Tafuta

Kipindi cha Majilio: Ujio wa kwanza wa Kristo katika Fumbo la Umwilisho! Ujio wa Pili ni Hukumu! Kipindi cha Majilio: Ujio wa kwanza wa Kristo katika Fumbo la Umwilisho! Ujio wa Pili ni Hukumu! 

Kipindi cha Majilio: Jiandaeni vyema kukutana na Kristo Yesu!

Jumapili ya kwanza ya kipindi cha Majilio inaufungua rasmi Mwaka Mpya wa Kanisa, hija ya maisha ya imani, matumaini na mapendo; inayowakumbusha waamini, Fumbo la Umwilisho na Siku ya ile ya mwisho, Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, kama waamini wanavyosali katika Kanuni ya Imani. Majilio linaunganisha mwili na roho vinaunganika kwa pamoja.

Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.

Mama Kanisa Mtakatifu sana anatualika kuingia katika Mwaka mpya, Mwaka C wa Kanisa. Hii ni ishara ya upyaishaji wa daima wa maisha ya Kanisa na hivyo kulifanya kuonekana daima jipya na linalopendeza. Mwaka mpya wa Kanisa uanza kwa kipindi cha Majilio. Neno “majilio” linajieleza lenyewe kuwa ni tendo la kufika au kuingia kwa kitu au jambo fulani na kunapokuwa na ujio bila shaka kunakuwa na wanaongojea. Kwa upande wa wale wangojeao hujikita katika maandalizi ili kumpokea huyo ajaye. Kiongozi mkubwa anapotarajiwa kufika mahali fulani basi jamii inayomngoja itajikita katika maandalizi ya miundo mbinu, chakula na vinywaji na hata maandalizi ya kimwili. Kwetu sisi Wakristo tunajiandaa au tunangojea ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunajiandaa kwa ujio wake kwani Yeye ndiye kitovu cha safari nzima ya Mwaka wa kiliturujia. Hii ni kwa sababu shabaha ya Mwaka wa kiliturujia wa Kanisa imejikita katika fumbo la ukombozi wa Mwanadamu ambalo linafumbatwa katika nafsi ya Kristo.

Kristo amekwishakuja ulimenguni; sasa tutajiuliza tunangojea nini au ni ujio gani huo? Hili linaelezeka kwa kukiangalia kipindi hiki ambacho kinagawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inatutafakarisha juu ya ujio wa pili wa Kristo. Ujio wake huu wa pili ni wa hakika kwani Mwenyewe aliahidi akisema: “Nakwenda kwa Baba kuwaandalia mahali… nitakuja tena kuwakaribisha kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo” (Yoh 14:2b, 3b). Hivyo maandalizi yetu yanajikita katika kuungojea huo ujio wake wa pili. Sehemu ya pili ambayo inaanza tarehe 17 Desemba inajikita katika maandalizi ya Sherehe ya Noeli ambayo inakusudia kulifanya hai tendo la Kristo kuzaliwa kati yetu zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Adhimisho hilo linamwingiza Kristo katika nyua za mioyo yetu na hivyo anakuwa kweli kielelezo na kitovu cha safari yetu ya Mwaka huu mpya wa Kanisa tunaouanza.

Masomo ya Dominika hii ya kwanza ya Mwaka wa Kanisa yanatuingiza katika tafakari ya sehemu ya kwanza ya kipindi cha Majilio, yaani ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la kwanza linaonesha kuwa kipindi hiki ni kipindi cha kungojea utimilifu wa ahadi ya Mungu. Kile ambacho amekipanda kitachipushwa ikiwa ni ishara ya kuzaa matunda na kukua. Hali hii ya matarajio ya kuchipuka kwa mbegu iliyopandwa kinahitaji mazingira stahiki ikiwa pamoja na rutuba, hali nzuri ya hewa lakini pia mabadiliko ndani ya mbegu yenyewe. Mama mjamzito angojeaye kuzaliwa kwa mtoto hujiwekea maandalizi mazuri kwa ajili ya mtoto kukua vema tumboni kwa kumpatia lishe bora lakini pia kwa kujiweka yeye binafsi katika hali ya usalama.

Kipindi cha Majilio katika muktadha huo kinapokea tabia mbili. Kwanza kinakuwa ni kipindi cha kujitafakari tulipotoka na kuangalia pale mmoja alipoanguka basi kutafuta suluhisho muafaka na pale alipofanya vyema basi ni kuimarisha zaidi. Hii ni kwa sababu kipindi hiki ni mahususi kwa ajili ya kuanza tena katika hali ya kiimani. Ni wakati wa kuiwasha taa iliyofifia.

Tabia nyingine inayoonekana ni tendo la toba. Mmoja anajikabidhi kwa Mungu ili kupata utakaso na hivyo kutoa nafasi mbegu ya imani iliyopandwa ndani yake iweze kukua. Tabia hizi ni muhimu sana kwa ajili ya mabadiliko ya kweli na kutupeleka katika kuupokea ujio wa Kristo mara ya pili tukiwa tumechipuka, kukua na kuzaa matunda. Mwanzo mpya wa safari ya kiimani katika kipindi hiki maridhawa ni fursa ya kujiandaa tena ili kujiweka tayari kuipokea siku hiyo ya ujio wa Bwana.

Somo la Injili linatuonya dhidi ya matendo yetu ya kila siku yanayopindisha maadili na hivyo kutoa nafasi finyu kwa kuchipuka kwa mbegu ya imani iliyopandwa ndani mwetu. Kristo anatuambia kuwa siku hiyo itakapofika “changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia”. Uchangamfu huo na namna ya kuinuia vichwa unajionesha katika kuepuka kuelemewa na “ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya” kusudi siku hiyo isije kutufikia ghafula “kama mtego unasavyo”. Kwa ujio wa kwanza wa Kristo, kama tunavyoelezewa na Prefasio ya kipindi hichi cha Majilio, ni kwamba “alitufungulia njia ya wokovu wa milele…tunangojea kwa hamu siku ile atakapokuja mara ya pili katika utukufu wake, tupewe tunayongojea tukikesha kwa imani”. Hili ni dokezo kwamba tumekwisha wezeshwa kwa kupandwa ndani mwetu mbegu ya neema ambayo tunapaswa kuifanya kuwa hai wakati wote. Njia ya kuufikia mwisho huo mzuri imeshafunguliwa kwa tendo la wokovu la Kristo.

Kristo anatuonya akitutaka kuwa na taadhari ili mioyo yetu isilemewe na uovu na kujisahau kujiweka tayari na kukutwa ghafla na siku ya ujio wake wa pili tukiwa hatujajiandaa. Himizo hili la kimaadili linanuia kufufua ndani mwetu uhai wa kiimani kwa kuwa tayari wakati wote kuwa mashahidi wa Injili ya Kristo. Hapa inaoneshwa kuwa Kristo hapendi siku hiyo imkute mmoja hajajiandaa na hivyo kuangukia katika adhabu. Hili linaithibitisha kiu ya Mungu ambaye hapendi watu wake wapotee bali wote wafikie uzima wa milele. Kwa maneno mengine Mungu anaufunua upendo wake na kudhihirisha kuwa ni upendo wa milele. Daima yupo pamoja nasi anatuhangaikia na kutugutusha kutokutumbukia katika maangamizi. Hapa tunaona kuwa ingawa Kristo anaongea nasi kama onyo lakini ni tendo linalotupatia matumaini ya ulinzi wa daima wa mwenyezi Mungu.

Hivyo wakati huu wa Majilio ni fursa ya kujitafakari jinsi tunavyopaswa kusafiri na Kristo hatua kwa hatua kusudi kuweza kuifikia siku hiyo ya ujio wake wa pili. Mtume Paulo anatueleza katika Waraka wake kwa Wathesalonike kuwa tuutafute uongozi wa Mungu. “Mungu awaongoze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu”. Njia hii ya kuukuza upendo wa kindugu ni nyenzo ya kutupeleka katika maadili mema ambayo ndiyo udongo mzuri na hali ya hewa inayofaa kufanya chipukizi la mbegu ya imani iliyopandwa ndani mwa kila mmoja kuchipuka. Hii inawezeshwa na utii wetu kwa mafundisho ya Kristo. Safari ya Majilio kama nilivyoeleza hapo awali inanuia kutuanzisha upya na kutupeleka katika ukomavu unaowapasa wana wa Mungu katika Kristo.

Wakati wa kuanza kwa majira haya ni vema kila mmoja wetu kujiwekea malengo ya kujiimarisha katika fadhila fulani au jambo jema fulani ambalo limekuwa linalegalega. Tuchukulie mathalani mmoja anaweza kujiona kuwa yu mgumu katika kutoa msamaha, basi achukue fursa hii kuomba toba na kuomba neema ya Mungu kwa kuanza kujizoesha msamaha kwa wenzake. Majira yote yatakayofuata kwa kipindi cha mwaka mzima iwe ni fursa kwake kujiimarisha katika tendo la msamaha hadi mwishoni mwa mwaka huu ajione kuwa ameimarika katika tendo hilo. Hii inamaanisha kuwa vipindi hivi vya mwaka wa liturujia wa Kanisa visitupite tu kama kumbukumbu bali viadhimishwe ndani ya nafsi zetu na kuacha alama ya kudumu ambayo itatupeleka kukua zaidi katika wokovu.

Kipindi cha Majilio
30 November 2018, 07:31