Bikira Maria anamtembelea Elizabeth: Injili ya upendo na ukarimu
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma, Tanzania.
Jumapili ya kwanza ya majilio tuliadhimisha ahadi, Jumapili ya pili tuliadhimisha toba, Jumapili ya tatu tuliadhimisha furaha, leo tunaadhimisha sherehekeo la Fumbo la Umwilisho. Msukumo wa kutangaza Neno kama walivyofanya Maria na Yesu. Kwa ufupi, Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio ni ushuhuda wa ukarimu na unyenyekevu kama kielelezo makini cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake, changamoto na mwaliko wa kudumisha Injili ya huduma inayomwilishwa katika upendo. Bikira Maria kumtembelea Elizabeth ni ushuhuda wa fadhila; ni mkutano kati ya Agano la Kale na Agano Jipya; huruma na upendo wa Mungu unaookoa na kuponya; ushuhuda wa Injili ya matumaini, kwa watu wa Agano la Kale na kama ilivyo kwa watu wa ulimwengu mamboleo!
Ndugu wapendwa, leo tunaadhimisha jumapili ya nne ya kipindi cha Majilio. Jumapili ya mwisho kabla ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwake Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Injili ya leo yaelezea Bikira Maria kumtembelea shangazi yake Elizabeth na makutano hayo hukamilika Maria akimtukuza Mungu – moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu yamshangilia Mungu mwokozi wangu. Yohane anakutana na Yesu, Agano la Kale hukutana na Agano Jipya. Hapa, Bikira Maria atusaidia kuweka wazi mambo yaliyokuwa yamefichika kama vile kuzaliwa kwake mkombozi. Kilichokuwa siri sasa si siri tena na kwamba utukufu huo unatokea na kuonekana kati ya wanyonge na wanyenyekevu. Maria analeta furaha na utofauti katika maisha ya Elizabeth – baadaye Yohani anamsaidia Yesu katika maandalizi na utendaji wa utume wake.
Kwa namna ya pekee pia katika somo la kwanza tunaona jinsi mwandishi anavyozungumzia udogo wa Yerusalemu katika Yuda, katika yeye anazaliwa masiya – Zab. 138:6 na 1 Pt. 5:5. Sura hii ya tano ya nabii Mika yaelezea kwamba Israeli ataongozwa na mfalme mpya. Nabii anaonesha kuwa katika udogo na unyenyekevu, Mungu anaingia na kutenda. Hivyo tunaangalishwa tuingie katika mtazamo huu ili tuweze kuupokea utukufu wa Mungu. Ni kwa nini Mungu awaangalie wanyonge? Katika tendo la ufunuo wa Mungu kwetu sisi, daima Mungu amewaangalia wanyonge na waliopondeka moyo. Ni tendo ambalo hatuna budi kulitafakari sana.
Katika somo la pili – tunakumbushwa kuwa ni katika Kristo Yesu, sisi tumekombolewa. Somo latuonesha Mwana wa Mungu anayepokea hali ya mwili – dhamira kamili ya noeli. Pia somo latueleza ni kwa nini Yesu kaja ulimwenguni – kuyafanya mapenzi ya Baba – hivyo sadaka ya kweli. Hiki ndicho kitu halisi cha kutoa katika adhimisho la sherehe ya kuzaliwa Bwana kwetu. Kujitoa sisi ili tuwe kabisa mali yake Mungu na kumtumikia yeye tu. Ndugu wapendwa, sherehe ya noeli huendana na kutoa zawadi. Noeli ni kutoa. Mtoaji wa kwanza na mtoa chema ni Mungu mwenyewe. Tunamsherehekea Mungu anayemtoa mwanawe – Yoh. 3:16 – kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Mungu anatoa na watu wake wanatakiwa kutoa, hiyo ndiyo noeli. Kama noeli ni sherehe au kipindi cha kutoa, na Mungu ametoa utukufu wake, Je, sisi tunampatia nini Mungu kama shukrani? Changamoto hii itufikirishe sana.
Ni kitu gani cha kutoa na namna gani tutoe ili tumrudishie Mungu utukufu na sifa? Mama Bikira Maria katika somo la Injili anatuongoza vizuri sana na kutusaidia kuishi maisha ya shukrani na kujitolea. Yeye alitambua mahitaji ya shangazi yake, akajitoa mwenyewe, akafunga safari katika mazingira magumu akaenda kumtembelea binamu yake ili aweze kumsaidia katika wakati ule wa kujiandaa kupata mtoto. Hakika ni rahisi kutoa zawadi ya maua, keki, fedha n.k lakini uwepo hai wa mtu hasa kwa mwenye hitaji ni tofauti kabisa na zawadi ambayo hutolewa kama kitu. Mtu si kitu na kitu si mtu.
Anatufundisha Bikira Maria kuwa kujitoa huku kunaendana na hitaji la mwenye shida. Hali ya Elizabeth ilihitaji msaada wa karibu. Maria alitambua na kulifanyia kazi. Hiyo ndiyo zawadi ya kweli. Zawadi zetu kipindi hiki cha Noeli hazina budi kuwa na mtazamo tofauti na tulivyozoea. Oneni furaha ya Elizabeth kwa kutembelewa na mama wa Mungu. Ndiyo zawadi ya kweli ya kimungu. Kwa njia ya hawa wawili tunapata kuona wazi ujio wa ukombozi na ukamilifu wa utukufu wa ahadi ya ukombozi kwetu. Mkutano wa Maria na Elizabeth waonesha utimilifu wa ahadi ya Mungu.
Pia leo Mwinjili Luka anatusaidia kujua zaidi nafasi ya Yesu katika maisha yetu. Tukiongozwa na Yohani mbatizaji, twaona jinsi Mungu anavyomtumia mwanadamu katika kumfahamu yeye. Luka aonesha muunganiko wa Agano la kale na jipya na jinsi Yesu anavyotoa maana mpya kwa kile kilichotokea kabla. Yohani mbatizaji ana nafasi kubwa sana katika taalimungu ya mwinjili Luka. Yohane ni ukamilifu wa ujumbe wa Agano la Kale. Yesu anafunga historia moja na kuanzisha au kufungua mlango kwa kipindi kipya.
Baada ya watoto hawa kukutana wakiwa tumboni mwa mama zao, hakuna mahali po pote Luka akionesha Yesu na Yohane kukutana tena. Luka anaongea Yohani kutuma wafuasi wake wawili kumwuliza juu ya ujumbe wake – Lk. 7:18-23. Lakini hakuna mahali panapoonesha kuwa walikutana. Wakati wa Yesu ni wa kipekee na wa kwake peke yake. Yeye peke yake anatoa maana mpya kwa historia. Hata katika ubatizo wa Yesu uliofanywa na Yohane, Luka hataji jina la Yohane. Asema tu kwamba Yesu alibatizwa – Lk. 3:21-22. Na zaidi sana katika kifungu kinachotangulia ubatizo wa Yesu, Luka asema kuwa Herode alikuwa amemfunga gerezani Yohane. Lengo kuu la mwinjili Luka ni kuonesha kuwa Yohane alitoa nafasi kwa Yesu kufanya kazi yake kwani ndiye aliyesubiriwa. Jambo hili kwa Luka ni muhimu sana. Yesu anaweka/anakamilisha kile kilichotokea au kilichotangulia na anafungua kipindi kipya. Yeye anakuwa sasa ndiye Bwana wa historia mpya.
Mtakatifu Ireneo katika maandishi yake karne ya 3 “DHIDI YA UZUSHI” “AGAINST HERESIES” anaandika hivi: akielezea kazi ya Kristo akisema, imani ya Kikristo, inatambua kuwa Mungu ni mmoja na Yesu Kristo mwanae, Bwana wetu, ambaye vitu vyote viko chini yake. Kati ya vitu hivyo yupo mwanadamu, ambaye ni sura na mfano wake Mungu. Hivyo naye mwanadamu ni mali yake naye Mungu asiyeonekana, akaonekana kwetu, tukamfahamu, 3,16,6 Gia’ e Ancora’ (Already and not Yet) CCCXX, 1979, p 268.
Kwa kuadhimisha kipindi cha majilio, muda wa kumbukumbu na matumaini, sisi waamini tunapata nafasi ya kukumbuka matendo makuu ya wokovu aliyotutendea Mwenyezi Mungu na kuishi kwa matumaini huu upendo wa Mungu wa wokovu ulioletwa kwetu na Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu. Wajibu wetu ni kumpokea huyo mwokozi. Maisha ya kina mama hawa wawili – Elizabeth na Maria yatupatie changamoto kubwa juu ya namna ya kumpokea mwokozi, namna ya kumshukuru Mungu na namna ya kumrudishia Mungu sifa.