Tafakari: Imani inamwilishwa katika huduma ya mapendo!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Yesu anasema: “Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu”
Masomo kwa ufupi Somo la kwanza (Is. 53:10-11) Katika kitabu cha nabii Isaya kuna vifungu vinne vinavyoeleza dhamira ya Mtumishi wa Bwana. Vifungu hivi huitwa Nyimbo za Mtumishi wa Bwana. Nyimbo hizi hueleza utume wa huyo mtumishi wa Bwana, mateso yake, kutukuzwa kwake na zinataja sifa alizonazo huyo mtumishi; upole, utii na unyenyekevu kwa Mungu. Somo letu la kwanza leo ni sehemu ya wimbo wa mwisho wa huyo mtumishi ambapo baada ya yote ambayo mtumishi ameyapitia na baada ya kifo chake, watu wanayatafakari yote hayo kupata maana yake-ni kwa nini ameyapitia yote hayo na kwa lengo gani. Wanachokiona waziwazi ni kuwa mtumishi ameyapitia yote hayo kwa sababu ilikuwa ni mapenzi ya Mungu, “Bwana aliridhia kumchubua, amemhuzunisha” ili abebe hatia ya taifa zima. Yeye aangamie, taifa liokoke.
Tunapomtafasiri mtumishi huyu kama kiwakilishi cha taifa zima la Israeli na kuyaona mateso yake kama mateso waliyokuwa wakiyapitia Waisraeli katika kipindi cha historia yao, ujumbe wa Nabii Isaya kwao katika kifungu hiki ni kuwa Bwana aliridhia wayapitie hayo kwa ajili ya ustawi wa Taifa lake kubwa zaidi ambalo ni watu wote wanaomwamini na watakaomwamini. Pamoja na tafsiri hii, Jumuiya ya Kikristo tangu mwanzo imeipa tafsiri ya kimasiha taswira hii ya mtumishi wa Bwana. Hivyo imeona katika mateso ya mtumishi wa Bwana mpango mzima wa Mungu wa kupokea kama maondoleo ya dhambi si tena sadaka za kuteketezwa za wanyama bali sadaka ya mwanadamu na tena mwanadamu asiye na doa na aliyehiari mwenyewe kujitoa sadaka yaani Kristo Mwana wa Mungu, Masiya.
Somo la pili (Ebr. 4:14-16) Somo letu la pili, waraka kwa Waebrania, linaanza kwa kuwaalika waamini kuyashika maungamo yao - “tuyashike sana maungamo yetu”. Kuyashika maungamo yaani kushika kile tunachokiri, kushika tunachoungama katika imani, kuishika imani. Na hasa kinachosisitizwa ni kushika imani katika Kristo, kuhani mkuu na kushikamana naye kabisa. Kwa nini? Msingi wa kufanya hivyo ni aina ya kuhani aliye Kristo; ni binadamu kama sisi na hapo hapo ni mwana wa Mungu, ni Mungu. Kwa sababu ya ubinadamu wake Yesu anaweza kuchukuliana na sisi katika ubinadamu wetu; anaufahamu. Anaufahamu kuwa ni ubinadamu uliodhaifu na unaohitaji msaada na huruma. Na kwa sababu ya umungu wake yeye anao uwezo huo wa kutusaidia katika sala na maombi yetu. Ndivyo walivyoeleza pia mababa wa Kanisa kuhusu Kristo, “alikuwa kama sisi, atatusaidia: hakuwa kama sisi, anaweza”.
Injili (Mk 10:35-45) Katika injili ya leo mitume wawili, Yakobo na Yohana wanaomba nafasi ya heshima wakati Yesu atakapochukua utukufu wake. Inawezekana kuwa wao pia walikuwa na mawazo kuwa Yesu amekuja kuanzisha enzi mpya ya utawala wa kisiasa na kuwapindua Warumi waliokuwa wakiwatawala katika kipindi hicho. Ndiyo maana Yesu anawaambia “Hamjui mnaloliomba”. Na hapo anawaambia utukufu anaoweza kuwapa yeye ni ule tu unaokuja baada ya msalaba. Ndio anawauliza “mnaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi”. Wanasema tunaweza. Yesu anawatabiria kuwa ni kweli watakinywea. Katika Mdo. 12:2 tunaona kuwa Yakobo aliuwawa Yerusalem. Na tena utukufu huo anaowapa baada ya Msalaba hasa sio yeye anaowapa bali ni Mungu. na hii iaonesha kuwa nyuma ya yote anayoyatenda Kristo yupo Mungu. Ndiye anayeamua ni nani ampe nafasi ipi katika kushiriki utukufu wa Kristo. Injili inaonesha pia fundisho muhimu analoliongeza Kristo, “Mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu” kusisitiza roho ya utumishi. Na kitu anachopaswa kukiomba mtumishi ni kutumikia sio ukubwa.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanatualika tuitwae roho ya utumishi. Tuitwae roho ya utumishi katika ukristo wetu, tuitwae roho ya utumishi katika kuiishi imani yetu na tuitwae roho ya utumishi katika kuwa kwetu kanisa. Roho hii ya utumishi iwe ni sifa inayoonekana katika na iwe moja ya sifa zilizo wazi kabisa zinazolitambusha Kanisa.
Roho hiii ya utumishi tunaalikwa tuitwae kwa sababu ndiyo roho iliyomwezesha Kristo kuyatimiza mapenzi ya Mungu, kutimiza kile alichokuwa amekisudia Mungu kwa ulimwengu na katika kumtuma yeye ulimwengu. Ndiye ambaye utabiri wa Nabii isaya kuhusu mtumishi wa Bwana unatimia kikamilifu kabisa kwake. Ndiye yeye hasa yule mtumishi ambaye licha ya kuwa hakuwa na hatia alipokea mateso na aibu kubwa kwa ajili ya kulikomboa taifa zima la Mungu. Ni kwa roho hii hii ya utumishi hakusita kusema waziwazi “kama Baba alivyonituma…. Chakula changu ni kutimiza mapenzi ya Baba yangu…. Ili nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa baba…. na katika injili ya leo anasisitiza kuwa mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa bali kutumikia na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi”.
Injili ya leo inatuonesha watu waliokuwa karibu kabisa na Kristo, mitume wake wawili Yakobo na Yohane, ambao huenda pamoja na mitume wengine pia hawakupokea na hawakumwelewa kabisa Kristo alipokuwa akizungumza kwamba atahukumiwa, atateswa na atauawa. Inawezekana bado walikuwa wanamfuata kama kumfuata mtu mashuhuri ambaye hapo mwishoni watafanikiwa kuwa nao mashuhuri na kupata nafasi za heshima mbele ya watu. Kukosekana kwa roho ya utumishi ambayo mwishoni Yesu anawaalika wanafunzi wake wote kunakuwa ni chanzo cha kutokumwelewa Yesu, kutokuelewa fumbo la Mateso yake na umuhimu wake, kunakuwa ni chanzo pia cha kutokumwamini.
Papa Francisko anatufundisha kuwa imani ya kikristo huwezi kuitofautisha na utumishi, huwezi kuitofautisha na kuhudumia. Imani na huduma vinaendana. Na daima huongeza kusisitiza kuwa katika kanisa hatualikwi tu kuhudumia mara nyingi bali tunaaliwa kuishi kwa kuhudumia, na huko ndiko kutwaa roho ya utumishi, roho ya huduma. Kwa wahudumu wa daraja na walio katika maisha ya wakfu, Papa Francisko haachi kukumbusha kuwa kuishi roho ya utumishi na huduma ni kwanza kuwepo pale wanapohitajika: kuwa tayari kutoa huduma na tena si kuweka mazingira ya wao kufuatwa bali wao kuwatafuta “kondoo” na kutokuogopa kunukia harufu ya “kondoo”. Tena kuwa na roho ya utumishi ni kukumbuka daima kuwa mhudumu wa daraja si mmiliki wa neema za Mungu, si mmiliki wa mafumbo matakatifu anayoadhimisha, yeye ni mhudumu, ni mgawaji na mlinzi wake. Kumbe furaha yake iwe ni kufungua milango ili wale wanaotafuta kwa moyo radhi, kwa nia na kwa njia ambazo kanisa limeaminishwa waweze kuzipata.
Kanisa huwaalika daima waamini walei kuishi roho ya utumishi na huduma katika ushuhuda wa imani yao. Na tena huwaalika kuwa motomoto katika kuushiriki utume wa kanisa kwa majitoleo yao mbalimbali na kwa kushiriki moja kwa moja katika utume uleule wa Kanisa. Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaeleza kuwa walei wanaitwa kwa namna ya pekee kuonesha uwepo wa kanisa na utendaji wake mahali na katika mazingira yale ambamo lenyewe haliwezi kuwa chumvi ya dunia, isipokuwa kwa njia yao tu. Hivyo kila mlei kwa sababu ya vipaji vyenyewe alivyopewa anakuwa ni shahidi na wakati huo huo chombo hai cha utume wa Kanisa lenyewe kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo (Lumen Gentium, 33). Katika roho ya utumishi na huduma, tujibidiishe kuiishi imani yetu na tuzidi kufanana naye zaidi katika kuwahudumia aliokuja kuwakomboa.