Kenya:Jimbo la Embu kuwa na chombo kipya cha mawasiliano!
Frt. Titus KImario - Vatican
“Fikeni kwa wakati muafaka, hivi karibuni tutapata radio, hivyo mnaweza kutoa michango yenu kwenye programu za redio kwa sababu watu wanahitaji kujua nini kinachoendelea katika maisha msingi ya kijamii hata vijijini”.Hayo yamesema na Askofu Paul Kariuki Njiru, wa jimbo la Embu nchini Kenya, alipokuwa anazungumza na wajumbe wawakilishi thelathini wa mawasiliano kijamii parokiani, ambao wamefuzu mafunzo yao yaliyoandaliwa na Tume ya Maaskofu ya Mawasiliano ya jamii.
Askofu Kariuki amewataka wahitimu kushughulikia hali za wanyonge na kuripoti kazi nzuri nyingi ambazo Kanisa linafanya katika kazi za uinjilishaji. “Badilisheni maisha ya wengine” anasisitiza huku akiweka wazi hali ngumu za masikini katika jamii, ili kwamba watu waweze kuguswa na kujitolea kuwasaidia. “inyi muwe mawakala mtakaosaidia kukusanya habari ambazo ni tofauti na zile za vyombo vingine vya habari vya kiraia”.
Naye Katibu mtendaji wa mawasiliano wa Tume ya Maaskofu ya Mawasiliano ya kijamii, Padre Elias Mokua, amesema lengo la mafunzo ya wanahabari ni kusaidia Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya katika mawasiliano na wakatoliki, hata wasio wakatoliki na kujenga mtandao wa mawasiliano kitaifa ambao utakuza utambulisho wa Kikatoliki, Maadili, Amani na Haki.
Akiendelea na msisitizo Padre Mokua amesema, “Daima tunahitaji kutumia nguvu zetu kama Kanisa katoliki kuinjilisha, kufundisha tunu za Injili, kukuza haki za kijamii, kuyafikia majimbo yasiyokuwa na redio au gazeti, kuunda na kuweka Kanisa katoliki katika mtandao wa moja kwa moja katika mindao ya kijamii, kuwa na Kanisa linalotumia teknolojia za kisasa za vyombo vya habari katika uinjilishaji”.
Padre Mokua Kadhalika ameonesha haja ya kuendeleza utambulisho mkubwa wa Kikatoliki katikati ya ushindani unaokua kati ya vyombo vya habari mbalimbali na kuonesha mambo ya Kikatoliki, kuweza kuondoa habari na taarifa ambazo zinakwenda kinyume na habari au mazingira halisi ya dunia ya sasa. Hiyo ni inahitaji kujikta katika kutangaza habari za Kanisa na nyingine ambazo zitasaidia uinjilishaji na kuinua kizazi kipya na endelevu cha wafanyakazi wa vyombo vya habari Kikatoliki!