Askofu Renatus Nkwande: Kilele cha Maadhimisho ya Noeli Kitaifa!
Na Askofu Renatus Nkwande, - Mwanza
Utangulizi: Wapendwa katika Kristo, sikukuu ya Noeli ni Siku kuu ya familia, sikukuu ya jumuiya, sikukuu ya upatanisho na amani. Katika Fumbo hili la umwilisho, Mwenyezi Mungu anapenda kurudisha mahusiano ambayo mwanadamu aliyapoteza kwa kutenda dhambi na hivyo kujikuta akiwa mbali na Mungu. Kristo anachukua ubinadamu wetu, ili kutupatanisha tena na Mungu. Upatanisho huu, ndiyo unaomrudishia mwanadamu hadhi yake kuwa mwana mpendwa wa Mungu, na hivyo kuwa mshiriki na mrithi wa Familia kubwa ya Mungu. Familia ambayo inakaa katika umoja unaodumishwa kwa amri kuu ya mapendo, kwa kuzingatia haki na amani ya kweli. Mwenendo wa namna hii, ndiyo mwenendo unaotuletea uzima tele, tena uzima wa milele.
Familia ya binadamu na Mungu: Familia ni zawadi ambayo Mungu alipenda kumtunuku mwanadamu. Kama vile Mungu mwenyewe anaovyoishi katika Familia ya Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Baba, Mungu mwana na Mungu Roho Mtakatifu, sisi nasi tunaalikwa kuishi na kutenda katika uhalisia huo wa kifamilia. Familia zetu zidumu katika upendo wa kweli, upendo wa dhati. Kila mwana familia aonje furaha ya upendo huo. Familia zetu sio kamilifu, na kwa pamoja tunapaswa kuchukuliana na kusaidiana ili kuufurahia upendo huo wa familia.
Kila mmoja na wote kwa pamoja tufanye wongofu wa ndani, ili tuwe kweli chanzo cha furaha ya upendo katika familia zetu, na sio chanzo cha maumivu na madonda. Familia nyingi leo hii zimepasuka, familia nyingi zina madonda au majeraha yenye maumivu ya upendo na uaminifu. Sikukuu hii ya Noeli, katika Fumbo la Umwilisho, tufanye juhudi za dhati kutubu, kubadilika, kurekebisha palipoharibika, ili tuweze kurudisha hali ya furaha ya upendo katika familia zetu. Mtoto Yesu awe kwa hakika kiungo chetu katika familia na jamii yetu. Tupendelee zaidi msamaha, ukweli, uvumilivu, wema, upole, kujali, kuwajibika, haki na amani.
Familia ya Kikristo nchini Tanzania: Familia nyumbani, inaunganisha familia nyingi ili kutengeneza familia pana katika jamii. Kanisa la Tanzania tunaadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya ukristu. Kuna mafanikio mengi tunayashuhudia katika uinjilishaji kwa kipindi hiki. Kwa hakika tunamshukuru Mwenyezi Mungu, kutujalia mapadri na maaskofu wazawa wengi, pia watawa wa kike na wa kiume, ingawa bado mavuno ni mengi na tungependa tupate watenda kazi wengi zaidi. Tunamshukru Mwenyezi kwa kutujalia vyama vya kitume na Jumuiya ndogo ndogo, vyenye washiriki hai na vinavyoonesha kukua siku kwa siku.
Tunamshukuru kwa zawadi ya Halmashauri Walei inayoadhimisha miaka 50 mwakani., yaani 2019 Utume ambao ni wa msingi katika kujisikia sehemu muhimu ya Familia ya Mungu hapa nyumbani, na katika kuyatakatifuza malimwengu. Tunamshukuru Mungu kwa mahusiano mazuri kati ya Kanisa na serikali katika kuhudumia raia na wakazi katika taifa letu, kwenye sekta mbali mbali na hasa katika afya na elimu. Tunashukru pia kwa mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya watu wa madhehebu na dini mbali mbali kati yetu. Hatuwezi kuzikwepa changamoto zinazotukabili kwa mfano uinjilishaji wa kina. Imani hii tuliyoipokea kupitia wamisionari, kama zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tunahitaji kuimwilisha zaidi na zaidi katika maisha yetu. Namna yetu ya kuishi na kutenda inapaswa kuakisi imani tunayoikiri na tunayoiadhimisha. Haiwezekani kutenganisha imani na utamaduni, mila na desturi za watu mahalia. Sababu imani sio nadharia, bali ni maisha ya watu.
Hivyo tamaduni zetu safi zipokee na kuboreshwa na Injili yake Kristu. Mfano ukarimu, mshikamano, umoja, maisha ya Jumuiya, undugu na urafiki. Kati ya changamoto kubwa tulizonazo, ni hatari ya kuiga tamaduni za wengine kiasi cha kupoteza kabisa utambulisho wetu. Tuzingatie na kuenzi yale mema tuliyofundishwa na kurithishwa katika mila na desturi za mababu zetu. Tuwe wakarimu, wapenda umoja na amani.
Kutakatifuza Taifa la Tanzania: Nabii Isaya anatabiri “Tazama jinsi ilivyo mizuri juu ya milima, miguu yake aletaye habari njema, yeye aitangazaye amani, aletaye habari njema ya mambo mema, yeye autangazaye wokovu” (Rej., Isaya 52:7). Zawadi ya umoja na amani katika taifa letu, ni tunu ambayo inatutambulisha kimataifa na tunapaswa kujisikia fahari kwa hilo. Hata hivyo tunapaswa pia kuilinda amani hiyo kwa hali na mali, bila kuruhusu wadudu wowote waharibifu kuitafuna.
Usiku ule anapozaliwa mtoto Yesu, Malaika anawatokea wachungaji kondeni ili kuwapasha habari hiyo njema. Kisha jeshi kubwa la malaika wa mbinguni linaimba kumsifu Mungu “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Rej., Luka 2:14). Kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristu kunapaswa kutuletea amani katika familia zetu, katika taifa letu na ulimwengu kwa ujumla.Amani hii ya mtoto Yesu, ni amani ya kweli, amani inayobubujika kama kijito cha maji kutoka ndani kabisa ya moyo wa mtu. Ndiyo sababu kabla ya kuondoka kwake kutoka duniani, Bwana Yesu anapoahidi Roho Mtakatifu anatamka wazi mwenyewe kutuachia amani hiyo ya kweli: “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa, niwapavyo mimi, sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu wala msiwe na woga” (Rej., Yohane 14:27). Ulimwengu huu waweza kudhani kwamba amani inapatikana kwa visasi na mtutu wa bunduki, la hasha!, amani inapatikana kwa mazungumzano.
Katika Ujumbe Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2019, Baba Mtakatifu Francisko anasisitiza kwamba: amani inapaswa kujengwa katika siasa safi ambayo ni huduma kwa ajili ya wananchi; inayofumbatwa katika sanaa ya kusikiliza na kushirikisha karama na mapaji kwa ajili ya ujenzi wa jamii katika misingi ya haki na usawa, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Kwa mantiki hiyo, amani inapaswa kuonekana katika jamii kwa kuzingatia huduma kwa maisha ya wananchi. Tunaipongeza serikali yetu, na wadau wote wa maendeleo na watetea haki na amani kwa juhudi zao katika hilo. Mwaliko kwa taifa zima, kuhakikisha tunailinda amani hii kama mboni ya jicho, na kuunga mkono kwa hali na mali juhudi za maendeleo kwa kila mmoja na taifa letu kwa ujumla.
Hitimisho: Tuendelee kuwaombea hawa watakaoimarishwa leo, waweze kuwa kweli chachu ya kutakatifuza malimwengu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wanaempokea. Tuwaombee na kuendelea kuwasindikiza kwa sala na malezi endelevu, ili watolee ushuhuda wa Injili ya Kristu katika maisha yao ya kila siku. Nasi sote, tumpokee mtoto Yesu, yeye aliye nuru halisi na amani ya kweli katika maisha yetu. Tumpokee mtoto Yesu ili tufanyike kweli wana wa Mungu, ndani ya familia yenye amani na wapenda maendeleo. Nakutakieni nyote sherehe njema za Noeli, na heri ya mwaka mpya. Mungu azibariki familia katika taifa letu la Tanzania.
Alleluya… Mtoto Yesu Amezaliwa!