisraeli walikwisha elewa tayari kuwa walawi hawakupewa eneo na hawakuwa na mashamba, ridhiki yao ilipatikana madhabahuni walipohudumu. Hawa pia Yesu aliwatuma wakapate mahitaji yao kwa hao wanaokwenda kuwahudumia. Hii pia ni ili wajikite kikamilifu katika utume bila kusongwa na mahitaji mengine. Anawapa nguvu ili wakapambane na uovu na ujumbe wanaobeba ni mwaliko watu watubu kwa kuwa ufalme wa Mungu umekaribia.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu leo yanaturudisha kwanza kwenye asili ya utume na kutuonesha kuwa asili ya utume ni Mungu mwenyewe. Ni Mungu anayechagua, anayeita na kutuma. Hakuna anayejitwalia utume isipokuwa yeye aliyeitwa na Mungu. Waraka kwa Webraenia unaeleza “hapana mtu ajiwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu kama vile Haruni” (Ebr. 5:4). Ni katika msingi huu mara nyingi tunapata shida kuelewa ni nini asili ya utume ya makundi na watu binafsi wanaoibuka kila kukicha na kujibandika vyeo ya utume, unabii, uchungaji na hata uaskofu.
Utume si pekee tu kuwa na uwezo wa kufafanua mambo hadharani au kuwa na uwezo wa kukusanya umati bali utume unatokana kwanza na kuitwa na kutumwa kama ambavyo Mungu amefanya tangu enzi na enzi. Tafakari ya kina juu ya msingi na asili hii ya utume ni msaada mkubwa katika kipindi hiki tulichomo ambapo waamini wengi wanasongwa na kasumba ya kutangatanga kiimani.
Mungu anaita kwa utume kwa sababu tangu kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu alikwishawachagua watu wake na kuwaweka ili wawe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo (Ef. 1:4). Huu ndio wito wa utakatifu ambao ndio wito wa kwanza ambao kila mmoja wetu ameitiwa. Tumeitwa ili tuishi kitakatifu na ili tuufikie utakatifu.
Kumbe wajibu wa kwanza wa yeye anayetumwa na Mungu ni kuwasaidia na kuwaongoza wale ambao tayari Mungu alikwishawachagua ili waufikie utakatifu. Huu ndio wajibu wa mtume na huu ndio wajibu wa utume wa kanisa zima, utume ambao kwa tabia yake ni wa kimisionari. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika mafundisho yake juu ya utume wa kimisionari wa Kanisa, anatualika tuuangalie umisionari si tu katika kupeleka Habari Njema kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine. Anatualika katika nyakati zetu hizi kuuangalia umisionari kama kupeleka Habari Njema si tu katika mahali bali katika hali mbalimbali za maisha hata ndani ya mahali pamoja. Umisionari uziingie hali, umisionari upenye katika mazingira ya watu katika undani wake, umisionari usibaki juu juu tu bali uguse nyanja zote za maisha ya mwanadamu kwa sababu ni katika nyanja hizo mwanadamu anaishi kumbe zenyewe zizipojengewa mazingira ya utakatifu haziwezi kuwa na msaada kwa mwanadamu anayeziishi kuufikia utakatifu. Katika mausia yake ya kitume Africae Munus yaani “Dhamana ya Afrika” aligusia hali tatu ambazo ni: Elimu, Afya na Mawasiliano (rej. AM 134-146). Lakini si hizo pekee. Kuna ulimwengu wa siasa, ulimwengu wa uchumi, ulimwengu wa michezo na kadhalika ambapo bado kuna harakati za kimisionari zinahitajika.
Tuuombee leo utume wa umisionari wa Kanisa na tuwaombee wajumbe wake mbalimbali walioitwa na Mungu kuutekeleza utume huo ndani ya kanisa na kwa jina la Kanisa. Tuupokee pia mwaliko wa kutegemeza kazi ya kimisionari ya Kanisa, kwanza kabisa kwa kushiriki utume huo na pia kwa kuuwezesha kadiri ya majaliwa mbalimbali ambayo Mungu amemjalia kila mmoja wetu.