Tafuta

Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu:  Dhamana na wajibu wa kila mwanafamilia Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Dhamana na wajibu wa kila mwanafamilia 

Sherehe ya Familia Takatifu: Dhamana na utume wa wanafamilia!

Kanisa linaweka mbele yetu mfano wa Familia Takatifu ya Nazareth kama kioo cha familia bora ambayo kwayo tunachota hazina kubwa kwa ajili ya kuziimarisha familia zetu. Familia hii ya Nazareth ni tunu bora na kielelezo kwetu cha familia mpya ya mwanadamu. Leo tunaalikwa kuziombea familia zote ulimwenguni ili ziweze kujimithilisha na Familia takatifu ya Nazareth.

Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.

Mpendwa msikilizaji wa Vatican News, Dominika inayoangukia katika Oktava ya Sherehe ya Noeli Mama Kanisa hutualika kusherehekea sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kanisa linatuwekea mbele yetu mfano wa familia hii ya Nazareth kama taswira ya familia bora ambayo kwayo tunachota hazina kubwa kwa ajili ya kuziimarisha familia zetu. Familia hii ya Nazareth ni tunu bora na kielelezo kwetu cha familia mpya ya mwanadamu. Leo tunaalikwa kuziombea familia zote ulimwenguni ili ziweze kujimithilisha na Familia takatifu ya Nazarethi na kwa namna hiyo kuimarisha tunu ya familia, kuinua umoja na kuuhifadhi undugu.

Masomo ya Sherhe hii yanatupatia sifa muhimu za familia ambazo kwazo ni ukombozi kwa mwanadamu. Tunaziona wazi wazi haki za kila mwanafamilia na kwa upande wa pili tunauona wajibu wa kila mwanafamilia. Watoto wanapewa wajibu wa kuwatii na kuwatunza wazazi wao. Hili ni tendo la shukrani ni kujikusanyia baraka kutoka kwa Mungu. Kuwasaidia na kuwatunza wazazi kunawafanya waingie katika uzee wao wakiwa na hali ya furaha. Kwa upande mwingine Wazazi wanaonywa kutokuwaudhi watoto na kuwakatisha tamaa. Maonyo na maelekezo muhimu na ya lazima yanuie katika kujenga. Ni kituko kwa mzazi kunuia kutaka kumkomoa mtoto wake. Kwa wazazi inapendekezwa kuwa utii na kupendana kati yao. Anayependa atatii na anayetii atapenda. Hivyo angalizo la kitume la Mtume Paulo linawataka wote kujivika fadhila za utii na upendo.

Mahusiano yetu ya kibinadamu yanapata msingi wake katika hiki kinacholetwa na fumbo la umwilisho, yaani tendo la kufanywa kuwa wana wa Mungu katika Mwana wake, yaani Bwana wetu Yesu Kristo. Ubinadamu wetu unainuliwa na kupewa cheo kikubwa sana kwani tunakuwa na uwezo wa kumwita Mungu Baba. Napenda tuielekeze Tafakari yetu mwaka huu katika upya unaeletwa na fumbo la umwilisho katika familia ya mwanadamu. Katika sherehe za kipindi hiki cha Noeli tunakiri kuwa kwa fumbo la umwilisho mwana wa Mungu amefanyika mtu na kuwa ndugu yetu. Tendo hili la neema na la upendo limepyaisha asili yetu ya kibinadamu na kuirudisha katika namna yake ya tangu uumbaji.

Tunapomuita Mungu Baba kwanza tunaanza kukiri kuwa hatukujileta wenyewe hapa duniani na hivyo kipo chanzo chetu ambacho ni Baba yetu wa mbinguni. Taswira hii inajionesha katika wazazi ndani ya familia walio chanzo cha uwepo wetu. Hivyo tunategemewa kudhihirisha haiba tunayoipokea kutoka kwa Baba na kuepuka matendo yanayoweza kuichakachuka haiba hiyo. Tukumbuke kuwa matendo hufunua asili au namna tulivyofanyika. Pili tunapokuwa wana ndani ya Baba yetu wa mbinguni tunajitambua kuwa hatuko peke yetu. Wapo wenzetu pembeni yetu ambao pia wameumbwa na Baba kama sisi tulivyo. Msingi huu unatupeleka katika kuimarisha tunu ya undugu. Ndani ya familia ya mwanadamu ndipo tunaanza kujifunza fadhila muhimu za undugu kama kusaidiana, kusameheana, kupendana nk.

Tatu tunapokuwa na Mungu kama Baba yetu na sisi tukiwa wana katika Kristo tunaelekezwa katika ufuasi. Hatua hii ni muhimu kutufikisha katika kusikiliza neno lake. Hivyo utegemezi, utii na kufuata miongozo yao ndilo jambo linalotarajiwa. Watoto ndani ya familia hata wawe wajuzi namna gani wajaribu daima kuepuka kiburi cha kutokusikiliza hekima za wazazi. Tukumbuke kuwa sikio kamwe haliwezi kukizidi kichwa. Ndani ya familia ya mwanadamu usikivu kwa maelekezo ya wazazi ni uthibitisho wa utayari wa kusikiliza maelekezo ya Mungu kama Baba yetu.

Nne tunapokuwa na Mungu kama Baba na sisi tukiwa wana katika Kristo tunategemewa kuzaa matunda. Hii inajidhihirisha katika huduma zetu kwa wenzetu kwa matendo mema. Mwanadamu hakuumbwa ili kudumaa, bali kuzaa matunda na kudhihisha uwepo wake. Ndani ya familia ya mwanadamu utegemezi wetu kwa wazazi, uimarishaji wetu wa undugu na usikivu wetu kwa maelekezo tupewayo na wakubwa wetu ni nyenzo muhimu za kutupeleka katika kuzaa matunda yaliyo mema.

“Mustakabali wa ulimwengu na Kanisa unategemea familia. Familia ya Kikristo ni msingi thabiti siyo tu wa jumuiya ya kikristo bali pia ni sekta msingi ya jamii” (Rejea Ecclesia in Africa, namba 80) Hivyo ndani ya familia ya mwanadamu tunachota tunu mbalimbali za mahusiano kati yetu na kwa namna hiyo familia inabaki kama tunu msingi ya kuimarisha mahusiano ya kibinadamu siyo tu ndani ya kanisa bali kwa watu wote ulimwenguni kote. Tunu hizi zinajidhihirisha wazi katika Familia Takatifu ya Nazareth ambamo ndani mwake mambo manne tuliyoyajadili hapo juu yanajionesha kwa wazi. Mungu ameamua kuiweka kwetu Familia hii ya Nazarethi, ambamo ndani mwake Kristo kwa kipindi cha miaka thelasini aliwaheshimu na kuwasikiliza wazazi wake na kwa upande wa wazazi wake walimpatia maelekezo muhimu yaliyotoa nafasi kwake ili kuimarika kimwili na kiroho ili kuupokea vema wito wake.

Jamii yetu leo hii imeisulubu taasisi hii nyeti ya mahusiano ya kibinadamu kwa kuiondoa kutoka katika misingi yake ya kweli, na matokeo yake hasi yanaonekana waziwazi. Chuki baina ya binadamu, visasi, ubinafsi, dhuluma na mengineyo mengi yanadhihirisha namna tulivyoondoa kiungo muhimu cha mahusiano yetu kibinadamu ambacho kina msingi wake katika Fumbo la Umwilisho. Ni vipi tunaupata msingi huo katika familia ambazo zimeamua kuishi katika muktadha wa ushoga, au familia ambazo watu wameamua kuishi hovyo hovyo bila baraka ya neema za Sakramenti ya ndoa. Ndani mwake ni vigumu kuuona uwepo wa Mungu na matunda ya uovu dhidi ya binadamu ndiyo matokeo yake. Hata ndani ya familia zinazoanzishwa ndani ya jamii ya mwanadamu nafasi hii ya Mungu inaondolewa na mara nyingi kila mwanafamilia hujifanyia mambo yake kana kwamba familia zetu zimekuwa ni mkusanyiko au genge la watu linaokosa kitu msingi kinachowaunganisha.

Kila mmoja leo katika familia zetu anaalikwa kumpokea Kristo Yesu na kumwilisha katika familia husika kusudi kwa njia yake aweze kupyaisha tena familia zetu za kibinadamu na kuziimarisha. Tumpokee, tumsikilize, tuongee naye, tuutunze uwepo wake na kuulinda na tukue pamoja naye. Sakramenti ya Ubatizo, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, inatuunganisha na Kristo na kutufanya kuwa wana wa Mungu kweli. Muunganiko huo unapaswa kudhihishwa na kila mmoja ndani ya familia kusudi misingi tunayopewa kama mfano ndani ya Familia Takatifu ya Nazarethi idhihirike katika kila familia ya kikristo na kwa njia kuwa chumvi na chachu kwa ulimwengu wote. Kwa namna hii, tutakuwa kielelezo kwa ulimwengu wote na uthibitisho wa kusafiri katika ulimwengu huu katika namna kinzani na ulimwengu, huku tukiuimarisha umoja kati ya binadamu na kuhifadhi hadhi ya watu wote.

Familia Takatifu
27 December 2018, 14:14