Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha yetu ya kiroho. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha yetu ya kiroho. 

Kristo Yesu ni chakula cha uzima kwa roho zetu!

Tukitaka kuelewa vizuri somo la Injili ya Jumapili 19 ya Mwaka B wa Kanisa ni lazima kuelewa vizuri fundisho la Mt. Paulo katika somo la pili. Fundisho hili la Paulo latusaidia kuelewa maana ya Msalaba, alama ya upendo na wokovu kwa anayeamini. Anakazia ile maana ya kujitoa kwa ajili ya wengine kama Yesu anavyofafanua katika Injili.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Ndugu wapendwa, dominika iliyopita tuliona Yesu akitoa mkate wa uzima, mkate wa Mungu, utokao mbinguni ambao ni uzima wa ulimwengu. Wote wakajibu, Bwana tupe daima mkate huo.  Na jibu la Yesu linakuwa ni mwaliko wenye changamoto – mimi ndimi mkate wa uzima. Yeye ajaye kwangu hataona njaa kamwe, aniaminiye hataona kiu kamwe. Katika somo la Injili ya leo hali ya hewa kati ya wale watu inabadilika kabisa. Yaonekana kuwa fundisho hili linawapa changamoto kubwa. Wanalalamika kati yao – yawezekanaje? Hao ni wale waliompinga Kristo. Basi tuingie kwenye tafakari yetu ya leo tukianza kuangalia masomo yetu ya leo katika ujumla wake.

Katika somo la kwanza: Nabii Eliya anajikuta katika mazingira magumu: watu wakaidi, miungu ya uongo, Yezebeli – mtawala wa Israeli, malkia dhalimu anataka kumuua. Nabii anatorokea jangwani, katika mlima Sinai, mahali taifa jipya la Israeli lilipozaliwa. Anahangaika sana na kukata tamaa. Mungu anamlinda na malaika wanakuwa walinzi wake. Chakula chake kinakuwa maji na mkate. Na hii inakuwa alama ya Mungu kumlinda.

Katika somo la pili – Mtakatifu Paulo anaona alama za upinzani toka kwa Waisraeli. Lakini yeye anataja fadhila mbalimbali kama namna mpya ya mahusiano. Huu mtazamo mpya wa maisha, wazungumzia maisha mapya na Paulo anauita – kumuiga Mungu. Na kwa fundisho hili anaeleza vizuri maana ya fundisho la Injili ya leo. Tukitaka kuelewa vizuri somo la Injili la leo ni lazima kuelewa vizuri fundisho la Mtakatifu Paulo katika somo hili la pili. Fundisho hili la Paulo latusaidia kuelewa maana ya msalaba, alama ya upendo na wokovu kwa anayeamini Efe. 5: 2 – ile maana ya kujitoa kwa ajili ya wengine – kama ilivyo katika Injili.

Katika Injili – yaonekana tatizo kubwa la imani – wao wanasema haiwezekani – katika mtazamo wao na uelewa wao – mstari 42 – kwa sababu wanamfahamu, wanaukataa umungu wa Kristo – Mk. 6:3. Wao wanamfahamu. Hapa unatokea mgongano kati ya uelewa wa mwanadamu na ufunuo wa Mungu. Wanaungana mkono kati yao kuukataa ukweli. Tunajua kuwa ukweli husimama wenyewe ila uongo hupigiza kelele na kutafuta waungaji mkono batili. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema – ukweli ni nguvu inayosimama yenyewe katika maisha. Hakuna hitaji la jeshi kuulinda. Yesu anabaki katika msimamo wake na anasema wazi hakuna awezaye kuja kwangu asipovutwa na Baba aliyenipeleka na mstari 44-47 – yazungumzia fumbo la utendaji la Mungu katika moyo wa mwanadamu. Kwa kuongezea uelewa wetu, maelezo yapatikanayo katika somo la pili yangetosha kuondoa hofu hiyo. Ni lazima kusikiliza anachosema Mungu. Sauti ya Mungu inasema nini? Mpango wa Mungu wa ukombozi unasema nini? Katika mstari 37-39 – Yesu anaweka wazi – ni kufanya atakayo aliyenituma.

Tutambue kuwa imani ni zawadi ya Mungu. Imani yataka mshikamano na hii huondoa vikwazo. Jumapili iliyopita tumeona kuwa Yesu ni kazi ya Mungu, anafanya mapenzi ya Mungu, aliyepelekwa naye kuyafanya mapenzi ya Baba kwa kusema neno lake. Wote wamwaminio Baba kama Mungu wao, wanampokea pia huyo Mwana na ukweli alioutangaza. Kwa namna ya pekee tunaona katika jumapili ya leo Yesu anaendelea kusisitiza upekee wake na Baba yake. Wote watafundishwa na Baba na kusikia hilo fundisho

Tunaposoma mstari 48-51 twaona kuwa imani pamoja na mapendo huzaa maisha mapya. Huu uzima mpya hutoka mbinguni na hilo neno la MUNGU ni mkate toka mbinguni.  Mtakatifu Paulo katika Gal. 2:20 anatusaidia kuelewa fumbo hili  – si mimi tena ninayeishi, bali  ni Kristo anayeishi ndani yangu. Muda huu ninaoishi bado mwilini, ninaishi katika imani inayomtegemea Mwana wa Mungu, ambaye amenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

Tunamshukuru Mungu ambaye amempeleka mwanae wa pekee kwa ajili yetu ambaye ndiye uzima wenyewe.

Tumsifu Yesu Kristo.

 

11 August 2018, 09:29