Kipindi cha Majilio: Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli!
Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.
Mpendwa msikilizaji wa Vatican News! Dominika ya tatu ya Majilio inajulikana kama Dominika ya furaha (Gaudete). “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu”. Ujio wa Masiha ni hakika ya wokovu wa mwanadamu. Utume wake ambao tunatarajia autekeleze unampatia mwanadamu utukufu ambao aliupoteza kwa sababu ya dhambi. Ndiyo maana mwanadamu anaingia katika hali ya furaha. Furaha hii tunaweza kuitafakari katika namna mbili: kwanza kama nafasi mpya anayotupatia Kristo ya kuaanza upya na kumfanya azaliwe tena ndani ya nafsi ya kila mmoja na hivyo kukua naye na kutembea naye.
Pili ni furaha ipatikanayo tunapotembea katika uhuru wa kweli. Namna hii hupatikana pale tunapobaki tumeunganika na Kristo. Hivyo namna zote mbili za kungojea wakati wa majira haya ya Majilio zinaonekana, yaani furaha ya kuungana tena na Kristo na kuufanya uwepo wake kuwa kichocheo cha maisha yangu na pili ni kuungana naye siku ya mwisho katika furaha inayojengwa na uhuru wa kweli.
Leo hii tunaalikwa kujitafutia furaha ya kweli ipatikanayo katika Kristo. Tunaambiwa: “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu”. Ni furaha ambayo inatufanya kujiachilia katika yote kwa ajili ya Kristo ili kuyapata yote. Ni furaha ambayo inatuunganisha na Mungu na ndugu zetu. Furaha hiyo ni kuwa na Kristo moyoni mwako. Yeye aliye asili yetu na sababu ya kila lililo jema anabisha hodi katika nafsi ya kila mmoja wetu ili kumneemesha na mema ya mbinguni na hivyo kuipokea furaha ya kweli.
Katika somo la Kwanza Nabii Zefania anatupatia mwaliko huo wa furaha akisema: “Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu”. Sababu ya furaha hiyo anaielezea chini kidogo akisema: “Bwana Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa”. Fumbo la umwilisho ambalo tunakaribia kuliadhimisha, ambalo pia ndiyo sababu ya furaha yetu linauthibitisha uaguzi huu kwani Mungu anatwaa asili yetu, anafanyika mtu kama sisi na kufanya maskani yake kati yetu.
Yohane Mbatizaji anaelezea namna ya kujiandaa ili kuipokea furaha hiyo. Bila shaka wasikilizaji wake katika Injili wamemwelewa na kugundua maana na umuhimu wa mahubiri yake na hivyo wanaifungua mioyo yao ili kuipokea furaha ya kweli: “Tufanya nini basi?” Hili ni swali la mmoja ambaye anatafuta suluhisho la yanayomsibu kuendeana na kile ambacho amekisikia. Yohane Mbatizaji anawaelekeza kutimiza wajibu wa kawaida wa kijamii; wajibu wetu kwa jirani zetu. Kama umedhulumu basi unapaswa kurudisha ulichodhulumu, kuepuka kuwasingizia wengine uongo, kutenda kwa haki katika kufanya maamuzi na katika ujumla wake ni kumweka Mungu wa kwanza katika utendaji wako wote.
Yohane Mbatizaji anawaambia kuwa upendo wetu au hamu yetu ya kutaka kujiunga na Mungu inapaswa kuonekana katika muuganiko wetu na wenzetu. Pale ambapo mmoja anaistawisha haki, amani, umoja, msamaha, kumsaidia mwingine kuinuka, kuhudumiana n.k, ndipo atakapoweza kuidhihirisha furaha ya kweli. Mwenye furaha ya kweli ni yeye ambaye hana deni na Mungu wala na jirani yake. Yohane Mbatizaji anamwambia kila mtu atekeleze vema kile ambacho amefanyika kukifanya. Katika utekelezaji huo yeye hasiti kuwaonesha mahali au namna ambayo inasababisha ukosefu wa haki na kuziainisha hitilafu ambazo mmoja anapaswa kuzishinda. Hii inakwenda sanjari na wito wa jumla wa wanadamu wote kuelekea utakatifu. Wito huu unamtaka kila mmoja wetu kuitikia nafasi yake na kuitekeleza vema kadiri inavyotakiwa.
Hapa tunaliona jukumu nyeti la Waamini Walei ndani ya Kanisa ambao wanaitwa kuutakatifuza ulimwengu kwa matendo yao. Wao huitwa kuwa nuru ya ulimwengu. Mkristo hapaswi kujirandanisha na mienendo ya kidunia kama anavyoonya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita akisema: “Wakristo wameitwa ili kuikataa mienendo haribifu na kuogelea wakikinzana na mkondo” (Rejea Africae Munus, namba 32), bali anapaswa kuwa taa inayoangaza jamii ya mwanadamu kuelekea katika ukweli.
Jamii mamboleo inatafuta furaha. Furaha hii haijengwi katika haki kwa kumpatia jirani yako kinachomstahiki au kupokea unachostahiki bali katika kudhulumu na kupata zaidi. Furaha hiyo huonekana katika vitu vinavyoshikika kama fedha na mali; katika umaarufu na madaraka na si katika amani, uelewano na upendo na ndugu yako. Hivyo, kila mmoja yupo radhi kutumia nguvu za kiakili kwa kuhadaa, silaha au wakati mwingine nguvu za giza ili mradi mwishoni aonekane ni mwenye furaha. Kwa bahati mbaya mara nyingi furaha hizi huwa ni za mpito na mwisho wake huwapeleka wengi katika majuto, mahangaiko na msongo mkubwa wa mawazo. Haya ni matokeo ya dhambi, wakati ambapo mwanadamu alipojitenga na Mungu. Kitendo hiki kimemfanya mwanadamu kutoweza kuiona tena sura ya Mungu iliyopambwa katika sura ya ndugu yake. Furaha yake inajengwa na matendo yake ya kujitenga na kujilimbikizia mwenyewe. Furaha yake ipo katika kuona mwenzake anakosa na kuteseka ili hali yeye anaendelea kutajirika na mambo ya ulimwengu huu.
Mkristo anaishi katika ulimwengu huu uliojaa kila namna ya taabu na dhiki. Hii inamaanisha kwamba yeye si kisiwa. Taabu wanazozikabili wanadamu zinampata hata yeye. Kimwili anavutika kutaka kutafuta furaha kama ulimwengu unavyoelekeza leo hii. Lakini huo haupaswi kuwa mwenendo wetu. Mtume Paulo anatuambia: “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu”. Wosia huu unatuelekeza katika kuitafuta furaha ya kweli ipatikanayo kwa Mungu. Kristo amekuja ulimwenguni ili tuwe na uzima tena tuwe nao tele. Katika hili ndipo tunapoionja furaha ya Injili, yaani kujiweka hai na kujirandanisha na Kristo. Katika Yeye tunaweza kutembea katika ukweli na hivyo tunaweza kuyakabili maisha si kwa namna bandia bali katika uhalisia.
Tendo hili linadokeza paji la imani. Muunganiko wetu wa ndani na Kristo ndiyo unaotufanya tujitegemeze kwake na kutuwezesha kuyapokea yote anayotuelekeza kama msingi wa ukweli na mwongozo wa maisha. Ukaribu wetu na Mungu ndiyo unatuimarisha katika imani. Matendo yetu ya kiimani kama sala, sadaka na kushiriki masakramenti ndizo nyenzo za kutuweka karibu zaidi na Mungu na hivyo kujirandanisha na Kristo daima. Hivyo, tunapoalikwa kuitafuta furaha ya kweli, idumuyo na ipatikanayo kwa Kristo tujibidiishe katika imani yetu. “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu”.