Tafuta

Sherehe ya Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. Sherehe ya Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. 

Ufalme wa Kristo unafumbatwa katika: utukufu, kweli na haki!

Utawala wa Kristo ni utawala wa kimungu ambao unanuia kutupatia uzima wa milele, kutukomboa kutoka uovu, na kuungamamiza utawala wa dhambi. Ni utawala wa upendo unaweza kuustawisha wema kutoka katika ubaya. Ufalme ambao unaondoa chembechembe zote zinazomuingiza mwanadamu katika ubaya wa dhambi na mauti!

Na Padre Padre Joseph Peter Mosha. – Vatican.

Leo ni Dominika ya 34 ya Mwaka B wa Kanisa, Dominika ya mwisho katika Mwaka wa Kanisa ambapo tunapata fursa ya kumshangilia Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme. Liturujia ya Mwaka wa Kanisa imefumbatwa na utimilifu wa fumbo la Kristo ambaye ni tumilifu wa Ukombozi wetu wanadamu. Baada ya kusafiri pamoja kwa kipindi cha Mwaka mzima kuitafakari kazi hiyo ya ukombozi ya Kristo tunapata fursa ya kushangilia pamoja naye na kumpokea kama Mfalme, yaani mtawala wa maisha yetu. Ufalme wake ambao ameusimika duniani ni ufalme wa wote na kila mmoja anaalikwa kusafiri pamoja na Kristo ili kuusimika utawala wake katika maisha yake. Hapo ndipo Mungu anakuwa yote katika yote.

Masomo ya liturujia ya leo yanaufafanua ufalme wa Kristo. Somo la kwanza linausema ufalme wake kuwa “ni ufalme usioweza kuangamizwa”. Nabii Danieli anamwelezea Kristo kama Mwana wa Adamu ambaye atapewa mamlaka, utukufu na ufalme. Danieli anaota njozi hii wakati ambapo taifa la Israeli lilikuwa utumwani. Utawala wao ulikuwa umeangamizwa na kuwapelekea kuwa watumwa. Njozi yake hii kwa nafasi ya kwanza, ilionesha matumaini kuwa Mungu atawarudishia tena utawala wa kiserikali na utakuwa utawala ulio imara. Lakini wokovu huo unaufunua ufalme ulio na nguvu zaidi, ufalme wa Kristo ambao “watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie, mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa”.

Matarajio ya kibinadamu juu ya udumifu wa ufalme huu wa Kristo yanapingana na maana ya ndani ya udumifu huo. Kristo anatamka waziwazi katika Injili ya leo kuwa “ufalme wangu sio wa ulimwengu huu”. Katekesi ya Kristo kuhusiana na urefu na upana wa ufalme wake inatupatia mwanga. Yeye anatuambia kuwa: “Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli”. Moja kwa moja tuona dhumuni na utambulisho wa ufalme wake: ni kushuhudia ukweli. Kinyume na matarajio ya washitaki wake mbele ya Pilato anawaonesha kuwa Yeye haitaji utawala wa kisiasa au umaarufu wa kijamii bali yeye ni Kristo, yaani Masiha ikimaanisha mkombozi ambaye amekuja kuusimika ukweli ulimwenguni.

Safari nzima ya Ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme imejikita katika kuurejesha utawala wa Mungu kwa wanadamu. Mwanadamu alipoamua kuukataa uhuru wa kweli na kujivika uhuru bandia ambao ulimtoa mwenyezi Mungu ndipo alipojiingiza katika utumwa wa dhambi. Dhambi ndiyo chanzo cha utumwa wote ambao unamsibu mwanadamu. Matendo yote ya dhambi kama uasherati, uzinzi, wizi, rushwa, kupora haki za watu, magomvi na mapigano na mengine mengi ni matunda ya kuukataa ukweli. Ukweli huo ambao ndiyo utawala wa Kristo ndiyo kanuni ambayo inaratibisha na kuyafanya yote yawe katika uwiano. Kanuni hiyo ndiyo inayomsukuma mwanadamu kuwa na kiasi, uvumilivu, subira, upole, msamaha na katika ujumla wa yote upendo kwa wenzake. Kurasa za Injili Takatifu zina utajiri wa kutosha unaoufunua ukweli huo. Huo ni muhtasari wa maisha ya Kristo ambayo yameurudisha utawala wa ukweli ulimwenguni.

Utawala wa Mungu ulimwenguni unadhihirika katika utawala wa ukweli. Ukweli ndiyo unampatia mwanadamu uhuru wa kweli. Hamu ya Waisraeli walipokuwa utumwani Babeli ilikuwa ni kupata uhuru. Uhuru huo kama usingejengwa katika ukweli ungekuwa ni wa kupita. Mwanadamu anapokubali kuukumbatia ukweli haki utawala, amani hupata nafasi na jamii hutengeneza uwiano. Sisi sote tunaitwa kuwa sehemu ya utawala huu wa Kristo ambao kwao tumefanywa kuwa warithi, wahifadhi na wajenzi wake katika jamii ya mwanadamu. Huu ndiyo utume wetu wa kimisionari, utume wa kuwaeleza watu ukweli ili Kristo atawale milele. Tumefanywa kuwa raia na mabalozi wa ufalme wa Kristo. Udumifu wake unadhihirishwa na matendo yetu yanayoustawisha ukweli. Tuepuke kishawishi cha kuukwepa ukweli na kuupaka rangi nzuri uovu tukifikiri kuwa tutaugeuza kuwa ukweli. Tabia hiyo hutupatia uhuru bandia ambao humuingiza mwanadamu katika maangamizi makubwa zaidi.

Dunia na vyote vilivyomo vitapata amani na utulivu tunapotembea katika ukweli. Hii ni kwa sababu kazi yote ya uumbaji ni kazi ya Mungu na ni kwake Yeye peke yake ndipo tunapata maana, umuhimu na namna ya kuratibisha kazi hiyo. Mungu ni mkuu wa ulimwengu mzima. Somo la la pili linamuelezea Kristo kama mkuu wa Wafalme wa dunia. “Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho… aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja”. Ukuu wake huo unaonekana katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, amana ya mbinguni ambayo kwayo ametuachia ukumbusho wake na udumifu wake kati yetu siku zote. “Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake”. Tuijongeapo Sakramenti hiyo kuu tutambue akilini mwetu kile tunachoshirikishwa, yaani ukweli ulioletwa kwetu kwa njia ya Kristo, na hivyo kuwa mabalozi wa kuueneza ukweli huo katika maisha yetu ya kila siku.

Utawala wa Kristo ni utawala wa kimungu ambao unanuia kutupatia uzima wa milele, kutukomboa kutoka uovu, na kuungamamiza utawala wa dhambi. Ni utawala wa upendo unaweza kuustawisha wema kutoka katika ubaya. Ufalme ambao unaondoa chembechembe zote zinazomwingiza mwanadamu katika ubaya, chembechembe ambazo zinamuondoa mwanadamu kutoka katika ukweli. Ni ufalme ambao unaweza kuulainisha moyo mgumu na kuufanya kuwa laini ili kuruhusu kupenya kwa neno la Mungu. Ni ufalme unaoleta amani penye machafuko, unaowasha moto wa matumaini katika giza nene. Lakini ufalme huu wa neema ya Mungu kamwe haulazimishwi kwa mabavu bali unaheshimu uhuru wetu. Hivyo ni jukumu letu kuupokea au la.

Hivyo kila mmoja katika dhamiri yake anapaswa kujiuliza anapenda kuufuata utawala wa namna gani: ule wa Kristo unaotupeleka katika ukweli au utawala mwingine ambao daima unatuingiza katika maangamizi? Utawala wa Kristo hautuhakikishii mafanikio kadiri ya muono wa kidunia lakini utuhakikishia ile furaha na amani ambaye yeye tu ndiye anaweza kutupatia. Katika historia ya mwanadamu tumeona mifano ya watu mbalimbali katika zama tofauti ambao wamekuwa kielelezo kwetu katika jina la Kristo na katika ukweli na haki wametambua ulaghai wa utawala wa kiulimwengu hadi kufikia ujasiri wa kuyatoa maisha yao kwa ajili ya ukweli ambao ndiyo uthibitisho wa utawala wa Mungu. Tuombe neema ya Mungu katika adhimisho la Sherehe hii kusudi kwa mifano yao nasi tupate ujasiri wa kuustawisha milele utawala wa Kristo.

Sherehe Kristo Mfalme
21 November 2018, 15:41