Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili XVIII ya Mwaka B wa Kanisa
Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha. – Vatican.
Mpendwa msikilizaji wa Vatican News! Tuanze tafakari yetu kwa kujiuliza: Kwa nini tunamtafuta Mungu? Kwa nini tunasali? Je, imani yetu imejengwa katika nini? Uzoefu unatuonesha mara nyingi mwanadamu anapokuwa na hitaji ndipo humkimbilia Mungu. Mmoja ataomba kupata mtoto, mwingine kupata kazi, mwingine kupata uponyaji nk. Ukarimu wa Mungu hutujia na hapo tunafarijika. Lakini baada ya hali hii wengi humgeuzia kisogo Mungu au wakati mwingine hali ya kiimani hupungua. Muunganiko wetu na Mungu tunaupatia zaidi vionjo vya kidunia. Tunamkimbilia ili kutupatia chakula na mahitaji ya kimwili tu. Dominika ya leo inatualika katika safari ya kiroho, safari ambayo itatufanya tuunganike na Mungu katika ukamilifu wote kwani tunapoimarika kiroho hata changamoto za kila siku tutazikabili katika ukweli tukiwa na tumaini la kuwezeshwa na mwenyezi Mungu.
Safari ya Waisraeli kutoka utumwani Misri ambayo tunaelezewa katika somo la kwanza ilinuia kuwaandaa kiroho Waisraeli ili kuunganika kweli na Mungu. Katika safari hiyo tunaoneshwa taabu ya mwanadamu anayeshindwa kuitambua nia ya Mungu. Wao walibaki katika namna za kimwili na hivyo kwao ni bora kubaki katika utumwa ili mradi mkono unakwenda kinywani: “Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulivyokula vyakula hata kushiba…” Wanasahau mara moja kilio chao na ugumu wa utumwani kwa sababu tu wameona njaa; wanasahau mara moja jinsi walivyopoteza hadhi yao.
Kumpitisha mwanadamu njia ngumu ili kuufikia uhuru wa kweli ni kazi ngumu. Namna hii ambayo hudai kujitoa, juhudi na sadaka huonekana kama kikwazo. Ndiyo maana wengi hata katika jamii yetu letu hukimbilia njia nyepesi kujipatia masuluhisho ya kimaisha. Wapo wengine wanaodiriki hata kuwatoa kafara watoto, ndugu au watu wa karibu ili kupata utajiri na madaraka. Watu hawa hawajitambui kuwa wamefanywa watumwa na mambo ya kidunia ambayo mara nyingi huwanyima furaha ya kweli na inayodumu. Wanahangaika kila leo kuhuisha mambo hayo ya giza kwa sababu si ya kudumu. Ni vigumu sana kwa watu waliofikia hali hii kuwarudisha na kuwapitisha jangwani mithili ya waisraeli; kwao ni bora kuendelea na utumwa wao wa kidunia.
Katika Injili ya Dominika hii Kristo anaeleza umuhimu wa kubadili mwelekeo huo. Anaanza kwa kuonya akisema: “Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika”. Onyo lake hili linatokana na namna watu aliowalisha walivyohangaika kumtafuta. Yeye alitambua kuwa wanamtafuta si kwa sababu wamepata njaa ya kiroho bali ni kwa sababu walikula na kushiba kimwili. Hawamtafuti kwa sababu wamekula na kushiba kiroho bali kwa sababu “walikula ile mikate wakashiba”. Ni shibe ya kimwili ndiyo inawasukuma kumtafuta Kristo. Wanavyomkumbushia jinsi baba zao walivyopewa chakula kutoka mbinguni kupitia Musa wanaonesha namna yao ya kumwona Kristo kama “Musa” mwingine aliyekuja kuwapatia chakula. Bado hawajapata msukumo wa kiroho.
Mwaliko wa Kristo ni kufanyia safari ya kiroho ili kupata chakula cha kiroho, chakula ambacho kitawapatia nguvu ya kiroho. Pengine tunaweza kujiuliza sababu za msisitizo kutoka kinywani mwa Yesu kwa kushugulika na chakula cha kiroho. Chakula hiki ni nini? Na ipi ni tija yake kwa mwanadam mzima? Kristo aliye kuhani wetu, yaani kiunganishi chetu na mwenyezi Mungu ndiye pekee anayetupatia chakula cha kiroho. Yeye ndiye chakula hicho kishukacho kutoka mbinguni. Msisitizo wake unatupeleka katika ukamilifu wa kazi ya Mungu ambayo inapaswa kumgeuza mwanadamu mzima, mwili na roho. Ukarimu wa Mungu unapaswa kutujenga kiroho. Hii inamaanisha kwamba, wema na ukarimu wake anaotukirimia kila siku ni nafasi kwetu na kutambua hakika ya uwepo wake na hivyo kuzikabili changamoto zote za kiroho na kimwili tukiwa na tumaini katika yeye. Tumaini hilo ndilo chachu ya uimara wa imani yetu na kichocheo cha maisha yetu ya kimaadili yanayopata maana katika ufunuo wake kwa njia ya mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.
Injili ya leo inaendelea kumdadavua Kristo kama hicho chakula cha kiroho ambacho tunapaswa kukihangaikia. Je, ni kwa nini chakula hicho kinapewa uzito? Sababu ya kwanza ni kwa sababu ya asili yake na muunganiko wake na Mungu. Chakula hicho kinapata nafasi ya kwanza kwa sababu kinaupatia ulimwengu uzima. Uzima huu unapaswa kutofautishwa na namna iliyozoeleka ya uzima. Ni uzima wa kimungu unaodumu milele: “Yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe”. Hivyo ni mwaliko wa kuuona wema wa Mungu na muunganiko wake na sisi, namna ambayo inaufanya uwepo wetu hapa duniani uwe ni wa matumaini.
Chakula hicho cha kiroho kinatuelekeza katika matendo mawili muhimu. “Yeye ajaye kwangu”… hii umaanisha yeye anayeacha namna yake, tamaduni zake na mazoea na kumfuata Kristo. Pili, “Yeye aniaminiye”… ikimanisha paji la imani katika ufunuo wa Kristo. Hizi ni hatua mbili muhimu. Kristo anatutaka tutoke katika utu wetu wa zamani, yaani kusadaka na kufanya “metanoia” ya kweli. Maisha yetu katika imani ya kikristo ni mwanzo mpya. Namna na matamanio ya kidunia hayajatupatia suluhisho la kudumu. Kila mara tunajikuta tunahangaika kutafuta faraja nafsini mwetu. Tugeuke na twende kwa Yesu. Tendo hili la kumwendea Yeye ni tendo la kiimani na lenye mguso wa kiroho. Hivyo linahitaji paji la imani. Vinginevyo tutaingia katika hatari ya kumpokea Kristo kama mganga wa kienyeji ambaye tunamkimbilia tunapokuwa na shida tu na mambo yetu yanapokuwa sawia tunamsahau.
Safari ya kiroho inadhihirika katika utu upya tunaouvaa kwa njia ya ubatizo. Mtume Paulo anatuasa sisi Wakristo kudhihirisha huo utu mpya. Mkristo hapaswi kuhangaika na kuridhika na mapaji mbalimbali au mema wapokeayo kutoka kwa Mungu mithili ya utamu wa manna waliyokula pale jangwani wana wa Israeli. Tukibaki katika namna hiyo ni sumu kwa maendeleo yetu kiroho na kizuio cha kuwa vyombo vya kuufunua upendo wa Mungu kwa wengine. Tunapouona mkono wa Mungu tunapaswa kusafiri katika namna ya kiroho na kuelewa maana yake; mkono wake unaotenda kazi kwetu unatupatia neema, utulivu na kutosheka. Unatuonesha upendo na kujali. Hayo ndiyo yanapaswa tuyatafute kwa bidii na kuyaeneza. Karamu ya kimwili itushibishe kwanza roho zetu na kutufanya tuwake ndani mwetu uwepo wa Mungu.
Kubaki kufurahia mafanikio ya kimwili na yaonekanayo tu ni kushindwa kujivua utu wa kale. Namna hiyo inamfanya mmoja kuhangaika kumtafuta Mungu si kwa ajili ya kukua kiroho bali kwa ajili ya faida za kimwili. Changamoto nyingi za kimaisha zinaonekana kutopata mwarobaini wa kutosha kwa sababu ya mmoja kutuama katika masuluhisho yanayomjenga kimwili tu. Wema na ukarimu wa Mungu kupitia mapaji mbalimbali haumjengi mtu kufika hali kukua katika wema, upendo, huruma, ushirikiano, ukarimu na fadhila nyingine nyingi. Tunu za kimungu tuzipatazo kwa njia ya imani ni nyenzo ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha. Hivyo, tufanye juhudi ya kutafuta kile kinachotukuza kiroho. Hicho ndicho kinachodumu milele na hakika ya ustawi wetu kimwili na kiroho.