Tafuta

Sherehe ya Noeli: Ujumbe wa Mtoto Yesu Sherehe ya Noeli: Ujumbe wa Mtoto Yesu 

Sherehe ya Noeli 2018: Ujumbe mzito kutoka kwa Mtoto Yesu!

Yaani mtoto huyu amechukua kila kitu cha binadamu. Ni dhaifu, anatetemeka baridi ovyo-ovyo na kulia asipofunikwa vizuri nguo na kushikwa na mama yake. Anaweza kufa wakati wowote ule kama tunavyokufa binadamu wote. Hapo ujumbe anaotaka kutuambia ni kwamba, hali ya Mwenyezi Mungu asiye kufa, imeungana kwa upendo wa ajabu na hali dhaifu ya binadamu anayekufa.

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Seoul-Korea ya Kusini.

Leo kila mtu amejipanga kivyake-vyake kusherehekea sikukuu ya Noeli. Kama wewe huna mkakati wowote ule, basi vuta taswira ifuatayo. Pata picha unaingia kanisani. Unaona nyuso za waumini wenzako zilivyojaa furaha. Waangalie pia jinsi walivyotoka na viwalo vya sikukuu. Unajua kwa vyovyote hata majumbani kwao wamejipanga sawasawa kwa ulaji na vinywaji. Wengine pengine wameyaacha maboksi ya  zawadi za Noeli walizopata ili zifunguliewe ile siku ya “Boxing Day”.  Humo kanisani unaona pango la mtoto Yesu pamoja na kanisa vimepambwa vizuri. Unawaona wanakwaya na vyombo vyao vya muziki wanajiweka sawasawa.

Ama kweli hali ya hewa ni ya sikukuu ya Noeli! Misa inapoanza unawaona ministranti wamevaa vizuri wanaingia kanisani kwa ibada wakifuatiwa na Padre mwongoza ibada. Wakati wa Injili umejipanga kusikia Injili ya kuzaliwa kwa mtoto Yesu Bethlehemu pangoni ikiwa ni pamoja na ujio wa wachungaji wanaofika kumwona mtoto na wazazi wake Yosefu na Maria. Kumbe, kinyume chake unasikia fasuli ya Injili iliyoshonana Taalimungu ngumu kuieleweka. Injili inatuambia eti kuwa mtoto aliyezaliwa  amebeba ujumbe mzito. Kwa kuwaibia ibia tu mambo yanajieleza yenyewe pale utakapoina hali ya mtoto ilivyo.

Yaani mtoto huyu amechukua kila kitu cha binadamu. Ni  dhaifu, anatetemeka baridi ovyo-ovyo na kulia asipofunikwa vizuri nguo na kushikwa na mama yake. Anaweza kufa wakati wowote ule kama tunavyokufa binadamu wote. Hapo ujumbe anaotaka kutuambia ni kwamba, hali ya Mwenyezi Mungu asiye kufa, imeungana kwa upendo wa ajabu na hali dhaifu ya binadamu anayekufa. Hivi piga ua, hata kama ukijibaraguza na kukataa kuyakubali mahusiano hayo naye,  kwa upande wa Mungu imetoka hiyo. Ikirudi pancha! Huo ndiyo ujumbe wenyewe wa Noeli.

Mwinjili Yohane anatuelezea chanzo cha muungano wa upendo huo kati ya Mungu na ubinadamu. Katika kutusimulia chanzo hicho tunakumbana na jina jipya la Yesu. Sisi tumezoea kumwita Yesu kwa majina yanayojulikana kama vile: Bwana, Kristu, Mkombozi, Masiha, Mwana wa Mungu, Emmanueli (Mungu nasi) nk. Kumbe hapa anaitwa Neno, kama tunavyosoma: “Hapo mwanzo kulikuwa Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyu mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Jina hili Neno unalikuta katika maandishi ya Yohane peke yake. Kwanza katika  barua yake ya kwanza; halafu mara moja katika Ufuanuo wa Yohane na mwisho katika Injili ya leo.

Kwa Kilatini Neno ni verbum na kwa  Kigiriki ni logos. Kwa kawaida tunatumia maneno kwa mawasiliano. Kwa njia ya neno tunashirikishana taarifa ikiwa kama alama ya kujali mwingine. Unajisikia vizuri sana endapo mtu wa pekee kwako anataka kukuambia Neno. Mathalani, msichana aliyemzimikia msanii fulani kiasi hata cha kupamba kuta za chumba chake kwa picha za huyo msanii. Ikitokea kwa bahati na kwa wakati asiotegemea anasikia simu inaita. Anapoisikiliza anagundua kuwa ni sauti ya huyo msanii anayemwalika wakutane faraghani amwambie neno. Hapo binti huyo atasisimka na kujiuliza kama ni kweli au anaota ndoto za mchana! Makubwa, madogo yana nafuu yake!

Kumbe, leo Mungu mwenyewe amekubali kuzaliwa na kuwa kama mtoto mchanga, dhaifu, mnyonge, mpole na mnyenyekevu. Mtoto huyu asiposhikwa na kufunikwa vizuri nguo, anatetemeka baridi na kulia. Amezaliwa kwa ajili yako. Anakuangalia. Kwa sasa hana uwezo wa kuongea lakini kinachoongea kwa kishindo ni nafsi yake. Hadi hapo kama husisimki kama yule mdada, basi ujue furaha ya Noeli imekukwepa. Ujio namna hiyo wa Mungu kwetu ni kizungumkuti kinachotuacha solemba. Kutokana na kizungumkuti hicho ni vigumu zaidi kuusadiki Ujumbe wa Neno hilo lililozaliwa kwetu.

Kizungumkuti kingine kipo bado katika jina la mtoto huyo. Kwa kawaida binadamu tunawasiliana kwa maneno na kwa nafsi zetu. Tunawasilisha ujumbe jinsi tunavyotazama, tunavyovaa, tunavyochanja miili yetu ili wengine watuangalie, watushangae, watusikilize na kutuona tulivyo.  Aidha kutomwitikia anayetusalimia ni lugha pia ya mawasiliano. Mtoto huyu ni Neno la Mungu lililobeba ujumbe mzito kwa binadamu bila kuzungumza. Atakapokuwa mkubwa atatueleza kwa maneno anachokitaka Mungu kwa binadamu. Hapo inabidi kumwangalia mtoto huyu kwa dhati siyo kwa chati, na kumtafakari kwa kina, ili kumwilisha ujumbe huo katika uhalisia wa maisha ya waja wake.

Mwinjili analiainisha Neno hilo kuwa ni Nuru inayoangaza giza lililogubika ulimwengu. “Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Giza linalotuzuia tusione vizuri na kutufanya tuchanganye mambo, yaani tumchanganye binadamu na vitu. Kama alivyosema Yesu mwenyewe baadaye: “Binadamu hana thamani kuliko kondoo.” Aidha giza linapugaza akili kiasi cha kumwona Mungu kuwa mtawala na hakimu katili. Kumbe Neno (Mtoto) ni nuru inayoangaza gizani na giza halitaishinda nuru ya Neno hilo.

Baada ya hapa Mwinjili anatujulisha Yohane, shahidi wa hiyo nuru: “Palitokea mtu ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Binadamu hatuoni nuru au mwanga, bali tunaona vitu vilivyoangazwa na mwanga. Kama akavyosema Yesu mwenyewe: Ninyi ni nuru ya dunia na ndivyo mtakavyotakiwa kuangaza. Siyo  kuangaza kwa nuru yenu, bali mtang’aa nuru yangu. Kama mtajiruhusu muangazwe na nuru yangu, basi mtakuwa kama asili ya nuru. Yohane Mbatizaji aliangazwa na nuru ya Neno la Mungu na uso wake ukaangaza kiasi wengine wakamdhani kuwa yeye ndiye hiyo nuru. Naye akawajibu: “Mimi siye yule ajaye.” Kwa hiyo shahidi wa kweli hazungumzi kutoka elimu ya vitabuni au magazetini, bali anashuhudia na kujihusisha katika jambo analolisimulia. Kw hiyo, ushahidi wa Yohane Mbatizaji haukaniki kwa sababu  anaishuhudia nuru ya Neno.

Baada ya kutujulisha shahidi wa hiyo nuru, Mwinjili anaturudisha tena kwenye mada ya nuru ya kweli anaposema: “Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu akija katika ulimwengu.” Yaani  kutoka mwanzo ulimwengu uliumbwa vizuri ili uweze kuipokea nuru. Lakini ulimwengu ukakataa kuupokea kwa sababu ulipendelea giza. “Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.” Maneno ya binadamu yanaweza kuwa mwanga au giza, ukweli au uwongo. Yanaweza kuletesha upendo au chuki; uzima au kifo. Kwa hiyo tujihadhari kwa sababu kuna hatari ya kutoa ushahidi kwa nuru ya uwongo. Tumsikilize mtoto ambaye ni Neno linaloakisi nuru kweli.  “Mtoto ni anasema ukweli.”

Wale wanaolipokea Neno hilo, yaani walio wanyenyekevu, wanyonge, fukara wanafanywa kuwa watoto wa Mungu. “Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.” Tuifuate nuru hii inayotuongoza gizani na katika bonde hili la machozi, na tulisikilize Neno hili la ukweli. Kiini cha historia ya binadamu ni pale Mungu anapofika na kukaa nasi: Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Huu ndiyo umwilisho mzima wa Mwana wa Mungu. Neno liliuvaa mwili siyo kama kuivaa kanzu au koti. Bali amekuwa mmoja wetu katika kila kitu, katika udhaifu wetu, ulegevu wetu na ubinadamu wetu unaokufa  ili kwa njia ya ubinadamu wake tuweze kuuona utukufu wa Mungu. Kumwamini Mungu ni rahisi sana. Lakini ni vigumu sana kuusadiki umwilisho wake katika mtoto huyu.

Imani juu ya Fumbo la Umwilisho wa Mungu ndiyo inayoshangaza na kuchanganya akili ya binadamu. Kama wewe hushangazwi nalo, basi hapo hujaufahamu bado ukuu wa upendo wa Mungu. Huyu ndiye Mungu  ambaye kutokana na upendo wake usiokoma amekubali kujenga mji wake katikati yetu: “Naye Neno alifanyika mwili akakaa kwetu” Mungu amechagua kuwa mtumwa, kuosha miguu na kutoa maisha yake msalabani kwa ajilia ya binadamu. Ukweli wa Fumbo la umwilisho wa Mungu ni ajabu  kwa vile ufahamu wetu unashindwa kukamata ukweli huo. Kwa hiyo Noeli ipo katika kushindwa kwetu kuufahamu ukweli huo na kutufanya tuutafakari utukufu wa Mungu. “Nasi tukauona utukufu wake, ututukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

Katika Agano la kale Utukufu unamaanisha kudhihirika  kwa upendo wa Mungu. Tukiupokea upendo huo wa Mungu, hatuna budi kukiri kwamba hivi ndivyo Mungu alivyo. Hivi maisha yetu yataangazwa na mwanga wa Neno la upendo. Yohane alilishuhudia hilo Neno, akapaza sauti na kusema: “Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea neema juu ya neema.

Ndugu zangu, hakuna aliyemwona Mungu wala aliyewaona mababu zetu akina Adamu, Abrahamu, Yakobo, nk. “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote.” Lakini aliyeishi na Yesu alibahatika kumwona na kumgusa Mungu: “Mungu Mwana pekee aliye katika kiti cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.” Hawa ndiyo wale mitume kama anavyoshuhudia Mwinjili Yohane: “Kile tulichokiona na kukisikia tunawatangazieni kusudi furaha yetu iwe kamili. (I Yoh.) Nasi tutafakari Neno hilo la Mungu katika Injili na tutamwona yeye ambaye hakuna anayeweza kumwona. Kisha tukawatangazie wengine furaha ya Noeli.

Heri kwa Sikukuu ya Noeli.

24 December 2018, 07:06