Kristo Yesu ni ufunuo wa hekima ya Mungu, Itafuteni kwa ari na moyo mkuu!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Kutoka maandiko matakatifu yapo maelezo yanayojitosheleza – 1 Fal. 3:4, Mfalme Solomoni aliomba hekima kwa Mungu badala ya mali. Anafahamika kama mtu wa kwanza mwenye hekima katika Israeli. Hekima ya Mungu – ni thawabu ya Roho wa Bwana kwa njia ya ufunuo. Hekima ya Mungu ni bora – Mit. 21:30, huhusiana na haki – Mit. 1:7, ni Mungu anayegawa hekima – Mit. 2,6, 1Kor. 2:6-16 - hekima aliyejionesha kama Nafsi na Mwumbaji.
Katika Agano Jipya tunaona kuwa Yesu Kristo ndiye hekima yenyewe – Mt. 11:19, Lk. 11,49 n.k. ndiye hekima ya Mungu, hekima anayeshiriki katika kazi ya kuumba na kuhifadhi ulimwengu – Kol. 1:16-17, katika kutunza Israeli n.k. Kwa kifupi: Hekima ni Kristo na Kristo ni Mungu. Kadiri ya maandiko, hekima ya Mungu haiwezi kufahamika na mtu. Mtu hawezi kufahamu hekima na kuipata kwa nguvu zake – Bar. 3:9 na 4:4. Mungu anamfunulia hekima Israeli peke yake.
Ayubu 28:28 anasema – mtu yampasa ajitoshelee na uchaji wa Mungu – ambao peke yake ndiyo hekima inayomfaa. Kadiri ya Rum. 16: 27, 11:33-36 na 1Kor. 1:24 – Mungu ndiye mwenye hekima peke yake. Hivi sasa mbele yetu ingewekwa fursa ya kuchagua katika mengi yaliyopo na tunayohitaji, tungechagua nini? Hii ingeweza kuwa tafakari tosha kwa siku yetu ya leo. Mtaalaamu mmoja katika kujaribu kuandaa tafakari ya siku ya leo anauliza – Je Ukristo unawezekana? Anaendelea kusema wa kwanza anaomba hekima, katika injili anaambiwa akauze vyote alivyo navyo. Katika hali ya kawaida ataishije?
Katika somo la 1 - hasa tukiangalia - 1Fal. 3:3-15 – tunaona kuwa katika ndoto. Mungu alimpa mfalme nafasi ya kuomba zawadi yo yote – anaomba ufahamu wa moyo – sawa na hekima. Katika Maandiko Matakatifu – hekima ni hali ya kimbingu – karama iliyo kuu zaidi ambayo mtu aweza kufurahia. Mwenye hekima – anatambulika kama aliye na vyote, asiye na mahitaji tena. Hii ilionekana wakati wa ufalme wa Solomoni katika taifa la Israeli – kwa macho ya watu uwepo wa Hekima ya Mungu. Kijana mmoja alijigamba – nina hekima, kwa vile nimeongea na watu wengi wenye hekima. Epictetus akamjibu – hata mimi nimeongea na watu wengi matajiri lakini mimi si tajiri.
Katika Somo la Injili tunaona kuwa ujio na uwepo wa Kristo ambae ndiye Hekima yenyewe ambao ni uonesho wa ufalme wa Mungu, utakaokamilika wakati ujao, ukidhihirisha uwepo wa ufalme wa Mungu kwa watu wake. Hivyo swali la kijana tajiri – nifanye nini niupate uzima wa milele? Kadiri ya Wainjili Mk. na Lk.- uzima wa milele maana yake ni UFALME WA MUNGU, ulio utajiri kamili. Na jibu la YESU – uelewa na mtazamo wetu juu ya ufalme uwe kama ule wa Solomoni na Hekima – utajiri unaozidi utajiri wa aina nyingine ile. Zaidi sana ni kufanya kwa matendo, kuuza ulivyo navyo. Swali letu au wasiwasi wa kibinadamu unarudia – yawezekana kuwa Mkristo?
Tuendelee kutafakari. Mahangaiko yetu na mengi ni kupata zaidi – hasa vitu vya ulimwengu na kuvikumbatia. Tunafunga nyumba/vyumba/tumeweka mageti mbalimbali/walinzi/ tumeweka pin namba kwenye simu na akaunti zetu n.k kwa sababu gani? Ni ulinzi tu wa kawaida? Woga wa kuibiwa? Kitu gani kwa mfano? Ulinzi wa watoto, wazee, wagonjwa. fedha, mali, simu, rosari, msalaba, kitabu cha masifu, biblia, meseji za simu? Mbona pengine kisichofaa au kuhitajika sana tunawekea ulinzi wa pekee ili hali kile kinachofaa au kuhitajika zaidi tunaacha kinazagaa ovyo? Palipo na hazina ndipo penye moyo. Hazina yako ni ipi na iko wapi? Yule mtoto anamwuliza baba yake, je waweza kumpa housegirl wetu namba ya siri ya benki? Baba anasema hapana. Na mtoto anamwambia mbona unaniacha na housegirl? Ni kipi bora zaidi, benki akaunti au mimi mtoto wako?
Kwa mafundisho ya Yesu na iko wazi, utajiri wa dunia ni kuzuizi, ila kwa Mungu hakuna lisilowezekana. Yule aliyeuliza swali – je Ukristo utawezekana? Anatoa jibu hili: Kama ni jinsi ilivyo katika benki – kuongeza hela ili kupata riba – ukristo hautawezekana. Ila kama ni kuishi kama inavyotakiwa na kadiri ya mafundisho inawezekana – vinginevyo Yesu atakuwa mwongo. Je, neno hili tulolisikia leo na imani yetu inawekwa njia panda? Yule wa kwanza anaambiwa aombe zawadi – anaomba hekima ambayo hata hajui pengine uzito wake. Huyu kijana wa Injili anasema – nifanye nini? Yesu anamjibu – shika amri, nenda kauze – tena vyote ulivyo navyo, ikawa shida, anaondoka zake, anamwacha Yesu. Yaonekana wazi kuwa – utajiri ( lakini utajiri ni nini) ni kitu hatari sana. Yesu anaonesha wazi wazi. Katika Fip. 2:6, Yesu mwenyewe anaonesha mfano wa kuacha yote ili kupata yote. Yesu kwa asili alikuwa Mungu, lakini hakung’ang’ania Umungu wake. Aliachilia hayo yote ili kutupata sisi.
Mifano mingine ni wasiwasi ya walioacha yote; Mt. Petro – sisi tuliyoacha vyote tutapata nini? Kumbe uwezekano wa kuacha vyote upo. Ushuhuda wa Petro – na jibu la Yesu. Atapata vyote na uzima wa milele. Je sisi tuliopo hapa leo, tunaweza kutoa ushuhuda wo wote kama Petro? Maisha ya Watakatifu wetu yanatupa changamoto gani kuhusu jambo hili? Hivi tajiri wa kweli ni yupi?
Je, utajiri wetu ni upi?: Kwamba tu watoto wa Mungu, Mali, Hali, Mila, desturi, tabasamu, makabila, ukabila, Sura nzuri, Upendo, Ukarimu, Tabia mbaya na chafu, Uvivu, Ukaidi, kiburi, tamaa mbaya, Uzembe, Usengenyaji, Uongo, Ukristo wetu, Imani n.k. katika haya machache uko wapi hapa, una kitu gani? Mfano wa yule mama aliyelemaa mguu mmoja baada ya ajali ya gari. Akitembea akitumia magongo. Siku moja akiwa jikoni anapika, akagundua moto toka ghorofani na ukitoka chumba alicholala mtoto wake. Ilimbidi kusahau ukiwete wake, akatupa yale magongo na kuwahi mbio kumwokoa mtoto wake. Ili kupata ni lazima kupoteza. Alimpenda mtoto wake na akasahau ukiwete wake. Akampata mwanae.
Katika hali ya kawaida, akiwapo mgeni, twajaribu kumpatia yaliyo mazuri na yaliyo mabaya kwa wakati huo tunayaficha. Huwa tunasema mgeni aje mwenyeji apone. Je uwepo wa Kristo unatuponja kweli na hali zetu? Zile hali zinazopingana na wito wake Kristo? Je tumezificha tu au tumeziacha kabisa? Kuna mfano mmoja wa yule aliyeshikilia tawi la mwisho kabla ya kukwanyuka mtini. Anamwomba Mungu amsaidie. Na sauti inasikika kama mwangwi, achia, achia. Lakini hajiamini, anashindwa kuachia. Anaomba Mungu amsaidie, anasikia sauti, lakini haiamini hiyo sauti. Wengi wetu kama si wote tunapofikia hali hii tunahangaika kweli kweli. Huku tumeshikilia mambo yetu, huku tunayataka ya Mungu.
Yesu yupo kati yetu leo na anaendelea kutualika, njoo unifuate, acha ulivyo navyo – nitakupa uzima wa milele. Kama yule kijana. Je, bado tuna nia ya kumwendea kwa dhati na kumwuliza siku hadi siku – nifanye nini niupate uzima wa milele? Au basi tunamfuata ili hali tukibaki jinsi tulivyomfahamu, tukitumia tu mbinu binafsi, maarifa au njia tunazodhania kuwa zinajitosheleza kuupata uzima wa milele? Tena pengine hizo mbinu, njia n.k – hata kibinadamu hazikubaliki? Na kwa kiasi gani na kwa kina gani tunatafakari maandiko matakatifu? Ni kwa kiasi gani tunabaki waaminifu katika kuishi maandiko hayo?
Yule kijana tajiri anakupatia changamoto ipi katika maisha yako kama mfuasi wa Kristo? Yule aliufahamu vizuri utajiri wake – ikawa vigumu kuuacha. Je wewe unaufahamu kwa kina utajiri ulio nao? Wakati wa utawala wa Napoleon, mateka mmoja huko Urusi alitumikishwa kama mtumwa na aliwekewa alama ya N katika mkono wake. Alipoelewa maana ya alama hiyo, alikata mkono wake ili kuwa huru kuliko kumtumikia adui yake. Katika maisha yetu ya imani kwa Kristo na ufuasi, tumeacha nini au kitu gani? Au tumeweka yote katika kapu moja? Yaani ya kwetu na ya Mungu? Je, leo tuna ujasiri wa kusema kama Mt. Petro – sisi tulioacha vyote tutapata nini?
Tumsifu Yesu Kristo.