Tafuta

Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, chakula cha uzima wa milele. Kristo Yesu ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni, chakula cha uzima wa milele. 

Shikamaneni na Yesu chakula cha uzima wa milele mpate utakatifu

Yesu anawakumbusha kuwa ni yeye wanayepaswa kumtafuta na wala si kitu kingine. Wanaweza kutumia vitu vingine kumtafuta Yeye lakini kamwe wasimtumie Yeye kwa ajili ya kutafuta vitu vingine. Mtume Paulo anawaalika watu kuhangaikia utakatifu wa maisha na kwamba, kuutafuta utakatifu wa maisha ndio kinapaswa kuwa kitu tunachokitafuta katika yote tuyafanyayo maishani.

Na Padre William Bahitwa. – Vatican.

UTANGULIZI: Yesu Kristo ndiye mjumbe halisi wa Mungu Baba. Ndiye anayebeba ufunuo kamili wa Mungu na ndiye anayefungua njia iendayo kwa Mungu. Yeyote anayemwamini na kumfuata, yeyote anayemsikiliza na anayemweka mbele maishani atapata uzima ule udumuo milele. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu leo ikiwa ni dominika ya 18 ya mwaka B wa Kanisa. Dominika ambayo Neno la Mungu linatualika tutambue maishani kile kinachodumu na kinachofaa zaidi kati ya mahitaji mengi na kati ya mengi yanayotuzunguka maishani.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Kut. 16: 2-4, 12-15) waisraeli wakiwa jangwani katika safari yao kutoka utumwani Misri kuelekea nchi ya ahadi wanaanza kuwalalamikia Musa na Haruni kwa kukosa chakula. Wanalalamika na hata kukata tamaa kwani wanafikia mahali wanatamani kufa, wanasema “afadhali tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri”. Wanaenda mbali hata kuona ukombozi aliowafanyia Mungu kutoka utumwani si kitu kulinganisha na chakula walichokuwa wakila huko. Mungu anasikia kilio chao na anawashushia chakula kutoka mbinguni: nyama wakati wa jioni na mkate wakati wa asubuhi.

Somo la pili (Ef. 4:17,20-24) ni mahusia ya mtume Paulo kwa waefeso kuhusu utakatifu wa maisha. Kwa kuangalia mazingira waliyokuwa wanaishi na mwingiliano wa watu mbalimbali, watu wa mataifa” kwa sababu za kibiashara, Mtume Paulo anawaasa wakristo wa Efeso kutambua kuwa ni utakatifu wa maisha utakaowatofautisha na watu wengine, watu wasiomwamini Kristo. Kufikia utakatifu wa maisha anawaalika wawe tayari kuuvua utu wa kale unaoharibika. Huu ndio mwenendo usiofaa, mwenendo wa kuzifuata tamaa zenye kudanganya na wauvae utu mpya na wafanywe upya katika roho na nia.

Mwenendo usiofaa unaitwa “utu” wa kale kwa sababu nao upo kama mtu. Una viungo vyake mbalimbali na una uwezo wa kujiimarisha na uwezo wa kukua. Lakini ni utu unaoharibika kwa sababu kwa ndani yake una asili ya uovu; na uovu au dhambi kwa asili huharibu. Pale unapopewa nafasi uovu au dhambi huanza kwa kudanganya kuleta furaha, uhuru na kadhalika lakini kimsingi huishia kuharibu kabisa kabisa. Na hii ndiyo maana unahitaji kuvuliwa na kuondolewa kabisa. Utu mpya ndiyo asili mpya inayomwezesha mwanadamu kuishi maisha mapya yasiyo na uharibifu. Utu mpya ndio neema inayomsaidia kuufikia utakatifu.

Injili (Yn. 6: 24-35) Kristo anawaonya wanaomfuata kwa sababu walishibishwa kwa muujiza ya mikate. Anawaonya akiwaambia “msikitendee kazi chakula chenye kuharibika bali chakula kidumucho hata uzima wa milele”. Kama awali Mungu alivyowapa waisraeli jangwani chakula kutoka mbinguni kwa ajili ya kushibisha miili yao ndivyo kwa njia ya Yesu Kristo Mungu anawapa sasa chakula halisi kwa ajili ya kushibisha roho zao. Kisha anaongeza kuwaambia Yeye ndiye chakula hicho halisi, chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni, chakula ambacho yeyote akilaye hataona njaa naye aaminiye hataona kiu kamwe.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, ninawaalika tuianze tafakari yetu ya leo kwa kujiuliza; ni nini kinachonishughulisha maishani? Ni nini ninachokitafuta? Na haya ni ya kujiuliza katika hali mbalimbali za maisha: katika utumishi, katika kuajiriwa au kujiajiri, katika, kazi au ustaafu, katika biashara au ubangaizaji, katika masomo au katika uangalizi wa familia nyumbani ni nini ninachokitafuta? Kwa kawaida tunaweza kusema tunatafuta maisha mazuri au mafanikio maishani, lakini je ni uzuri gani wa maisha tunautafuta au ni mafanikio yapi tunayatafuta? Ni nini kipimo chake? Tunapaswa mara kwa mara kuweka kituo katika maisha na kujihoji maswali haya na mengine kama haya ili katika yote tufanyayo tutafute kilicho bora, kilicho cha maana na kidumucho. Vinginevyo tutakuwa kama wakimbizao upepo.

Yesu anapowaona umati mkubwa wa watu wanaomfuata na moja kwa moja anajua kuwa hawamfuati kwa kitu kingine isipokuwa kwa sababu ya ile mikate aliyowalisha. Anasikitika kwa sababu anaona wamebaki katika alama bila kushughulikia zaidi kile ambacho alama inamaanisha. Na tena wamebaki katika yale yapitayo, yale ya muda mfupi tu na kuacha yale yadumuyo. Kwamba wamebaki kutafuta kushibishwa kwa mara nyingine tena kwa muujiza bila kwenda mbele kupata kile ambacho muujiza huo ulikusudia. Anawakumbusha kuwa ni yeye wanayepaswa kumtafuta na wala si kitu kingine. Wanaweza kutumia vitu vingine kumtafuta Yeye lakini kamwe wasimtumie Yeye kwa ajili ya kutafuta vitu vingine.

Ni katika mwanga huu tunamwona Mtume Paulo katika somo la pili anawaalika watu kuhangaikia utakatifu wa maisha. Anasisitiza kwa waamini wa Efeso na kwetu leo hii kuwa kuutafuta utakatifu wa maisha ndio kinapaswa kuwa kitu tunachokitafuta katika yote tuyafanyayo maishani. Katika utume, katika kazi, katika ustaafu, katika biashara, katika ubangaizaji, katika masomo katika uangalizi wa familia tuyatekeleze yote bila kusahau kuuweka mbele utakatifu wa maisha.

Hii ni kwa sababu wito wetu wa kwanza, kama unavyotukumbusha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika hati yake ya Mwanga wa Mataifa, ni wito wa kuwa watakatifu; “kwa hiyo wote katika Kanisa, wawe watu wa hierakia au wawe waongozwao nayo, wanaitwa kuwa watakatifu, kadiri anavyosema Mtume Paulo ‘Haya ndiyo mapenzi ya Mungu katika kutakaswa kwenu’” (LG. 39). Hii pia ndiyo dhamira ya waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Gaudete et exultate” kuhusu wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo. Tumwombe Mwenyezi Mungu leo neema hii ya pekee, kuyatambua yadumuyo na ya msingi katika maisha na hayo ndiyo tuyape kipaumbele, yaani kumtambua Kristo Bwana wetu anayetujaza ya mema ya Kiroho kwa ajili ya uzima ule udumuo milele.

Sikiliza kwa raha zako mwenyewe!

 

04 August 2018, 07:54