Sherehe ya Noeli: Tafakari Juu ya Fumbo la Umwilisho: Upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu! Sherehe ya Noeli: Tafakari Juu ya Fumbo la Umwilisho: Upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu! 

Sherehe ya Noeli: Tafakari ya Fumbo la Umwilisho!

Mwishoni Mungu aliufunua upendo wake kwa yeye mwenyewe kuutwaa ubinadamu wetu. “Mwisho wa siku hizo amesema na sisi katika Mwana, alimweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu”. Nafsi ya pili ya Mungu ambayo tangu uumbaji imekuwa msingi na chanzo cha ubinadamu na kazi yote ya uumbaji ma ukombozi!

Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.

Taalimungu juu ya asili ya mwanadamu inamtaja mwanadamu kama yeye aliyezaliwa tangu mwanzo katika namna ya upendeleo kabisa. Kwanza anaonekana amezaliwa kwa sura na mfano wa Mungu: “Mungu akasema, na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu” (Mw 1:26). Kisha mzaburi anaukumbusha uzuri huo anaposema: “Mtu ni nini hata humkumbuke, na mwanadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima (Zab 8:4-5). Katika Agano jipya Mtakatifu Paulo akauthibitisha muunganiko huo kati ya Mungu na mwanadamu katika namna njema kabisa akisema: “kwa kuwa alitutangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake” (Ef 1:5). Nukuu hizi zote zinaonesha uteuzi wa mwanadamu tangu awali wa kuwa kiumbe aliyependelewa na kuwekwa karibu na Mungu.

Dhambi ilipoingia ulimwenguni mwanadamu aliififisha haiba hiyo na matokeo yake akaingia katika mahangaiko makubwa. Mungu wetu alimtangazia wokovu na katika safari ya historia nzima amejaribu kujifunua kwa mwanadamu kama Baba kwa lengo ya kuuonesha upendo wake mkuu na wa kudumu. Mwishoni Mungu aliufunua upendo wake kwa yeye mwenyewe kuutwaa ubinadamu wetu. “Mwisho wa siku hizo amesema na sisi katika Mwana, alimweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu”. Nafsi ya pili ya Mungu ambayo tangu uumbaji imekuwa msingi na chanzo cha ubinadamu na kazi yote ya uumbaji ameutwaa ubinadamu wetu na kudhihirisha kwetu jinsi ambavyo Mungu alinua mwanadamu awe. Hivyo ndivyo inavyoanza kuthibitisha Injili ya sherehe ya leo kwamba: “vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika”

Yeye ambaye ni sababu ya uwepo wetu anakuwa pamoja nasi; Yeye ambaye wakati wa uumbaji aliitia ndani mwetu asili yake ili kuufanya uwepo wetu uhisi uwepo wake anakuwa pamoja nasi katika namna si ya kuhisia tena bali anakuwa sawa na sisi. Mungu wetu hakai tena pembeni yetu, mbali na sisi bali ni Emmanueli, yaani Mungu pamoja na sisi. Ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho na nyakati zote ni zake. Mwanadamu anaipokea namna yake halisi ya tangu hawali ya kuwa mtu kweli. Hii ni kwa sababu mwanadamu kamwe hawezi kuwa mwanadamu kweli pasipo kuunganika na Mungu. Mungu ndiye kanuni iliyowekwa ndani ya kazi yote ya uumbaji na uwepo huu ndiyo unawezesha yote kufanyika katika harmonia nzuri. Sasa tujiulize: Ni uwepo gani wa Mungu ndani mwanadamu unaweza kuleta tija zaidi ya huu wa kufanyika wana wa Mungu kwa sababu ya fumbo la umwilisho? Hakika Mwana wa Mungu anapofanyika mtu kama sisi ubinadamu wetu unarudishwa katika namna yake njema ya tangu uumbaji.

Maandiko ya Mababa wa Kanisa yananogesha umuhimu wa fumbo hili la Umwilisho. Mtakatifu Ireneus wa Lyon anaandika hivi: “Ni kwa namna gani mwanadamu angeweza kwenda kwa Mungu kama Mungu hakuja kwa mwanadamu? Mwanadamu angewezaje kujikomboa kutoka katika mauti yake, kama asingeumbwa tena, kadiri ya imani, katika namna mpya aliyofadhiliwa bila malipo kutoka kwa Mungu, kupitia Yeye anayekuja katika tumbo la Bikira… Neno amefanyika mwili kwa ajili ya kumfanya mwanadamu kushiriki umungu, hivyo kwa sababu ya urithi huo, mtu huyo akawa mtoto wa Mungu: Hivyo namna ya mauti iliondolewa na sisi tulikubaliwa na kuwa watoto wa Mungu”. Hakika fumbo hili tunaloliadhimisha linatuonesha kweli mwanadamu anaondolewa katika hali ya dhambi; katika hali ya mauti. Ni fumbo ambalo linatangaza vita dhidi ya shetani na ni habari ya matumaini kwa mwanadamu anayeteseka akiwa amefungwa na kongwa la utumwa wa shetani.

Tendo la kufanyika upya kwa ubinadamu wetu ni tendo la ukombozi. Nabii Isaya katika somo la kwanza la Sherehe hii anamwelezea yeye anayeleta habari hii kuwa ni yeye aletaye habari njema na ya furaha. Ni maneno ambayo yanapata fursa kupenya katika nafsi zetu na kuutafakari ulimwengu wetu wa leo; ni fursa ya kuiangalia hali ya mwanadamu katika jamii inayotuzunguka. Ni dhahiri kwamba zipo dalili nyingi ambazo zinaonesha mwanadamu anajisikia yupo gizani. Hayo yanaweza kuelezewa na matukio kama vita, vurugu, mashindano baina ya watu, chuki, ukandamizaji wa haki na mengineyo mengi; wapo wanaoteseka kwa magonjwa ya kiroho na kimwili n.k. Wote hawa wanaonesha ipo sehemu ya ubinadamu ambayo bado haijaionja habari njema ya wokovu ulioletwa na Kristo.

Tunashindwa kuipokea nuru inayotushukia na tunaendelea kubaki gizani. Ni jambo la kusikitisha sana kwa kuipoteza nafasi hii adhimu. Ni dhuluma kubwa kweli kuligeuza tendo hili la kimungu kuwa la kibinadamu na kuyapatia uzito matukio ya kibinadamu tu. Angalia leo hii jamii inavyokazana kuandaa matamasha mbalimbali ya kuhamasisha jamii bila kuanza kuwaelekeza watu katika mambo ya kiroho. Wakati mwingine mambo haya yanaingia hata katika nyua za Kanisa, wakati ambapo tupo bize kuandaa burudani na mapambo bila kuwaandaa watu kiroho. Shamrashamra zetu zinauthibitishia ulimwengu kuwa tunafahamu maana ya fumbo hili tunaloliadhimisha. Sasa kama maana yake ikiwa ni kuurudishia ubinadamu hadhi yake tunajikuta mimi na wewe kuwa ni sehemu ya hao wanaotangazwa na Isaya katika somo la kwanza, yaani wale wanaowapelekea watu wote habari njema. Shamrashamra zetu zinapata tija pale tunapozifanya “ncha zote za dunia kuuona wokovu wa Mungu wetu”.

Katika Ibada ya Misa ya mkesha wa Sherehe hii Nabii Isaya anasema maneno yafuatayo: “watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangazia… maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume” (Is 9:2,6). Kwa maneno mengine siku hii isibaki kuwa tu ni ya shamrashamra, bali pia inatupatia jukumu kubwa la kuwa habari ya furaha kwa watu wote walioko gizani kuwa sasa wokovu wetu umetufikia. “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana wa pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”. Tuisherehekee siku hii kwa namna stahiki kwa kumwandalia Kristo makao ndani ya mioyo yetu ili aweze kufanyika mwili ndani mwetu. Kwa njia hii tunakuwa ni nuru ya kuwaangazia watu wote habari ya furaha, tunakuwa kama “yeye autangazaye wokovu, auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki”. Ninawatakia maadhimisho mema ya Sherehe ya Noeli.

Noeli 2018: Fumbo Umwilisho

 

24 December 2018, 07:57