Kristo Yesu ni ufunuo wa ufalme wa ukweli, haki, uzima, utakatifu, upendo na amani!
Na Padre William Bahitwa - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo Kanisa linaadhimisha sherehe ya Bwana wetu Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu. Ni dominika ya mwisho ya mwaka wa kiliturujia wa Kanisa ambapo tunaukiri na kuutukuza ufalme wa Kristo na kuona kilele cha maadhimisho yote ya Kanisa kuwa ni kuingia katika ufalme huo wa Kristo. Ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa haki na amani, ufalme wa mapendo na ufalme ambao Mungu anatawala katika mioyo ya watu wake.
Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Dan. 7:13-14) Somo la kwanza ni maono ya Nabii Danieli juu ya ujio wa mtawala atakayepewa mamlaka, utukufu na ufalme na ambaye watu wa kabila zote na taifa na lugha watamtumikia. Atakuwa na mamlaka ya milele ambayo haitapita kamwe. Maono haya ambayo kwa kweli ni maono ya kimungu na ni ufunuo yalimuijia Nabii Danieli katika njozi ya usiku ambapo kwa kawaida mtu huwa amejipumzisha na kazi na mambo yote ya kutwa nzima. Ndiyo kutuambia kuwa pale mtu anapoelekeza fikra zake kwa Mungu na kuyaondoa makandokando yake, anaweza kuyapata mangàmuzi ya kimungu na kufikia muunganiko naye.
Maono haya ya huyu mtawala aliye mfano wa mwanadamu yanakuja baada ya maono ya watawala wanne waliokuwa ni mfano wa wanyama: mmoja mfano wa Simba, mwingine wa Dubu, mwingine wa Chui na wa nne anayetajwa kama mnyama wa kutisha. Ujio wa mtawala aliye mfano wa mwanadamu unakuwa ni ujio unaoondoa enzi ya hao watawala wanne. Unakuwa ni ujio unaoondoa utawala wa unyama na kuanzisha utawala wa utu na heshima ya mwanadamu. Lakini ni nani huyu mtawala aliye mfano wa mwanadamu? Ni Masiya, Yesu Kristo. Na katika Injili ya Yohane 5:27 Yesu mwenyewe anasema “(baba) akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu”.
Somo la pili (Ufu. 1:5-8) Somo letu la pili linalenga kukazia kuhusu ujio wa pili wa Kristo. Kwanza linaanza kueleza Kristo ni nani, na hapo linataja sifa zake kuwa ni shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa na ni mkuu wa wafalme wa dunia. Somo linaeleza pia kile alichokifanya Yesu: ametuosha dhambi zetu katika damu yake na kutufanya kuwa makuhani kwa Mungu. Na ni kweli tunakuwa makuhani kwa sababu kila anayebatizwa kwa jina lake anashirikishwa ukuhani wake, unabii wake na ufalme wake. Ndiye atakayekuja mara ya pili kwa ujio wa hukumu kwa maana anayo mamlaka ya kuhukumu.
Injili (Yoh. 18:33b-37) Injili ya leo Yesu yuko mbele ya Pilato ili kusomewa mashtaka yake na kuhukumiwa. Pilato anaanza kwa kumuuliza “Je, wewe ni mfalme wa wayahudi?” Kwa kuyaangalia mazingira ya wakati ule ambapo wayahudi walikuwa ni koloni la warumi na walitarajia sana ujio wa mfalme wao ili kuwaokoa kutoka utumwa huo wa kisiasa, Pilato alitaka kujua kama Yesu ndiye huyo mfalme wayahudi waliokuwa wanamgojea. Swali hili pia ndani yake ni swali la kebehi: kwamba “kama kweli wewe ni mfalme wa wayahudi, iweje watu wako, wayahudi kama wewe ndio wakulete kwangu nikuhukumu”? Na tena ni sawa na kumwambia “ni mfalme gani wewe unayeonekana katika hali hii, hali ya unyonge na kutokuwa na nguvu iliyozoeleka ya kifalme?”
Katika majibu yake, Yesu hakanushi. Hasemi “mimi sio mfalme”. Anaanza kueleza kuwa ufalme wake sio wa ulimwengu huu na sio wa namna za ulimwengu huu kama vile kuwa na majeshi ya kivita. Ufalme wake ni ule unaotoa ushuhuda kwa ukweli. Anasema “nilikuja ulimwenguni ili niishuhudie kweli… nimezalwa kwa ajili hiyo na kwa ajili hiyo nilikuja ulimwenguni”. Ufalme wake ni ule ambao ukweli wa kimungu unatawala katika mioyo na maisha ya watu na kila aliye wa ukweli anaisikia sauti yake yaani kila anayekubali kuongozwa na ukweli wa kimungu katika maisha yake, anayeishi kwa kushuhudia ukweli ni mmoja wa wale walio ndani ya ufalme wake Kristo.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, leo Kanisa linaweka mbele yetu ukweli kuwa Yesu Kristo ndiye Mfalme wa ulimwengu mzima. Bwana wetu Yesu Kristo, Neno wa Mungu ambaye kwa njia yake vitu vyote vilivyopo ulimwenguni vilipata kuwapo na tena kwa njia yake ulimwengu wote ukakombolewa kutoka dhambi na mauti na kuuingiza katika ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa haki na amani, ufalme wa mapendo, ndiye yeye anayeendelea kuuongoza ulimwengu kufikia lengo la kuumbwa kwake. Yeye ndiye kweli aliye alfa na omega, yaani mwanzo na mwisho.
Kumbe, katika nafasi ya kwanza kanisa linataka kwa njia ya sherehe hii tuuone ukweli huo kuwa licha ya kuwa na viongozi katika jamii zetu na kwa ngazi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, sisi na viongozi wetu wote hao tuko chini ya utawala wa Kristo (tumeumbwa kwa njia yake, tumekombolewa naye na tunaongozwa naye). Sisi sote tunaalikwa kuingia na kuwa raia katika ufalme huo, kama Injili ya leo inavyotufundisha kwa kuisikia sauti yake na kuwa miongoni wa wale wanaoongozwa na ukweli, dhana ambayo kibiblia imeunganishwa na Mungu mwenyewe. Kwa namna ya pekee kabisa, sherehe hii inarudia mwaliko usiokoma wa kuutaka ulimwengu kuwa na hofu ya Mungu. Kujua kuwa ulimwengu haujaachwa tu ujiendeshe peke yake au kuamuliwa hatima yake kadiri ya matakwa yetu pekee. Ulimwengu unaye mfalme wake na mfalme huyo ni Kristo.
Sherehe hii pia inawekwa mwishoni mwa mwaka kutupa dhana ya kieskatolojia, mambo ya mwisho wa nyakati. Kwamba ufalme huu wa Kristo ni ufalme utakaodhihirika kikamilifu katika mwisho wa nyakati, Kristo atakapokuja mara ya pili kuuhukumu ulimwengu kama mfalme wake hasa. Kristo mfalme wa ulimwengu awe mtawala wa nafsi zetu aziongoze katika ukweli halisi na kuzifikisha katika makao ya Baba wa milele.