Kristo Yesu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. 

Kristo Yesu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu!

Dhiki mbali mbali katika maisha ya mwanadamu zimedhihirisha upendo na huruma ya Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ambaye aliamua kujitwika na hivyo kujiangalisha na maskini pamoja na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Kanisa bado ni mtetezi, chemchemi ya faraja na ukombozi wa maskini na wanyonge!

Na Padre Joseph Peter Mosha. – Vatican.

Mwanadamu katika hali ya mahangaiko na udhaifu hutafuta faraja. Hali hiyo inapopatikana, yaani kuwa na faraja au nafuu mwanzo mpya huonekana. Lakini tukijiuliza sababu za mahangaiko au udhaifu fulani tunaona haraka kuwa vyote husababishwa na upungufu fulani. Katika hali hiyo, na tukizingatia kuwa mwanadamu alipoumbwa aliumbwa katika hali ya ukamilifu, hali ya udhaifu au mahangaiko huashiria upungufu fulani katika ukamilifu wake. Mafundisho ya Kanisa yanatuonesha kuwa taabu hizi na masumbuko zilianza na na anguko la kwanza la mwanadamu. Anguko hilo limejumuishwa katika kitendo cha kumwasi mwenyezi Mungu. Hivyo tunaona kuwa taabu na mahangaiko yanamfika mwanadamu kwa sababu ya kuufukuza uwepo wa Mungu ndani yake na hivyo kuukosa msingi, chanzo na sababu ya uwepo wake na kazi yote ya uumbaji.

Historia nzima ya wokovu wa mwanadamu inajikita katika kuirekebisha hali hiyo. Somo la kwanza linaanza kwa kutuonesha jinsi Mungu anavyoanza kuwaunda upya watu wake. Hii ni baada ya uasi wao ambao uliwapeleka utumwani. Sehemu hii ya kitabu cha Nabii Yeremia huitwa «kitabu cha faraja». Nabii Yeremia aliishi wakati wa kipindi hiki kigumu ambapo alishuhudia kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu kulikotimizwa na jeshi la Babeli. Yerusalemu ilikuwa ni ishara ya uwepo wa Mungu kwa taifa la Israeli. Katika mji huu waliona ufahari wote wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Uharibifu wa mji huu, muhimu kama ulivyokuwa, umewaachia uchungu mkubwa sana. Lakini ujumbe wa faraja wanaoupata ni sababu ya kupata tena nguvu. “Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia”. Mwaliko wa Bwana Mungu kwao unawahakikishia wokovu na kuanza upya tena.

Bwana ananuia kuwakomboa hao wanaoitwa «mabaki ya Israeli». Pengine hali zao zinaweza kuonesha udhaifu, maana tunaambiwa “pamoja nao watakuja vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa”. Lakini Mungu anaanzisha familia mpya kupitia watu hawa. Mwenyezi Mungu anawaahidia ulinzi na uongozi wake hadi kufikia ukamilifu. “Nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu”. Mungu anapojitambulisha katika sura ya baba anaifunua haiba yake kama chanzo na tegemeo la uumbaji wote. Haiba hii ni muhimu katika kukazia umuhimu wa uwepo na utegemezi wa mwanadamu kwa Mungu.

Somo la pili linatuonesha Kristo aliye Kuhani Mkuu na kwa njia yake tunahuishwa upya. Huu ni wito kwa wanadamu wote kuiona nafasi nyeti ya Kristo katika kuufanya hai uwepo wa Mungu na hivyo kumfanya Yeye, yaani Mungu, kuwa sehemu muhimu ya uwepo wa kazi yote ya uumbaji. Kristo kama kuhani wetu wa Agano jipya anatambulishwa katika Yeye “aliyetwaliwa katika wanadamu”. Hii inaturudisha Dominika iliyopita ambapo tulimwona Yeye aliye Kuhani wetu Mkuu akishiriki katika ubinadamu wote kwa hali zote. Yeye alichukua taabu na mahangaiko yetu katika mwili wake. Katika ushiriki huo anajitoa nafsi yake kuwa sadaka ya upatanisho wetu na Mungu. Uwepo wake huu wa kikuhani unaoneshwa vizuri katika namna yake ya umungu na ubinadamu na hivyo kwa njia yake umungu na ubinadamu, uliotengana kwa sababu ya dhambi, unaunganishwa tena.

Ukuhani wa Kristo mfufuka unajionesha kama nyenzo ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika taabu na udhaifu wake. “Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake” (Heb 2:17). Kwa kuyachukua madhaifu yetu katika mwili wake na kuyagongomelea katika mti wa msalaba anafufuka mzima, katika mwili wa utukufu, mwili unaooesha ushindi wa uhai dhidi ya kifo na mauti. Katika Yeye tunaupata upya wa ubinadamu wetu na hivyo tunaunganishwa tena na Mungu. Kristo Kuhani Mkuu anakuwa kwetu sababu ya kuunganika tena na Mungu na hivyo kupata hakika ya faraja aliyoiahidi katika somo la kwanza kwamba “nitawaongoza, nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyooka; katika njia hiyo hawatajikwaa”.

Uwepo wa Kristo unaonesha kwa vitendo uwepo wa wema wa Mungu unaorudisha matumaini na mwanzo mpya kwa mwanadamu. Nafasi hiyo ya Kristo inajionesha katika uponyaji anaomfanyia Bartimayo mwana wa Timayo. Kwa njia ya uponyaji huu wa kimwili kwa kipofu Bartimayo tunapaswa kuzama ndani na kuuona uponyaji wa kimasiha wa Kristo ambao ni kwa ajili ya wokovu wetu. “Enenda zako, imani yako imekuponya”. Dokezo hili la imani kutoka kwa Kristo linasakafia umuhimu wa paji la imani katika kuupokea uponyaji huo wa kimasiha ndani ya roho zetu. Imani hiyo huchagizwa na uelewa wetu wa ndani wa haiba ya Kristo na nafasi yake katika maisha yetu wanadamu. Hii inamaanisha kwamba, tusipomwelewa Kristo na haiba yake ya ukombozi inayodadavuliwa katika somo lake la pili ni vigumu kuomba uponyaji wake. Baada ya uponyaji tunaambiwa: “akamfuata njiani”. Hapa tunaiona nafasi ya mmoja anayefunuliwa uelewa wake wa ndani, anamtambua Kristo na nafasi yake na hivyo anayatoa maisha yake ili kuambatana naye.

Mwanadamu anapoamua kuasi na kumwacha mwenyezi Mungu huangukia katika upofu na kushindwa kutembea barabara. Mara nyingine huwa anajitutumua kwa kujikinai kuyafanikisha yote kwa uwezo wake lakini katika uhalisia taraja yake humwingiza katika ama majibu ya kupita kwa kitambo kifupi tu au kutokupata kadiri ya matarajio yake. Namna hii humwingiza mwanadamu katika utumwa mbaya zaidi ya ule wa kisiasa walioupata wana wa Israeli. Zama za falsafa ya “uangaziwaji” au Illumination ilimkuza mwanadamu katika kiburi chake na kufikiri kuwa akili yake inayo uwezo wa kumfikisha katika elimu yote. Akiwa amejisahau katika ukomo wa asili yake mang’amuzi mengi ya binadamu ambayo yalimwondoa mwenyezi Mungu yamempelekea balaa. Matokeo yake ni vita na vurugu zisizokwisha, dhuluma ya utu wa mtu kati ya jamii moja na ulimwengu mzima n.k.

Leo Kristo anatuuliza kila mmoja kwa nafasi yake: “Wataka nikufanyie nini?” Ni vema jibu letu likawa kama la Bartimayo mwana wa Timayo: “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona”. Jibu hili linafanana na ile hekima ya Solomoni pale alipopata nafasi ya kuomba chochote kwa Mungu na jibu lake nikawa: “nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?” (1Fal 3:9). Hekima hii inayoombwa na Solomoni hufanana na hamu ya Bartimayo ya kutaka kuona. Mwanadamu amejaliwa karama na vipaji mbalimbali. Mwenyezi Mungu amewekeza katika kila mmoja mmoja wetu kwa makusudi ya kuujenga vema ulimwengu huu. Tunapoitoa na kuidharau hekima ya Mungu mara nyingi tunajiingiza katika matumizi mabaya ya nafasi zetu na matokeo yake ni unangamizi kwa mtu binafsi na jamii nzima.

Tuombe Roho wa Mungu atuongoze na kutupatia ujasiri wa kuomba kuona. Kristo Kuhani wetu Mkuu ndiye kiongozi wetu na njia yetu ya kuipata hekima hiyo. Tujishikamanishe naye katika Neno lake na katika Sakramenti hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu sana ili kwa njia yake tuendelee kuuonja uwepo wa Mungu na hivyo kuongozwa na Yeye.

J30 Mwaka
25 October 2018, 13:30