Tafakari ya Neno la Mungu: Iweni wakarimu kwa jirani zenu ili kuonja wema wa Mungu!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.
Biblia inaweka wazi kuwa siyo juhudi binafsi ya mwanadamu inayompatia wokovu ila wokovu wake hutokana na tendo la upendo la ukombozi toka kwa Mungu. Tukiimarishwa na upendo huo, sisi tunaweza kupenda na kupendana. Tuliona hili jumapili iliyopita. Tunaye Mungu ambaye ni pendo, ni upendo. Maisha yetu hayana budi kuwa ni shukrani kubwa kwa Mungu ambaye ni upendo kama kweli tuna amini na kusadiki kweli kwamba Mungu ni mkuu.
Katika somo la kwanza twaona mwanamke mjane anatoa chakula chake cha mwisho na anamwambia wazi wazi Eliya kiasi na kitu alichokuwa nacho bila kuficha na anatoa chote alichokuwa nacho na anampatia yeye kwanza ale na baadaye yeye na mtoto wake wanakula. Tena cha kushangaza huyu ni mpagani na hamjui au haamini katika Mungu wa Eliya.
Katika somo la pili tunaona ujane wa Kanisa pale Yesu alipojitoa sadaka ili kufuta dhambi zetu. Yeye aliye Mwana pekee anajitoa sadaka. Katika Kol. 1:19 - tunasoma hivi; kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae na katika Kol. 2:9 neno la Mungu linasema hivi; maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu kwa jinsi ya mwili. Katika somo la Injili, yule mjane anatoa senti yake ya mwisho.
Kwa kifupi tunaona kuwa wahusika wote katika masomo yetu ya leo wanaweka matumaini yao yote kwa Mungu. Wanaongozwa na roho wa Mungu na wanatoa bila kubakiza cho chote. Katika somo la I na III wanamtumainia Mungu ili wasife na njaa na yule wa kwanza anapata chakula na hafi na njaa na yule wa injili habari yake na uhodari wake unaandikwa katika maandiko matakatifu. Katika somo la II Yesu anamtumainia Mungu amwinue toka kwa wafu na anapata thawabu ya Mungu.
Matokeo yake ni kuwa wote wanabarikiwa: Unga na mafuta hayaishi; Yesu anatukuzwa na Mungu Baba. Ebr. 1:3-4 tunasoma neno hili, yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu, amefanyika bora kupita malaika kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao Tendo lake yule mjane maskini linatoa ushuhuda unaobaki milele.
Ndugu zangu, sadaka ya Yesu ni sadaka ya Agano Jipya na mwongozo kwa sadaka zote na namna yetu ya kutoa sadaka. Tunataka kutoa sadaka zetu kwa Mungu na kwa wenzetu basi tujifunze kutoa na kujitoa kama alivyofanya Yesu. Hicho ndicho kipimo cha utoaji. Ni mfano hai na mtakatifu. Sote twajua kuwa atakapokuja mara ya pili haji kwa ajili ya ukombozi toka dhambi zetu bali kuwahukumu wazima na wafu. Je akija leo atatukuta tu wazima au wafu? Atakuja kuwakusanya wale waliodumu katika imani kwa Mungu kwa ajili ya wale wanaomngoja Bwana. Tukumbuke maneno ya Mungu kwa Abrahamu; mimi ni Mungu wa wazima na si Mungu wa wafu. Kadiri ya maelezo hayo wanaoishi ni wale wanaoangaza duniani, ni wale wanaong’aa mapendo kwa Mungu na kwa ndugu. Hawa ndo wanaohesabika kuwa na uzima.
Mfano wa sadaka hai kwa wakati wetu huu ni sadaka ya Mt. Marximiliani Maria Kolbe mfungwa wa kinazi. Huyu alifungwa gerezani kwa sababu aliongea vibaya dhidi ya utawala wa Hitler. Akafungwa gerezani. Siku moja mfungwa mmoja kutoka gereza lao alitoroka. Mkuu wa gereza akatoa amri wafungwa kumi wauawe kwa kunyimwa chakula. Kati yao alikuwepo kijana mdogo ambaye familia yake ilimtegemea. Padre Kolbe aliamua kuchukua nafasi yake akiamini kwamba siku moja uhuru utapatikana na pengine yule kijana atapata nafasi ya kuachwa huru apate nafasi ya kuhudumia familia yake changa.
Katika orodha hiyo ya kifo wa mwisho kuuawa alikuwa Padre Kolbe na kwa vile alikawia kufa alidungwa sindano ya sumu ili afe. Katika chumba chake walikuta picha ya Yesu ukutani aliyochora kwa kucha za vidogo vyake. Mpake leo haieleweki aliwezaje kufanya hivyo kwenye ukuta mgumu wa mawe. Imani ya ajabu kweli. Hii ndiyo sadaka hai na takatifu. Mtume Paulo katika Rum. 12,1 anasema – basi ndugu, nawasisitiza kwa ajili ya huruma ya Mungu, toeni miili yenu kuwa sadaka iliyo hai, takatifu na yenye kumpendeza Mungu. Hiyo ndiyo ibada iwafaayo. Na Richard Braustein anasema, unaweza kutoa bila upendo, lakini huwezi kupenda bila kutoa kwa upendo.
Hatuna budi kufanya bidii kubwa ili kuupata uzima wa milele. Mt. Gaspari anasema kwa Mungu ni lazima kufanya mengi, vizuri na haraka. Katika ufu. 3:15-16 tunasoma neno hili la Mungu - nayajua matendo yako, ya kuwa huu baridi wala hu moto, ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi kwa sababu hu uvuguvugu wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Ndugu zangu, taifa la Mungu, kwa Mungu tusifanye kidogo na pengine kwa udanganyifu au tusitoe tu kidogo tena kwa kusita na wasiwasi, tena kwa mashaka na manung’uniko. Kuna watu wachoyo hata kumtolea Mungu wanasita. Tunapotoa kwa Mungu tusipime au tusitoe kwa malalamiko. Mara nyingi sisi tunamtolea Mungu kile kilichobaki. Tunamtolea Mungu mabaki. Hatari kweli.
Tutafakarishwe na mfano huu. Maskini mmoja na fukara anasikia kuwa tajiri atapita katika mtaa wao na yeye anajipanga kumwomba. Yule maskini alikuwa ameokoteza mchele kidogo kwa kuombaomba. Kumbe yule tajiri alipomkaribia akamwomba yeye ampatie chochote. Yule maskini akakasirika sana. Sasa huyu tajiri ananiomba mimi nimpatie cho chote hali yeye ni tajiri? Basi kwa manunguniko makubwa akachukua punje tano za mchele akampatia. Yule tajiri akamshukuru akaenda zake.
Yule maskini alipofika nyumbani akaanza kuuchambua mchele wake ili aanze kupika. Alipochukua punje ya kwanza kumbe akaona dhahabu, akachukua ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano na ikawa mwisho. Yeye akaanza kuwaza kumbe zile punje tano nilizotoa zimekuwa dhahabu. Aliposhika ya sita ikabaki mchele tu. Akawaza moyoni mwake laiti ningempatia mchele wote. Uchoyo wake ukamfanya akose dhahabu na utajiri. Kwanza alitoa akinung’unika na akatoa kidogo.
Tunajiuliza tena nini leo kama tumeelewa vizuri neno la Mungu? Je wewe una kitu gani zaidi cha kumpatia Mungu? Familia yako? Jirani yako? Jumuiya yako? Kanisa lako? Jamii yako? Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anatukumbusha kuwa huwezi kupata bila kutoa. Na tuone raha katika kutoa kuliko kupokea.
Tumsifu Yesu Kristo.