Tafuta

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Mng'ao wa utukufu wa Bikira Maria Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Mng'ao wa utukufu wa Bikira Maria 

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili

Bikira Maria alikuwa daima mwaminifu na kusema: “Mimi ndimi mtumishi wa Bwana.” Bikira Maria ni alama na mfano wetu hai wa ushindi wa Mungu dhidi ya uovu, ya ubinafsi, na ya unyoka katika ulimwengu huu. Hii ndiyo maana ya Sherehe ya leo, changamoto na mwaliko wa kujiachilia katika mipango ya Mungu katika maisha.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB. – Vatican.

Papa Pio IX kunako mwaka 1854 alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria!

Kila binadamu anapenda mafanikio katika maisha. Binadamu anajipiga kifua na kujilundikia sifa kutokana na mafanikio aliyofikiwa. Kinyume chake anapokosa kufanikiwa na kupata matatizo ikiwa ni pamoja na kuumwa basi anamtafuta mchawi. Wakati wa mitetemeko ya ardhi na wa ajali zinazosababisha vifo vya watu wengi wasio na hatia, hapo hata Mungu analaumiwa na kuhojiwa: “Kama Mungu yuko kweli anawezaje kuacha majanga yatokee.” Ama kweli, “Mbaazi zikikosa maua husingizia jua.”

Bahati mbaya hali hiyo hutokea kwa sababu baadhi ya binadamu hatutambui ya kuwa nguvu njema na mbovu tulizonazo ndani mwetu zimewekwa na Mungu mwenyewe na tunatakiwa tuzitawale sisi wenyewe na kuziongoza kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwani Mungu ametupatia uhuru tutumie nguvu hizo tunavyotaka sisi. Hii ndiyo siri ya upendo wa Mungu kwa binadamu. Kwa hiyo, inabidi kayakubali na kuyapokea matokeo yake.

Ndugu zangu Sherehe ya leo inajibu maswali ya msingi yanayomkera binadamu. Maswali hayo yamejikita katika kuhoji chanzo cha maovu yote yatokeayo hapa duniani. Maswali hayo yanapatikana katika somo la kwanza katika sura ya tatu ya kitabu cha Mwanzo cha Biblia. Sura hii inatuletea mazingira na mwendo wa mambo yanayompelekea binadamu kumkana Mungu na kujichukulia maamuzi mkononi ya kufuata mambo yaliyo kinyume na matakwa ya Mungu. Matokeo yake binadamu anajitatiza mwenyewe na kuishia kulia na kusaga meno katika bonde hili la machozi.

Aidha katika Sherehe ya leo tunapata mfano hai wa binadamu wa kweli anavyotakiwa kuwa. Binadamu anayejikubali na anayeitawala nafsi (hulka) yake. Binadamu anayeyapokea matokeo ya maisha yanapomwendea kombo bila kumtafuta mchawi, bali anaishia kusema “Mimi ni mjakazi wa Bwana, nitendewe unavyotaka Mungu.” Na anapofanikiwa anafurahi na kuimba: “Moyo wangu wamtukuza Bwana, na roho yangu imeshangilia katika Mungu Mwokozi wangu.”  Binadamu huyo pekee ni Mama yetu Bikira Maria Imakulata ndiye tunayemsherehekea leo.

Katika Biblia imebainishwa wazi kuwa baada ya Mungu kumaliza kazi ya uumbaji: “Mungu akaona kila kitu alichofanya, na tazama, kilikuwa kitu chema na bora sana na cha kupendeza.” Duniani kulishamiri haki, amani na upendo; na binadamu walihusiana vyema. Kila mtu alikuwa zawadi kwa mwingine. Hali hii ndiyo inayoitwa Paradisi au bustani ya Edeni. Tungeweza pia kusema kuwa mimi ndiye hiyo bustani nzuri na ya kupendeza aliyoiumba Mwenyezi Mungu. Tunasoma pia kuwa katika bustani hiyo Mungu alimwumba nyoka. Huyo nyoka, “alikuwa mwerevu sana kati ya hayawani wote wa mwituni aliowaumba Mungu.”

Katika tamaduni za mataifa mengi hapa duniani, nyoka anatazamwa kwa jicho hasi. Nyoka ni mnyama hatari na wa kutisha. Mathalani katika hadithi za Wapersia, nyoka alichukuliwa kuwa adui mkuu wa miungu. Ni mnyama mwerevu, mwongo, mdanganyifu, mlaghai na anayeweza kuilaghai hata hekima ya Mungu. Katika tamaduni za makabila mengi ya Waafrika, nyoka anaogopwa sana na anatumiwa pia kufanya mazingaombwe. Nyoka hatabiriki, na kutokana na tabia yake ya kujivua gamba, daima anaonekana kuwa mpya, mchanga na asiyezeeka. Kadhalika nyoka anateleza haraka sana na kujificha. Nyoka anafisha kutokana na sumu yake.

Binadamu kutokana na uhuru alionao alitumia akili na utashi wake, kuvunja maagizo ya Mungu.  Mara moja baada ya kumwasi Mungu binadamu akajikuta mtupu bila nguo mwilini. Akajificha. Lakini Mungu kutokana na upendo wake mkuu akataka kumwumbua Adamu kutoka mafichoni na kumrudisha kwake. Mazungumzo yaliyofuata kati ya Mungu na Adamu, ni changamoto na tafakari ya binadamu dhamirini mwake baada ya kujikuta ametatika. Hasa baada ya kujifanya mjuaji na kumwacha Mungu. Ama kweli “Ndege mjanja hunaswa kwenye tundu bovu.”

Mungu alikuwa wa kwanza kuanzisha majadiliano hayo: “Adamu uko wapi?” Swali hili halikumaanisha kutaka kujua pahala alipojificha binadamu. Bali Mungu alitaka tu kumhadaa binadamu, kwamba baada ya kumwasi anajisikiaje. Adamu akajibu kwa aibu: “Nimejificha.” Na alipoulizwa “kulikoni ajifiche?” Adamu alijitetea na kusema: “Nipo uchi.”  Yaani, hakuwa tena na “chochote cha kujivunia.” Ama kweli ukimwacha Mungu, binadamu huna kitu: “Bila wewe mwanadamu hana kitu. Yote kwake yanakosa.” Baada ya hapa kunafuata mahojiano mazito kati ya Mungu na mwanadamu aliye uchi. Hapa ndipo unapomwona binadamu anavyomtafuta mchawi aliyemwingiza katika matatizo yake. Hebu tumsaidie Adamu kumtafuta mchawi aliyemvua nguo na kumwacha uchi.

Mungu alimwuliza Adamu: “Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi?” Ukweli wa mambo hakuna aliyemwambia Adamu kuwa yu uchi, bali Adamu amesutwa na dhamiri yake baada ya kumwacha Mungu. Mungu anaendelea kumhoji: “Je, umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?” Adamu akajibu bila wasiwasi: “Huyu mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.” Hapa mchawi ni Eva. Lakini ukweli, Adamu anataka kumlaumu Mungu mwenyewe kuwa ndiye aliyekosea kumwumba Eva. Hivi Mungu mwenyewe ndiye mchawi. Kisha Mungu anamhoji Eva: “Nini hili ulilolifanya?” Naye Eva anaruka kesi na kumtafuta mchawi wake na kusema: “Nyoka alinidanganya, nikala.” Ni dhahiri kabisa hata Eva naye alitaka kumlaumu Mungu kwa kuumba viumbe (huluka) mbalimbali ikiwa na pamoja na huyu nyoka mwerevu. Kadhalika hapa kesi ya uchawi anabambatizwa Mungu mwenyewe. Haya ndiyo mapato ya dhambi.

Mungu anaamua kutoa adhabu kali kwa nyoka. Anasema: “Kwa sababu umefanya hayo umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni. Kwa. tumbo utakwenda, na mavumbi utakuwa siku zote za maisha yako.” Ukifuatilia kwa undani malumbano hayo yote utagundua kuwa Adamu, Eva na nyoka yuko ndani ya nafsi ya binadamu mwenyewe. Yaani ile hali ya umimi na ubinafsi. Swali la kujihoji binadamu kwa sasa lingekuwa: “Hadi lini hali ya unyoka itabaki ndani ya binadamu?” Hali hiyo ya nyoka itavunjwavunjwa na kushindwa kabisa, na kulegea na kushindwa kusimama na kutembea mithili ya askari aliyevunjwa miguu na kubaki anagalagala kama nyoka. Hadi hapa kila mmoja anaweza kutafiti dhamiri na kutafakari juu ya imani. Kila mmoja wetu ni Adamu na Eva na kwamba binadamu amepagawa na nyoka mwerevu, mjanja, mwongo, mdanganyifu na mlaghai. Bikira Maria ni binadamu pekee aliyekikanyaga kichwa cha nyoka wa ubinafsi wa binadamu.

Kwa Sherehe ya leo sisi sote tunaalikwa kuyaiga maisha ya Mama Bikira Maria. Jinsi alivyomfuata na kumwangalia daima Mungu na kufuata mipango yake. Hata kama ndani ya Maria kulikuwa pia na nguvu hizo za nyoka wa ubinafsi. Lakini nyoka huyo hakufaulu kumdanganya na kumwendesha Mama Maria. Maria alikuwa daima mwaminifu na kusema: “Mimi ndimi mtumishi wa Bwana.” Maria ni alama na mfano wetu hai wa ushindi wa Mungu dhidi ya uovu, ya ubinafsi, na ya unyoka katika ulimwengu huu. Hii ndiyo maana ya sikukuu ya leo.Nasi sote tumeitwa na kualikwa kuwa akina Imakulata. Hii ndiyo maana ya sikukuu ya leo. Heri sana kwa Sherehe ya Mama yetu Bikira Maria Immakulata, Mama aliyekingiwa dhambi ya asili!

B.M. Mkingiwa Dhambi Asili
07 December 2018, 09:29