Bikira Maria: Injili ya uhai na matumaini kwa ujio wa Masiha!
Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.
Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji. Bikira Maria ni sanduku la Agano Jipya na la Milele. Ni Mama wa Mkombozi anayekwenda kumtembelea Elizabeth. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao zawadi ya maisha wanakutana. Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeth ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli. Bikira Maria anakwenda kwa haraka kumsalimia Elizabeth, kielelezo makini cha huduma ya upendo kwa jirani na mfano wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo uliogubikwa na ubinafsi na uchoyo. Yohane Mbatizaji anaruka kwa shangwe tumboni mwa mama yake Elizabeth, ushuhuda makini wa kufunguliwa kwa ukurasa mpya naye ndiye atakayekuwa Nabii na daraja kati ya Agano la Kale na Agano Jipya.
Antifona ya mwanzo ya Dominika ya nne ya Majilio inalifafanua fumbo zima la Umwilisho ambalo ni utimilifu wa Ukombozi wa mwanadamu. “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa mwokozi”. Dominika hii ambayo inatutafakarisha tendo hilo adhimu katika imani yetu inanuia kutukumbusha ujio wa Kristo hapa duniani na kuufanya tena hai uwepo huo na hivyo kuingia katika sherehe za Noeli tukiwa na mioyo iliyo tayari kumpokea Mwokozi. Mkombozi wa wanadamu ni Kristo ambaye ni nafsi ya pili ya Mungu. Yeye anashuka kutoka juu mbinguni na kutujia sisi wanadamu. Uwepo wake unadhihirika kwa kujimithilisha na sisi. Hivyo ni zawadi itokayo juu mbinguni inayoshuka chini mithili ya mvua na kuidhihirisha kazi yake ya ukombozi katikati ya jamii.
Katika Dominika hii mhusika mkuu anayeonekana sana ni Mama yetu Bikira Maria. Imani yake, “ndiyo” yake katika wito wa Mungu na umama wake unao nafasi muhimu katika ukombozi wetu sisi wanadamu. Leo hii tunaletewa mbele yetu tukio la Mama Bikira Maria kumtembelea jamaa yake Elizabeti katika nchi ya milimani katika mji mmoja wa Yuda. Yatokanayo na kutaniko lao hilo yanaifafanua vema nafasi ya Bikira Maria na namna alivyotimiza vema wajibu wake hadi kutuletea mkombozi.
Kitu cha kwanza ni imani yake thabiti kwa Mungu. Wakati wa kutaniko lake na Malaika Gabrieli alielezwa juu ya mkono wa Mungu ulivyomtendea makuu jamaa yake Elizabeti (Rejea Lk 1:36) na katika imani hiyo alikwenda mara moja kumsalimu, kumjulia hali na bila shaka kumsaidia kwani umri wake ulikuwa umeshasogea sana. Injili hiyo ya Luka inaonesha kuwa Elizabeti alijaliwa ujauzito katika umri wa uzee. Kibinadamu isingeeleweka lakini kutokana na imani thabiti ya Mama Bikira Maria kwa neno la Mungu, alilipokea neno la Malaika na kwenda kwa haraka kumtembelea binamu yake.
Imani thabiti ndiyo ilimfanya Mama Maria kuitii sauti ya Mungu na kwa utii wake ametuzalia mkombozi wa ulimwengu. Ndiyo yake hiyo iliyochagizwa na imani yake ni udhihirisho wa muunganiko wake na Mungu. Elizabeti anashuhudia hilo akisema: “Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana”. “Ndiyo” ya Maria inamwezesha kufanya mapinduzi dhidi ya fikra za kibinadamu zinazoathiriwa na mazoea na upepo wa kidunia. Athari hizi hutoa nafasi finyu kwa utekelezaji wa mipango ya Mungu ndani mwetu.
Pengine tunaweza kuwa tunaisherehekea Noeli kila mwaka, lakini bado tunakosa muunganiko wa ndani na Mungu na kusema “ndiyo” kwa neno lake. Pengine huwa tunalifurahia kulisikia lakini madai yake yanakuwa machungu. Yote haya huchagizwa na namna tunavyoipokea imani yetu. Mmoja anapobaki na imani ya juu juu tu ni aghalabu kuutambua na kuuona mpango wa Mungu. Ili kufanikiwa kutambua na kuuona mpango wa Mungu na kusema “ndiyo” yenye tija kwa ukombozi wetu tunahitajika kuwa mithili ya Mama Bikira Maria katika kuunganika na Mungu miyoni mwetu.
Bikira Maria alipokutana na Elizabeti yapo matukio mawili muhimu yaliyotokea na yanayohitaji Tafakari yetu. Kwanza ni furaha ya mtoto aliyekuwa tumboni mwa Elizabeti na pili ni kiri imani ya Elizabeti iliyochanganyika na furaha kubwa. Tunaweza kulifananisha tukio hili la mtoto anayefurahi tumboni mwa Elizabeti na furaha aliyokuwa nayo Mfalme Daudi mbele ya Sanduku la Agano (Rejea 2Sam 6:1-11), wakati likipelekwa Yerusalemu. Hivyo, furaha hii inamtambulisha Mama yetu Bikira Maria kuwa Sanduku jipya la Agano ambalo ndani mwake limembeba mkombozi wa ulimwengu.
Ndiyo maana Elizabeti anamtaja Bikira Maria kama mbarikiwa: “umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa”. Elizabeti kama anavyoelezewa na Injili anakiri imani hiyo baada ya kujazwa na Roho Mtakatifu, anatambua mara moja makuu ambayo Mungu ameyatenda kwa binamu yake Bikira Maria. Yeye anauona mkono wa Mungu na ukuu wa Yeye ambaye Maria amembeba tumboni kwake: “Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anilijie mimi?” Kwa namna hii anaukiri umama wa Bikira Maria kama Mama wa Mungu.
Kwa imani yake thabiti, “ndiyo” yake na umama wake Bikira Maria anakuwa ni chombo kitakatifu cha kuuletea ukombozi ulimwengu. Utii wake unamuunganisha tena Mungu na binadamu. Katika ujumla wake Bikira Maria anafanikiwa katika hili kwa sababu ya kujivika udogo na unyenyekevu. Hapa tunapaswa kuing’amua fadhila ya unyenyekevu ambayo ni muhimu katika kukua kwa paji la imani na hivyo kutufanya kuunganika kweli na Mungu katika mipango yake kwetu. Mara nyingi mwanadamu uhadaika na kiburi na majivuno yake iwe ni nguvu za kimadaraka, kiakili, kiuchumi nk na matokeo yake hutoa nafasi finyu kwa mapenzi ya Mungu.
Mungu hutenda vema na yule anayeutambua ukuu wake na umuhimu wake na hivyo kumpatia nafasi stahiki katika maisha yake. Nabii Mika anauonesha utendaji huo wa Mungu katika maaguzi yake tunayoyaona katika somo la kwanza. Masiha ambaye alitegemewa katika jamii ya kiyahudi hatoki katika miji mikubwa kama Yerusalemu bali kutoka Bethlehemu: “Bali wewe Bethlem Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli”. Uaguzi huu unajidhihirisha kwa namna mbili: kwanza ni hadhi ya mji wa Bethlehemu ukilinganisha na Yerusalemu lakini pia hadhi ya Bikira Maria ukilinganisha asili yake na wakuu wa jamii ya Israeli wakati wake. Kutoka kwake Bikira Maria, binti mdogo asiyejulikana kabisa Mungu anatengeneza ukuu wake. Ni udhihirisho wa uwezo mkuu wa Mungu dhidi ya fikra, matamanio na majigambo ya kibinadamu.
Mwandishi wa waraka kwa Waebrania anakazia umuhimu wa kuungana na Mungu katika muungano wa ndani ili kumtolea sadaka impendezayo. Fumbo tunalojiandaa kuliadhimisha siku za karibuni, yaani fumbo la umwilisho linauthibitisha muunganiko huo. Sadaka za zamani zilikuwa ni sadaka za mafahali na mbuzi lakini sadaka ya Kristo ni mwili wake. Sadaka yake inapata hadhi ya juu kwani tofauti na hizi za zamani ni yeye mwenyewe anajitoa nafsi yake kwa Mungu. Sadaka za zamani zilikosa muunganiko wa moja kwa moja na atoaye sadaka hivyo kulikuwa na hatari ya kujitoa juu juu tu bila kuguswa ndani. Lakini hii ya kujitoa nafsi inamfanya mmoja kuunganikwa kweli kweli na Kristo.
Huu ni mfano wa kujisadaka, kujishusha na kutotaka kuonekana bali Mungu aonekane na kutukuzwa yeye. Sadaka hii imeanza kuoneshwa kwa mfano wa utii wa Maria kwa kujitoa nafsi yake kwa ajili ya kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Kwa kujitoa kwake huko Kristo ameuchukua ubinadamu na hivyo kutupatia mwanzo mpya kwa Yeye kuwa kielelezo kwetu cha namna ya kujiachilia wazimawazima kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Tukiwa tumebakiwa na siku chache kuelekea maadhimisho ya Noeli tunapata wajibu wa kujikumbusha hadhi tuliyopokea kwa sababu ya fumbo hilo la umwilisho. Tumefanywa kuwa wana wa Mungu katika Mwana. Hadhi hiyo inawezeshwa na tabia tunazoziona kutoka kwa mama yetu Bikira Maria yaani imani, utii na unyenyekevu wake. Kutokana na tabia hizo ameweza kweli kumtolea Mungu sadaka ya mwili wake.
Kristo Yesu, ameithibitisha sadaka hiyo kwa Fumbo la Pasaka na kwa njia yake ametuwezesha mimi na wewe kuweza kushiriki ukuu wa Mungu. Tujifunze kwa mama yetu Bikira Maria kusudi tumpokee Kristo kweli na kwa kumpatia nafasi tena azaliwe ndani mwetu na hivyo tuwezeshwe kujitoa nafsi zetu na kuitika kila siku tukisema: “Tazama, nimekuja… Niyafanye mapenzi yako, Ee Mungu Wangu”. Katika hili tutadhihirisha kweli kufunuka kwa nchi na Mwokozi atadhihirishwa kwa watu wote.