Kifo ni kizungumkuti!
Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Vatican.
Huko Yerusalemu – Nchi Takatifu, makaburi ya marehemu yanatambulikana kwa alama iliyowekwa juu yake. Alama hizo zinaonesha matumaini waliyonayo watu hao. Mathalani juu ya kaburi la Myahudi kumewekwa mawe, ikiwa kama kumbukumbu ya mawe ya altare aliyotumia Abrahamu kumtolea mwanae Isaak kwa Mungu. Pia ni alama ya makao ya kudumu ya marehemu na ya usawa kwa wote. Juu ya makaburi ya Waislamu (Waarabu) kumewekwa matawi alama ya ushindi na amani ya paradisi. Kumbe juu ya kaburi la mkristu kumesimikwa msalaba ishara ya upendo. Leo tunapowakumbuka marehemu wetu tunawaombea wale wote ambao walipokuwa na mwili huu walibahatika kumjua Kristo na Injili yake ya upendo na wakawa na furaha na matumaini katika Msalaba. Tunawaombea pia wale ambao hawakuangazwa na mwanga huo wa msalaba.
Mfu na marehemu ni maneno mawili tunayotumia kumwita mtu aliyekufa, na mwili wake unaitwa maiti. Mfu ni jina la heshima kwa mtu aliyekufa, kumbe kwa mnyama aliyekufa tunaita mzoga. Maiti na mzoga ni kiumbe kilichopoteza uzima na uhai. Kumbe neno Marehemu linatokana na rehema-huruma linamaanisha mtu aliyerehemiwa au kuhurumiwa. Neno hilo lingefanana na la kilatini defungor (defungi) au kwa kiingereza defunct lenye maana ya kufikia kilele, mwisho, hatima, kukomaa, kuiva au ukamilifu. Kwa hiyo mwisho wa maisha haya ya mwili (ulimwengu) siyo kufa bali ni kukomaa au kukamilika.
Ndugu zangu kifo ni kizungumkuti. Binadamu anayahangaikia sana maisha yake lakini mwisho wa pilikapilika zote, anaona uhai wake unagota na kufikia hatima. Ama kweli, asiyejua kifo aangalie kaburi”. Kwa hiyo kutokana na akili zake, binadamu daima amejiuliza, kulikoni maisha yagote wakati bado kuna matumaini ya kuishi? Ama kweli binadamu anao ugonjwa wa kusahau–Arzheimer. Binadamu anashindwa kukumbuka kuwa akitaka kuwa na maisha ya kiutu, hana budi kuikabili pia hatima yake. Yaani kuyafuatilia maisha yako na kufikiria hatima yake kutoka pale unaposherekea birthday yako. Bila hivyo maisha yanakosa maana na matumaini na unaishia kuhangaika mambo yanapokuendea kombo.
Ndivyo inavyokuwa pale kifo kinapokubana kwenye kona hadi usijue kwa kukimbilia, unabaki kuhaha kama ngiri aliyezingirwa na mbwa pamoja na wawindaji. Hapo unamwona mkristu anashika moyo, anahangaika kumwomba Mungu na watakatifu ili wairushie mbele mihadi ya kifo, yaani kifo kisogezwe mbele. Ndivyo walivyofanya Marta na Maria walimjia juu Bwana Yesu wa sababu hakukizuia kifo kumfika kaka yao Lazaro. Kumbe wasijue kwamba Yesu hakufika duniani kuyaendeleza maisha ya kibaolojia bali kushinda mauti.
Aidha katika historia, binadamu amejaribu kukitafakari kifo na kukitafutia ufumbuzi bila kupata jibu lenye tija. Mathalani Wamesopotamia, waliilaumu sana miungu yao kwa vile yenyewe ilijibakizia uzima na kuwapatia kifo wanadamu. Kadhalika wanafalsafa wa Ugiriki, kama akina Filo na Socrates walikiainisha kifo kuwa ni kuyeyuka kwa mwili na kuwa vumbi ila mtima tu ndiyo haufi. Hata hivyo wanafalsafa hao walipata taabu sana kuelezea huko kutokufa kwa mtima kunakuwaje? Ndivyo tunavyosaliwa Wakristu tunapopakwa majivu siku ya Jumatano ya Majivu: “Binadamu kumbuka kuwa wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi” na wakati wa kutia udongo kaburini kwa marehemu wakati wa mazishi Kiongozi anasema: “Binadamu wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi, lakini Bwana atakufufua siku ya mwisho.” Fikra hii ni zuri lakini hakieleweki. Yaani haileti matumaini kwani tunanaendelea kujisikia bado gizani mwa ulimwengu huu kama mtuhumiwa anayesota lumande.
Kumbe hatima nzuri ya binadamu yaani kifo chake, ilianza kupata mwanga kwa njia ya Wayahudi (Manabii na Zaburi). Wayahudi walikitafakari kifo kwa kutumia kigezo cha mahusiano ya upendo kati ya Mungu na binadamu. Kwamba Mungu ameingia katika mahusiano ya upendo na binadamu na ametupatia mwanya wa kuwasiliana naye. Kwa njia ya upendo huo Mungu hawezi kamwe kutuacha sisi binadamu. Kijumla mpenda kwa mpendwa wake hawezi kufanya zaidi isipokuwa kumpenda tu basi. Kwa hiyo Mungu akinipenda nami nikimpenda hapo kimeeleweka na pendo hilo litadumu daima. Ndivyo Mungu alivyowaambia Waisraeli: “Wewe ni mzuri machoni pangu, unayo thamani sana, ninakupenda.” (Isaya).
Katika Injili ya leo unaouona wazi mpango huo wa upendo wa Mungu tunaposimuliwa juu ya mkate wa uzima (Yoh 6). Mpango wa upendo wa Mungu unaonekana Yesu anaposema: “Mapenzi ya Baba”. Maneno hayo anayarudiwa karibu mara nne juu ya zawadi ambayo Mungu alimpatia mpendwa wake binadamu. Mosi, Yesu anasema: “Chochote ambacho Mungu ananipa kitakuja kwangu. Anayekuja kwangu mimi simtupi nje kamwe.” Hapa ndipo unapoanza huo mradi wa Baba wa kumkabidhi na kumwaminisha Yesu bila masherti ubinadamu wote (wema na ubaya wa binadamu). Kwa hiyo ili kuupata wokovu, inatakiwa kuingia katika mahusiano ya upendo na Yesu.
Pili, Yesu anasema “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” Yesu alifika duniani kutekeleza mradi moja tu wa kuja kuwekeza upendo wa Baba yake. Yaani kuendeleza mahusiano hayo ya upendo yaliyoanza kutoka pale Mungu alipomweka duniani kiumbe wake binadamu anayempenda. Katika kuwekeza huko Yesu anaendelea kusema: “Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja,” Upendo wa Mungu unayo malengo ya kuuteka ubinadamu wote kwa njia ya Kristu, pamoja naye na ndani yake katika mahusiano hayo ya upendo na umilele. Hivi katika mradi huo wa uwekezaji wa upendo, Yesu anao uhakika wa kushinda kidedea.
Tatu, Yesu anasema: “bali nimfufue siku ya mwisho.” Hiyo siku ya mwisho siyo siku ya kiyama bali ni Kalvario. Pale ambapo Yesu kama kilele cha upendo wake anaitoa Roho yake parentopneuma (akatoa roho yake). Roho ni maisha ya kimungu ya Yesu. Yaani nguvu ya upendo aliyoikuza katika maisha yake ya umilele. Siku ya mwisho Yesu anatoa maisha yake ya milele anapoingia katika mahusiano ya upendo na Mungu kwa njia ya kifo chake Msalabani. Aidha, mapenzi hayo ya Baba yanajidhihirisha kwa namna tatu kama anavyosema Yesu mwenyewe: “Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.” Kwa hiyo namna ya kwanza ni “kila amtazamaye Mwana.” Kumbe inatakiwa kwanza kumtazama Mwana. Na Mwana maana yake ni kule kufanana na Baba.
Yesu anaionesha waziwazi kwa ukamilifu wote hali hiyo ya umwana ya kufanana na sura ya Baba yake katika upendo. Kwa hiyo inatakiwa kwanza kumwangalia na kumtazama yeye kama tunavyosoma Waraka wa Yohane: “Kile tulichokiona kwa macho yetu, kile tulichokitafakari, kile ambacho mikono yetu imekigusa, kuwa ni Neno la uhai, kwa vile uzima ulijionesha humo, nasi tukauona.” (IYoh). Leo sisi hatuwezi kufanya mang’amuzi ya kuona kwa macho kama ilivyokuwa kwa wanafunzi walioishi na Yesu. Lakini tunaweza kuona kwa njia ya Neno lake. Yaani kulitambua Neno la Mungu jinsi linavyowakilishwa na Yesu katika Injili na kuitambua sura ya Baba. Kwa kufanya hivyo tu tutaweza kuyaona mapenzi ya Baba.
Namna ya pili ni kule kumwamini Yesu. Kumwamini haina maana ya kumsadiki tu kwamba alifika ulimwenguni na kufanya miujiza. La hasha, bali kumkiri na kumtambua kuwa ni Mwana, na kuishi kama alivyoishi yeye. Namna ya tatu ni kwa yule aliyeona hiyo sura ya Mungu katika Yesu na kumwaminia sasa Yesu anamwambia: “nami nitamfufuka siku ya mwisho.” Maisha hayo hatuyapewi pale tunapokufa, bali tunapewa sasa.
Ndugu zangu leo ni sikukuu ya wenzetu waliorehemika, waliokomaa na kukamilika katika Bwana. Inatupasa sisi tuwe na mahusiano ya dhati na wenzetu waliozaliwa upande mwingine wa maisha yasiyoguswa na kifo. Kwa vyovyote siyo marehemu wote wanayo haki, yaani walimtambua na kumpokea huyo mwekezaji wa upendo wa Mungu na kufuata mapendekezo yake ya maisha ya kimungu. Wengi wao walishindwa kuiona sura ya Mungu katika Kristu na kumwamini, yaani maisha yao hayakuwa makamilifu. Lakini wengine walijitahidi kukamilika dakika za lala salama. Tusiwaombee kwa kusema eti tunawatakia mema na kuwapenda marehemu wetu. La hasha, tukumbuke msemo tunaoutumia sisi wenyewe tunapotoa pole kwa msiba: “Sisi tulimpenda, lakini Mungu amempenda zaidi.”
Maana yake, Mungu amewachukua kwake kwa sababu anawapenda zaidi kuliko tunavyowapenda sisi. Kwa upande wao marehemu wanabaki kuwa na mahusiano na mawasiliano ya upendo nasi kwa sababu hawawezi tena kufa. Lakini kwa vile sisi kwa macho yetu ya kimwili hatuwezi kuuona mwili wao wa ufufuo, basi sala zetu, upendo wetu na hata msamaha wetu kwao unaweza kuwasaidia wawe na furaha. Hivi wanaweza kuikamilisha safari ile ambayo pengine hawakuimalizia walipokuwa katika maisha haya. Sisi tunaweza sasa kuendeleza jema lile walilolifanya, hata kusahihisha makosa ambayo waliyatenda. Hilo ndilo tendo tunaloliita “kuwaenzi marehemu” wetu walio katika nyumba ya Baba ambako sisi sote tumeitwa kuingia, si kwa mastahili yetu, bali kwa sababu pendo liko katika mpango wa mapenzi ya Baba yetu. “Uwape Ee Bwana raha ya milele. Na Mwanga milele uwaangaze. Wastarehe kwa amani. Amina.”