Ekaristi Takatifu inatufanya kuwa hai katika Kristo!
Padre Joseph Peter Mosha - Vatican
Katika mkusanyiko wa karamu yoyote jambo kubwa linalotawala ni furaha. Mmoja anapopata mwaliko wa karamu hufanya maandalizi ya kimwili, kiakili na hata kihisia. Si rahisi mmoja kuchukulia mwaliko kama jambo la kawaida. Vazi lililo nadhifu na wakati mwingine linaloendana na wakati litaandaliwa, mpangilio wa siku hutawekwa vizuri na mengineyo mengi hufanyika ili mradi kuufanya mkusanyiko wa karamu uwe ni wenye tija. Tukiingia ndani zaidi na kutafakari tunaona karamu licha ya kuwa na lengo maalum lakini pia hutujenga katika mambo mengine ambayo hata hayo huiongeza furaha ya karamu. Huwa ni mahali pa kukutania, kufahamiana, kutengeneza mahusiano na kupata majukumu mapya binafsi au kwa ajili ya jamii nzima. Kwa ufupi, tendo la karamu hupata mwitikio chanya kwani humwongezea mwanadamu furaha, faraja na matumaini.
Masomo ya dominika ya 20 ya Mwaka B yanatupatia taswira ya karamu. Karamu hiyo inayoelezewa kwa namna fulani katika Somo la kwanza na katika Injili inalenga katika kumjenga na kumpatia mmoja kilicho cha kudumu. Inamuunganisha mmoja na Yeye aliye wa milele. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Mithali kinatuelezea jinsi karamu inavyoandaliwa ili kumpatia mwanadamu hekima. Anayeandaa karamu anatambulishwa kama Hekima. Hekima anaiandalia karamu yake mazingira: “ameijenga nyumba yake, amezichonga nguzo zake saba; amechinja nyama zake, amechanganya divai yake”. Maandalizi haya yaanaonekana katika taswira ya Kanisa, mwili wa Kristo ambao unaandaliwa na Mungu aliye Hekima yetu.
Maandalizi ya Hekima yanafuatiwa na mwaliko. Jambo linalotafakarisha ni aina ya wanaoalikwa: “aliye mjinga na aingie humu”. Tena amwambia “mtu aliyepungukiwa na akili, njoo ule mkate wangu, ukanywe divai niliyoichanganya”. Kifungu hiki kinatulazimisha kutafakari na kwenda mbali zaidi kuielewa lugha inayotumika hapa. Ni nani huyu aliye mjinga au aliyepungukiwa na akili? Mjinga katika tafsiri ya kawaida ni yule ambaye hana ujuzi au ufahamu wa jambo fulani na pia anatambua upungufu huo. Utambuzi huo wa kupungukiwa utamsukuma kutafuta maarifa na kuelewa. Hivyo mwaliko huu wa Hekima unatufafanulia maana ya karamu hiyo ambayo ni mwalimo wa Mungu kwetu, sisi tulio na upungufu wa ujuzi na kumwendea Yeye ili kujazwa na ujuzi wake. Ni mwaliko wa kwenda kwenye karamu, yaani kujitegemeza kwa Mungu.
Katika Injili Kristo anaichukua nafasi hiyo ya Hekima na anatualika akisema: “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu name ndani yake”. Yeye anakuwa ndiye mwandalizi wa karamu hiyo, anayetualika na pia chakula cha karamu hiyo. Karamu yake inatupatia uzima wa milele kwani inatuunganisha na Mungu. Yeye anakaa ndani yetu na sisi tunakaa ndani yake. Ekaristi Takatifu inatupatia uhai wa kimungu. “Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi”. Katika Ekaristi Takatifu tunaonja kwa karibu zaidi kuunganika na hekima ya Mungu kwani Kristo aliye Hekima anakuwa kwetu chakula na tunaunganika naye na hivyo sisi kufanyika yeye.
Kukaa ndani ya Kristo kunatupatia wajibu wa kuishiriki kazi yake ya ukombozi aliyoitimiza kwa fumbo la Pasaka. Kama wasemavyo mababa wa Kanisa kwamba anayeishiriki Ekaristi Takatifu anafanyika hicho anachokipokea, sisi nasi tunaona matokeo chanya ya kufanyika Ekaristi kwa Kristo kuwa chanzo, kichocheo na kikomo cha maisha yetu ya kiroho na kimaadili. Ekaristi Takatifu ambayo ni hekima ya Mungu inatuunganisha tena na Mungu. Kristo katika fumbo la Pasaka alisakafia muunganiko huo. Fumbo hilo ambalo ni muhtasari wa kazi yake yote ya ukombozi imeamsha tena dhamiri zetu na kuugundua upungufu wetu wa ujuzi na hekima ya kimungu. Hivyo mwaliko tuliousikia katika Somo la kwanza unatujia tena katika namna njema zaidi, yaani katika ujinga wetu tuijongee karamu ya Mungu ili kujazwa na Hekima yake na mwisho tuunganike naye na kuwa na uzima wa milele.
Kila mbatizwa amealikwa katika karamu hii na amejazwa hekima ya Mungu. Katika ulimwengu wa leo unaorindima kwa hekima za kibinadamu ushuhuda wa kiimani unahitajika sana. Mwaliko wa Mtakatifu Paulo katika Somo la pili ni ukumbusho wa haiba yetu: “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; kama ni watu wasio na hekima bali kama watu walio na hekima”. Na hivyo anatukumbusha wajibu wetu wa ushuhuda kwa “kuumboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu”. Ni maneno yanayotutaka sisi Wakristo tusiwe kama bendera inayofuata upepo tu. Mkristo anayetambua hadhi yake ni yeye anayetimiza mapenzi ya Mungu ambayo ni yale yaliyomo katika hekima ya Mungu aliyojaziwa.
“Awezaje mtu huyu kutupatia mwili wake ili sisi tuule?” Wayahudi walishindana wao kwa wao. Pengine wapo waliolipokea na wengine waliopinga kabisa ndiyo maana inaonekana mabishano kati yao. Fundisho la Kristo linaonekana ni jambo la ajabu na lisilopokeleka. Inawezekana vipi mtu kutuelekeza kula mwili wake na damu yake. Pamoja na mashaka hayo Kristo anaendelea kusisitiza kuula mwili wake na kuinywa damu yake kwa ajili ya uzima wa milele. Hapa inaonekana maana pana zaidi ya agizo lake; si kulipokea katika namna ya kimwili bali namna ya kiroho. Kuelewa mabadiliko ya kiroho ambayo yanaletwa na mwili wake. Kristo yu mzima kweli katika maumbo ya mkate na divai. Uwepo wake unapata mashiko katika nafsi ya mmoja anayekuwa na imani naye. Imani hiyo ndiyo inamfanya anayempokea Kristo kufanyika Kristo mwingine. Ekaristi takatifu inafanya sehemu muhimu ya uwepo wake na injini ya kusababisha utendaji wake.
Wapinzani wa Kristo katika Injili wanawakilisha jamii pinzani ya leo hii. Ni kundi la wanadamu wanaojikinai katika uwezo wao wa kiakili na vipaji vyao; wale ambao wanatumia nguvu zao za kishawishi iwe kiuchumi, kiutawala hata kidini kwa ajili ya kujistawisha wenyewe na si hekima ya Mungu. Mrengo huo wa kufikiria ndiyo unaozaa maswaibu mengi katika jamii ya mwanadamu. Hii ni kwa sababu kila mmoja anajijengea kaufalme kidogo ambacho mwingine haruhusiwi kugusa. Ubinafsi, chuki, dhuluma, magomvi na mengine yanayoendana nayo huipamba jamii hii. Mazingira haya kinzani ndiyo yanatualika sisi kuishuhudia Injili ya Kristo na kusema bila kuogopa kwamba tusipoungana na hekima yake hatuwezi kupata fanaka ya kudumu maishani mwetu.
Ekaristi Takatifu inatufanya kuwa hai katika Kristo. Hili ni fumbo la imani. Tunapaswa kuimarika kiimani ili kuyapata matunda yake. Ushiriki wa Ekaristi Takatifu unapaswa kuonesha matunda katika maisha ya Wakristo. Hivyo tuionapo jamii ya mwanadamu inakabiliana na majanga mbalimbali ili hali wapo wenye kumshiriki Kristo katika Ekaristi Takatifu kunakuwa na changamoto. Tunapaswa kuishi Ekaristi ambayo inatuunganisha na Kristo kwa kupata uzima mpya na wa milele. Hii ndiyo namna ya kuufanya uwepo wa Mungu uendelee kuwepo kati yetu.