Tafuta

Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho ni sehemu ya mafundisho tanzu ya Kanisa. Bikira Maria alipalizwa mbinguni mwili na roho ni sehemu ya mafundisho tanzu ya Kanisa. 

Bikira Maria amepalizwa mbinguni: roho na mwili!

Bikira Maria alishiriki kikamilifu katika mpango wa wokovu wa binadamu kwa njia ya imani yake na utii wake kama wanavyofundisha Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Alitamka ndiyo yake kwa niaba ya binadamu wote. Kwa utii wake amekuwa Eva mpya, mama wa walio hai!

Na Padre Joseph Peter Mosha. – Vatican.

Sherehe ya kupalizwa mbinguni mwili na roho kwa Mama yetu Bikira Maria ni hitimisho na kutawazwa kwa ufuasi wake uliotukuka katika safari ya Ukombozi wetu iliyotimizwa na mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Ufuasi wake huu unafunuliwa na “ndiyo” yake kwa mapenzi ya Mungu, tendo ambalo limeturudishia tena hadhi ya kuwa wana warithi pamoja na Mwana, hadhi ambayo tuliipoteza kwa sababu ya dhambi. Bikira Maria ni alama ya uwepo na utendaji wa Mungu katika maisha yetu ya ufuasi.

Kwa Sakramenti ya Ubatizo mwanadamu hufanywa kuwa mwana mrithi wa Mungu. Hadhi hiyo ni matokeo ya utendaji wa Roho Mtakatifu ndani mwetu. Hapa tunafanyika kuwa wana wa Mungu katika Mwanaye mpenzi. Ni Sakramenti ambayo inatuunganisha na upendo wa Utatu Mtakatifu. Hapa tunaupokea uwepo wa Mungu na utendaji wetu, utendaji ambao hufunuliwa kwetu kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo na kuwezeshwa kwetu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Utendaji huu wa Roho Mtakatifu unafanyika pale tunapokuwa tayari kuiruhusu nguvu ya Mungu kutenda kazi ndani mwetu. Mwenyezi Mungu hatulazimishi kuingia katika hali hiyo bali anatualika kila mmoja kuwa tayari na kufungua mlango ili aingie. Bwana asema, “tazama nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, name nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami” (Uf 3:20). Hivyo safari yetu ya kufanyika wana wa Mungu haitujii kama shinikizo. Tunu ya uhuru wetu wa kibinadamu haiaribiwi au kufujwa.

Hadhi yetu ya kuwa wana wa Mungu inatuingiza katika ufuasi wa Mungu. Hii inadhihirishwa na utendaji wetu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu anakuwa sehemu muhimu ya uwepo wetu na nguvu ambayo inatenda ndani mwetu na kujidhihirisha katika matendo yetu ya kiimani na kimaadili. Yeye anayefanyika mwana mrithi wa Mungu anaunganisha sehemu muhimu ya uwepo wake na Mwenyezi Mungu na hivyo Mungu anakuwa yote katika yote.

Mama yetu Bikira Maria ni ishara na kielelezo cha uwepo huu wa Mungu. Ni mfuasi nambari moja ambaye anatuelekeza katika kicheza vema nafasi yetu ya ufuasi. Bikira Maria anaitikia wito wa Mungu katika utii. Tukio la kupashwa habari kuwa Mama wa Mungu (Rej. Lk 1:26 – 38) linaonesha jinsi ambavyo aliitikia kwa “ndiyo” iliyo imara na isiyo na masharti wala woga kushiriki katika mpango wa Mungu. Bikira Maria aliweza kuitikia namna hii kwa sababu ya muunganiko wake na Mungu. Malaika Gabrieli alimtaja kama aliyejaa neema na uwepo wa Mungu ulikuwa pamoja naye.

Ili kuweza kuuitikia wito wa Mungu na kujiachilia mzima mzima katika mpango wako hali ya uwepo wa Mungu ni muhimu. Hali hii haijitokezi kwa nasibu tu bali inadai kuwekewa mazingira. Methali ya katika lugha ya kiswahili inasema: “mtoto umleavyo ndiyo akuavyo”. Hauwezi kuvuna zabibu katika mchongoma. Namna tunavyotengeneza mazingira yetu kuwa karibu na Mungu ndipo tunapata fursa ya kujazwa neema zake na hivyo kuitikia vema wito wake katika ufuasi wetu. Mama yetu Bikira Maria malkia wa watakatifu wote alikuwa daima katika ukaribu na Mungu kama wanavyokuwa Watakatifu wengine na ndiyo maana akasema kwa ujasiri na bila kuogopa: “na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38).

Katika hali yake ya ubikira, Bikira Maria anaendelea kuonesha utii wake kwa Neno la Mungu. Andhihirisha kuwa amejitoa mzima katika kumsikiliza Mungu tu. Sauti nyingine za pembeni, yaani mazoea na uovu wa kidunia hamkuyumbisha ama kumfanya apindishe usikivu wake kwa Mungu. Hii ilimfanya awe tayari kumsikiliza Mungu, kuliamini neno lake na kwa utii wake huo ameuzalia ulimwengu mkombozi. Hivyo Ubikira wake, unaofunua kujitoa kwake kikamilifu umemfanya kuwa Mama wa Mungu na Mama wa Kanisa. (Rejea Lumen Gentium, n. 56)

Hivyo, umama wa Bikira Maria unaunganika kwa nafasi ya kwanza na ufuasi wake kama binti mpendwa wa Mungu. Yeye amefanyika kwanza kuwa mwana mrithi wa Mungu, ameisikia sauti ya Mungu na kuruhusu utendaji wake ndani yake, hali ambazo ni muhimu katika kutufanya kuwa wana wa Mungu. Hapa anakuwa kwetu alama ya uwepo wa utendaji wa Mungu ndani mwetu. Hapa anatuthibitishia kuwa hali hii ya kufanyika wana wa Mungu si jambo la nadharia. Mwanadamu amewekewa ndani mwake uwezo wa kuipokea hali hiyo. Inatosha tu kuitambua hadhi hiyo na kuifanyia kazi.

Utendaji wetu kama wana warithi wa Mungu ni ufunuo wa utendaji wa Mwana mpendwa na Mungu. Uwepo wetu na utendaji wetu unapata mizizi katika yeye. Hapa tunakumbushwa kuwa mwana wa Mungu anapaswa kupata maana ya uwepo wake na utendaji wake wote katika Kristo. Yeye ndiye anayetufunulia uwepo wa Mungu na katika Roho Mtakatifu tunawezeshwa kutenda kweli kama watoto wa Mungu.

Kilele cha safari hii ni kuungana na Mungu mbinguni. Mama yetu Bikira Maria ameitikia kwa utii mkuu na kutenda kwa uaminifu ufuasi wake ndiyo maana leo Kanisa linashangilia kusimikwa kwake mbinguni kama Malkia wa mbingu na nchi. Hii ni chachu kwetu sisi tulio wafuasi wa Kristo. Kama tulivyoanza hapo juu tunaona Sakramenti ya ubatizo inatuingiza katika hadhi hiyo ya kuungana na Mungu. Tunapaswa kutambua kuwa hadhi hiyo haiishii tu katika ubatizo, inapaswa kudhihirishwa, kukua na mwisho tukaungane na Mama yetu Bikira Maria na Watakatifu wote mbinguni.

Sherehe ya kupalizwa mbinguni Mama yetu Bikira Maria inatusukuma kuendelea kuukimbilia ulinzi wake Mama Bikira Maria, kuomba msaada wa maombezi yake kupata neema za Mungu kusudi pamoja naye tuweze kusafiri na kupita salama katika bonde la machozi na hatimaye kuufikia uhuru wa kweli wa wana wa Mungu. Uhuru huo unapatikana pale Mungu anapokuwa yete katika yote. Yeye aliye muumba wetu anajua namna yetu na hivyo anavyokuwa ameenea kikamilifu katika uwepo wetu anatufanya kweli kuwa huru.

Bikira Maria uliyepalizwa mbinguni mwili na roho – UTUOMBEE!

 

14 August 2018, 17:07