Rudini nyumbani kumenoga! Toba na wongofu wa ndani!
Na Padre William Bahitwa. – Vatican.
Napenda kuchukua fursa hii ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika wasaa huu, ili kuweza kujiunga na Mababa wa Sinodi kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Sinodi yaliyokuwa yanaongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” Kwa sasa tunasubiri nyaraka kuu mbili: Mapendekezo kutoka kwa Mababa wa Sinodi pamoja na Barua ya Mababa wa Sinodi kwa ajili ya vijana wote duniani. Sinodi sasa imenoga, kwani, huu ni wakati wa kuanza kujipanga ili kumwilisha maazimio haya katika maisha na utume wa Kanisa!
Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Jer. 31:7-9) Mwenyezi Mungu kwa kinywa cha nabii Yeremia anaahidi kuwarudisha nyumbani wana wa Israeli waliokuwa utumwani, mbali na nchi yao. Watakaporudi, Mungu anawaambia kuwa ni yeye mwenyewe atakayewaongoza katika safari hiyo ya kutoka utumwani. Atatangulia kama kiongozi wa msafara wa taifa lake kama alivyofanya zamani alipowatoa Misri; “tazama nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia”. Tunaona mwangwi wa Zaburi ya 23 ambapo Mzaburi anakiri na kujiaminisha kuwa Bwana aliye mchungaji wake, aliye kiongozi wake na hivyo hatapungukiwa kitu: “nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji katika njia iliyonyoka, katika njia hiyo hawatajikwaa”.
Mwenyezi Mungu kukazia kuwapa ujumbe wa furaha kuwa atawarudisha nyumbani ni kuwakumbusha juu ya nafasi ya pekee waliyonayo kwake; ni nafasi pendwa kama ya mwana mzaliwa wa kwanza: “maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mwana mzaliwa wa kwanza wangu”. Ahadi ya kuwarudisha nyumbani waisraeli inaonesha jinsi gani wokovu - ukombozi wa Mungu kuwa sio kitu cha kiroho tu. Wokovu na ukombozi ni hasa wa kiroho lakini unayo mafaa ya kimwili pia. Unahusika na maisha yao yote, kiroho na kimwili.
Somo la pili (Ebr. 5: 1-6) linaeleza na kufafanua ukuhani mkuu wa Kristo. Kutoka katika ukuhani wa Haruni, ukuhani wa kurithi na ambao ndio ulikuwa ukuhani uliozoeleka na unaofahamika, waraka kwa Waebrania unamwonesha Kristo kama kuhani mkuu aliyeteleza majukumu yale yale ya kikuhani lakini kwa namna ya juu zaidi na kwa namna kamilifu zaidi. Ndiyo maana hatwai mlolongo wa Haruni bali ule wa Melkizedeki naye ni kuhani milele.
Injili (Mk 10:46-52) Injili ya leo inazungumzia muujiza wa uponyaji wa kipofu aliyeitwa Bartimayo. Ni muujiza kama ilivyo miujiza mingine ambapo Yesu anatangaza ujio wa ufalme wa Mungu na hapo hapo kutoa mwaliko wa imani. Awali tunamwona Bartimayo mwombaji asiyeona. Mbele yake ni giza, haoni na hajui nani yuko jirani yake. Ni kipofu na amekaa kando ya njia. Aliposikia kwamba Yesu anapita alipaza sauti kumwomba Yesu amrehemu, na licha ya kuzuiwa yeye aliendelea hadi pale Yesu aliposikia. Akamwita, akazungumza naye na akamponya. Mwisho Bartimayo akaona na akamfuata Yesu njiani. Kumbe, kutoka katika hali yake ya awali ya kipofu aliyekaa kando ya njia Bartimayo akawa anayeona na anayemfuata Yesu njiani. Kutoka kutokuona hadi kuona; kutoka kukaa hadi kutembea, na kutoka kuwa pembeni ya njia hadi kuwa kwenye njia hasa yaani kushiriki kikamilifu katika kumfuasa Kristo.
Huu ndio uponyaji alioupokea Bartimayo, uponyaji ambao Yesu anaposema “imani yako imekuponya” anatangaza si kwa Bartimayo bali kwa wote uponyaji ambao imani inaweza kuuleta ndani yake anayeamini. Kutoka katika giza la maisha ambapo mtu haoni mwanga wa matumaini au mabadiliko, kutoka katika hali ya kudumaa kiroho hadi kuanza safari ya ukuaji na kutoka katika hali ya kukaa pembezoni hadi kuwa mshiriki hai katika Kanisa, katika jumuiya ya waamini - jumuiya ya wanaomfuasa Kristo.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, ninawaalika katika dominika hii ya 30 ya mwaka B, tuielekeze tafakari yetu katika dhana ya “kurudi nyumbani”, dhana ambayo Mungu mwenyewe tumesikia anawatangazia waisraeli kwa kinywa cha Nabii Yeremia katika somo la kwanza. Kwa Waisraeli dhana hii - nyumbani- ilibeba maana nzito sana. Kwao nyumbani ni katika nchi yao ya ahadi, ni katika ardhi ile ambayo Bwana aliwapa tangu enzi ya wazee wao, ndipo hapo ulipokuwa moyo wao wote. Ndipo ilipokuwa historia yao na ndipo walipoiona maana ya uwepo wao na uhusiano walionao na Mungu wao. Ndiyo maana kila walipotoka nyumbani kwao, nje ya ardhi yao mambo hayakuwaendea vizuri.
Utulivu na amani yao waliipata tu waliporudi nyumbani. Ndivyo ilivyokuwa waliopotoka nyumbani kwenda kutafuta chakula Misri na baadaye kuhamia huko kumfuata Yosefu, waliishia kufanywa watumwa na kutumikishwa hadi pale Mungu mwenyewe alipowatoa utumwani kwa mkono wa nguvu. Hata baadaye walipokuwa uhamishoni, utumwani Babiloni, uchungu wao mkubwa ulikuwa ni kuwa nje ya nyumbani. Nje ya ardhi yao, ndiyo maana katika Zaburi 137 wanasema “Kando ya mito ya Babeli tuliketi tukalia tulipokumbuka Sayuni...tuimbeje wimbo wa Bwana tukiwa ugenini...Ee Yerusalemu nikikusahau mkono wangu wa kuume unyauke...” Hivyo ujumbe wa manabii wa kurudi nyumbani Waisraeli wameupokea kwa maana nzito ya kurudi si tu katika ardhi bali pia katika mahusiano naMungu wao, kurudi katika Agano waliloweka naye na kurudi katika ngome salama ya upendo wa Mungu.
Utamaduni wa Kikristo umeichukua dhana hii ya kurudi nyumbani na kuitumia katika maisha ya kiroho. Inatumika kualika wongofu; kuongokea imani na pia kuendelea na safari ya imani inayomrudisha mtu nyumbani kwa Baba mwenye upendo na huruma nyingi asiyetaka yoyote apotee nje bali anayetaka wote wamtafute, wampate na wawe na uzima wa milele. Ni hapa pia kilipo kiini cha zoezi la kiroho liitwalo Hija.
Nyumbani kwetu sisi tunaomwamini Kristo ni wapi? Sisi waisraeli wa Agano jipya aliloliweka Kristo Kuhani mkuu kwa damu yake Msalabani? Tunaweza kupaona kuwa ni Yerusalemu mpya, nchi ya ahadi ya wote wanaomwamini Kristo na wanaoishi maisha yao wakimtumaini yeye. Pamoja na hayo, katika ngazi ya ufuasi, katika safari ya imani iliyoanza kwa ubatizo wetu, nyumbani kwetu ni ile hali ya neema ya utakaso. Ndiyo hali tuliyoipokea kama ahadi ya wote wanaoamini na kubatizwa. Kuishi katika neema ya utakaso, kuishi katika muungano na Mungu, kuishi katika mahusiano na Mungu.
Kumbe, tunapotafakari leo thamani waliyokuwa nayo Waisraeli katika nchi yao ya ahadi, thamani iliyowafanya waupokee kirahisi ujumbe wa unabii, ujumbe wake Mungu nasi tunavutwa leo kuweka mbele yetu daima hali ya maisha ya neema kama matamanio yetu nambari moja. Kuweka hali hiyo mbele yetu ni kuona kuwa nje ya muungano na Mungu, nje ya hali ya neema hatuna nguvu, hatuna thamani, hatuna historia na tuko ugenini daima na tena ugeni unaotuweka mateka na unaotupoteza hata kama unatuonesha mafanikio hapa mwanzo. Safari ya imani yetu iwe ni safari daima ya kurudi, yaani kuutafuta wongofu kila siku, na kila wakati tunapojiona nje ya hali yetu ya neema ya mwanzo.
Shauku hiyo ya kurudi nyumbani, kurudi katika hali ya neema ya utakaso ndiyo itatusukuma daima kutafuta upatanisho naye, ndiyo itakayotufungua mioyo kulipokea Neno lake na ndiyo itaimarisha imani yetu, na kutuwezesha kuona nguvu kubwa iliyonayo imani yetu, nguvu ya kutuunda daima upya na kutufanya washiriki hai wa kazi ya ukombozi ya Kristo. Siku ya Jumapili, tarehe 28 Oktoba 2018, Mama Kanisa anafunga maadhimisho ya Sinodi ya Vijana kwa Ibada ya Misa Takatifu. Ni matumaini yetu kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, imekuwa ni fursa kwa Kanisa kujikita katika sala, tafakari, toba na wongofu wa kimisionari, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha na matumaini kwa watu wa Mataifa!