Kipindi cha Majilio: Furaha ya kweli inafumbatwa katika toba!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Hii ni dominika ya tatu ya Majilio, dominika inayotwa pia ya furaha. Kipindi chote cha Majilio ni kipindi kinachoashiria furaha ya ujio wa Masiha. Dominika hii ya tatu inachukua kwa namna ya pekee jina hili kutuonesha kuwa furaha hiyo sasa iko karibu. Ndivyo inavyosema pia antifona yake ya mwanzo “furahini katika Bwana sikuzote, nasema tena furahini, Bwana yu karibu”.
Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Zef. 3:14-17) ni kutoka kitabu cha Nabii Zefania. Huyu ni nabii anayefahamika pia kama “Nabii wa Siku ya Bwana” kwa maana kiini cha ujumbe wake wa unabii kilikuwa ni kuwakumbusha watu kuwa Siku ya Bwana i karibu. Ndani ya ujumbe wake huu Nabii Zefania alibeba mwaliko wa toba. Alilenga kuwaalika watu watubu na wageuze mienendo yao ili Siku ya Bwana ambayo ni siku ambayo Bwana atakuja kuwaangamiza wakosefu isiwe kwao siku ya uchungu, mahangaiko, giza na uharibu.
Katika somo la leo, Nabii Zefania anaanza kualika watu wafurahi na kushangilia: “Imba ee binti sayuni, piga kelele, furahi na kushangilia..” Anataja sababu ya kushangilia kuwa ni kwa sababu Bwana ameziondoa hukumu za Israeli na amemtupa nje adui yake. Hukumu za Israeli ni zipi? Na adui wake ni yupi? Ndani ya ujumbe wote wa Nabii Zefania, hukumu za Israeli ni adhabu kwa sababu ya makosa yao na adui wake ni dhambi zake. Kumbe Nabii hapa tayari anaidokeza Israeli kuwa iwapo itafanya toba kabla ya kufika ile Siku ya Bwana basi atasamehewa na adhabu yake itaondolewa naye atakuwa na sababu ya kufurahi na kushangilia katika siku hiyo ya Bwana. Na hii ndiyo sababu anaendelea kutaja katika somo hili kuwa Bwana atakushangilia kwa furaha kuu na atatulia katika upendo wake. Ni unabii unaodokeza furaha yake yule anayetubu.
Somo la pili (Fil. 4:4-7) ni waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Ni kutoka katika somo hili dominika ya leo inapata maneno ya antifona yake ya mwanzo “furahini katika Bwana siku zote, nasema tena furahini…Bwana yu karibu”. Mtume Paulo anawaandikia wakristo wa mwanzo ambao kama sisi walitumaini ujio wa pili wa Kristo lakini hawakujua anarudi lini. Na kwa kutokujua huko walijiaminisha kuwa ujio wake u karibu mno. Matokeo yake baadhi waliogopa, walikata tamaa ya kuishi maisha kama kawaida kwa kuwa hawakuona maana ya kujishugulisha kama ujio wa Bwana u karibu.
Mtume Paulo anawaandikia kuwaambia hawana sababu ya kuogopa hata kama ujio wa Bwana u karibu. Wawe watu wa furaha na tena wafurahi katika Bwana. Ujio wa Bwana usiwaondoe katika mfumo wa kawaida wa maisha kama wakristo. Na kwa maneno mengine anawaambia waendelee kutimiza wajibu wao kama kawaida. Wadumu katika kusali na kuomba, waishi katika fadhila za upole na kumcha Mungu na wawe na amani. Na amani hii ambayo ni tunda la fadhila ndani ya Bwana itawahifadhi arudipo Bwana wakati wowote ule.
Injili (Lk. 3:10-18) injili ya leo inaendeleza dhamira ya somo la kwanza na la pili kuhusu siku ya Bwana, siku ya ujio wa Bwana na inaiweka katika mafundisho ya toba ya Yohane Mbatizaji. Toba, ambayo ilikuwa ni sehemu kubwa ya manabii wa Agano la Kale, lilikuwa ni tendo ambalo liliambatana na matendo ya kiibada kama vile mtu kujivika mavazi ya magunia na kujipaka majivu. Yohane Mbatizaji katika Injili ya leo anaongeza kitu kipya: toba ijivike upendo kwa jirani na iambatane na mabadiliko katika mfumo wa maisha binafsi na maisha ya jamii kwa ujumla.
Na hivi kwa umati anawaambia mwenye kanzu mbili ampe asiye naye na mwenye chakula afanye hivyo hivyo; kwa watoza ushuru anawaambia toba ni kuepuka tamaa ya kuzidi kumyonya masikini kwa kisingizio cha kodi, kwa askari ambao waliwakilisha wafanyakazi katika dola ya kirumi ambao walikuwa na mishahara midogo, anawaambia toba yao ni kutokudhulumu watu ili kufidia mishahara yao midogo, toba yao ni kutokushitaki watu kwa uongo, yaani kutowatumia watu vibaya kukidhi mahitaji yao. Yohane Mbatizaji anasisitiza kuwa toba lazima lazima iendane na mabadiliko ya maisha.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya tatu ya majilio, dominika ya furaha, ni dominika inayoleta kwetu mwaliko wa kumgoja Bwana kwa furaha. Kwa maana Kristo tunayengojea ujio wake ndiye masiya anayetuletea furaha; furaha ya kimasiha. Tunapoyaangalia vema Maandiko Matakatifu katika liturujia ya leo tunaona kuwa kiini cha furaha hii ya kimasiha ni toba na wongofu. Kumbe dominika ya leo inaendeleza mwaliko ule ule wa majilio, mwaliko wa kufanya toba na wongofu, kwa kutuonesha furaha aipataye yule anayetubu na kugeuza mwenendo wake.
Kwa maneno mengine, dominika ya leo inalenga kutuambia kuwa ni yule aliyetubu anayeweza kwa kweli kuwa na furaha maishani. Ni yeye tu anayeweza kufurahi kwa sababu baada ya maondoleo na msamaha anakuwa ameutua mzigo unaoelemea maisha yake, anakuwa ameipatia roho yake amani na wala dhamiri yake haitamsuta kwa sababu toba inamuweka mtu mbali na hatia ya dhambi na kwa maneno ya nabii Zefania Bwana atamfurahia. Ujumbe huu wa dominika ya leo unaleta kwetu mwangwi maneno ya mzaburi “ana heri aliyesamehewa dhambi na kusitiriwa makosa yake. Ana heri Bwana asiyemhesabia upotovu ambaye rohoni mwake hamna hila” (Zab. 32:1) na yale ya Yesu mwenyewe “kuna furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye” (Lk. 15:10).