Tafakari ya Neno la Mungu: Hekalu jipya na sadaka mpya!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.
Katika milima ya Andes zinapopakana nchi za Argentina na Chile ipo sanamu kubwa ya Yesu Kristo inayoshikilia Msalaba. Wakati fulani nchi hizi mbili zilitaka kuingia katika hatari ya vita. Sababu ya ugomvi ni kipande cha ardhi ambayo kila nchi ilidai kuwa ni mali yake. Kila nchi ikajianda kwa vita. Ikatokea kuwa wakati wa jumapili moja ya Pasaka Maaskofu wa nchi zote mbili wakaanza kampeni dhidi ya vita na kutaka amani. Wakazunguka katika nchi zao wakitaka amani kwa jina la Yesu Kristo. Watu hawakutaka vita na hivyo wakawafanya viongozi wa nchi hizi mbili kutaka amani kati yao. Wito ukasikika.
Silaha zote nzito za kivita zikayeyushwa katika matanuru ya moto na hivyo kutengenezwa sanamu kubwa ya Kristo Yesu. Sanamu hii imesimikwa katika milima ya Andes zinapopakana nchi hizi mbili na chini ya sanamu hii yameandikwa maneno haya; ‘milima hii itaanguka na kusambaa kuwa majivu lakini watu wa Argentina na Chile hawatasahau kamwe maagano yao makuu yaliyofanyika chini au katika miguu ya sanamu hii ya Yesu Kristo.’ Agano hili la amani likawa mwanzo mpya, sadaka mpya, hekalu jipya la maisha ya amani ya watu wale.
Ndugu zangu, Kitabu cha Danieli katika Agno la Kale ni mojawapo ya vitabu vinavyoongea kuhusu ufufuko wa wafu. Danieli anaandika, waongoza wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele. Baadaye katika Agano Jipya, ikawa wazi kuwa Yesu ndiye anayeondoa dhambi za dunia na kwamba wakati wa mavuno tuna uhakika wa kuvuna ikiwa talipanda pamoja naye. Tumaini ni fadhila kuu ya Kibiblia. Ni kutumaini kwa matarajio ujio wa ufalme wa Mungu, ufalme wa haki na amani kati ya watu wake. Yule anayetumainia atapata amani na haki hiyo. Kwanini tumaini ni fadhila yenye nguvu kiasi hicho? Tumaini ni tarajio la furaha na katika Biblia ni tarajio la ujenzi wa ufalme wa Mungu, katika amani na haki. Anayetumaini anatarajia nafasi katika huo ufalme. Ni nini msingi wa tumaini hilo? Ni imani thabiti kwa mkono wa nguvu wa Mungu.
Historia ya wokovu wetu inadhihirisha hilo. Mkono wa Mungu, wenye nguvu, wenye dhihirisho la upendo ni wokovu. Matokeo yake ni furaha. Kwa sababu Mungu ameonesha tayari kwa watu wake. Mkono wa Mungu tayari umefanya kazi kwa watu wake. Angalia historia ya ukombozi wetu, kwa upendo kabisa ametukomboa. Kwa nini tusifurahi? Hivyo katika Biblia twaona mitazamo miwili iliyo wazi; tunatazama nyuma kiimani na huku tukiwa na matumaini kwa siku zijazo. Waisraeli waliweza kusherehekea jambo hili tangu walipokombolewa; manabii wakawakumbusha juu ya imani na matumaini yajayo.
Hali kadhalika sisi wakristo tunasherehekea Fumbo la Pasaka la Kristo ambapo Mungu ametukomboa na ametuita kwenye maisha ya utakatifu. Kwa sababu hiyo basi tuna uhakika wa kuokoka toka hasira ya Mungu kama tukibaki waaminifu. Hayo aliyofanya Mungu kwa upendo yatuhakikishia matumaini yetu katika siku zijazo. Ndiyo maana tupo hapa tunasherehekea upendo wa Mungu kwetu kwa matumaini.
Masomo yetu ya leo yanaongea wazi kuhusu jambo hili. Somo la kwanza na la pili yazungumzia matokeo ya mambo yajayo na tumaini hilo lijalo. Tutaokoka ikiwa tutaishi ile imani, ule upendo aliotushirikisha Mungu. Kitabu cha Danieli kiliandikwa wakati wa utawala wa Assyria (Ashuru) na mfalme mpagani alilazimisha ibada za miungu wake katika Israeli. Watu walikata tamaa. Walipoteza matumaini. Tukumbuke kuwa wakati huu hekalu lilishabomolewa na hivi kadiri ya imani ya Waisraeli walipoteza matumaini. Lakini Danieli anakumbusha utukufu wa Mungu uliokuwa kati yao. Na hii ndiyo dhamira kuu ya leo – (sadaka mpya) wataishi milele na watang’aa kama nyota. Hivyo wanakumbushwa historia yao na kuweka matumaini yao kwa maisha yajayo.
Katika somo la Injili, tunasikia habari juu ya ujio wa mtu ambaye atauweka ufalme wa Mungu. Ndicho tunachokumbushwa leo na kanisa. Fundisho hili ni zaidi ya kukumbuka. Latuita kuliishi kama fumbo ili jambo hilo lionekane kwa watu. Yesu tayari alishakuja ulimwenguni kwa msamaha wa dhambi. Hatuna budi kujiuliza; Je, atakapokuja mara ya pili atatukuta katika hali gani? Hatuna budi kushi kama watu wanaoamini katika Yesu aliyetufundisha na kuushuhudia uwepo wa ufalme wa Mungu kati yetu na siyo watu wanaoigiza au wanaokariri tu alichotufundisha Yesu.
Tukumbuke kuwa katika dini yo yote ile tendo la sadaka huonekana kutambulisha imani hiyo kuliko kitu kingine cho chote kile. Kama wakristo leo, tunatoa sadaka gani? Hakika sadaka ya Kristo yatangulia. Lakini tunaiishi namna gani? Katika 1 Kor. 3:16 tunaangalishwa kuhusu jambo hili; je hamjui ya kuwa ninyi ni hekalu la Mungu, na Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Na katika 2Kor. 6:16 tunasoma kuwa; tena hekalu la Mungu linapatanaje na sanamu za miungu wa uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Ndivyo alivyosema Mungu, nataka kukaa miongoni mwao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa taifa langu. Jenerali William Booth aliandika wakati mmoja kuwa janga kubwa la karne ya ishirini ni kuwa na; Dini bila Roho Mtakatifu; Ukristo bila Kristo; Msamaha bila mwanzo mpya; Maadili bila Mungu; Mbingu bila jehanamu. Kwa kifupi neno la Mungu dominika hii latudai upendo na matumaini ili kujenga hekalu jipya na kuwa sadaka mpya.
Padre J. Healey, M.M katika kitabu chake “Hadithi za Kiafrika” anaelezea tendo la upendo lilofanywa na wasichana wa Shule ya Sekondari Muramba katika mkoa wa Gisenyi, Rwanda kama tendo la upendo na matumaini. Namna mpya ya kuishi sadaka ya maisha yetu. Hii ndiyo sadaka mpya na hekalu jipya. Ilitokea kuwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Wahutu na Watutsi, kikundi cha wanaume wenye silaha, kilivunja na kuingia katika shule yao na kuwalazimisha wajipange kadiri ya makabila yao. Wao walikuwa ni jumuiya moja na walipendana sana. Na waliitambua nia mbaya ya wauaji wale. Wauaji walikuwa na nia ya kuwaangamiza kikabila. Hawakuitii amri ile. Bila huruma wale wauaji wakawafyatulia risasi na kuua 17 na kujeruhi wengine 14. Kati yao alifariki pia sista Margarita Bosmans, aliyekuwa mkurugenzi wa shule ya jirani aliyejaribu kuwazuia wauaji. Hawa wasichana waliishi upendo na matumaini na wakawaaibisha wauaji wao.
Mwandishi wa Waraka kwa Tito 2:11-13 anaandika hivi; maana neema ya Mungu imetokea kwa kuwaokoa watu wote. Nayo inatuongoza kuzuia yasiyo ya Mungu, na kupinga tamaa za kidunia, tupate kuishi duniani hapa kwa kiasi, kwa haki na kwa uchaji wa Mungu, tukingoja heri tunayoitazamia na ufunuo wa utukufu wa Mungu mkuu na wa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Huu ni mwaliko wa kuishi maisha mapya ya upendo na matumaini. Hatuna budi kuishi hiyo neema ya Mungu iliyopo kati yetu. Tumsifu Yesu Kristo,