Tafuta

Epifania ni Sherehe ya Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Epifania ni Sherehe ya Ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! 

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Yesu ni ufunuo wa upendo wa Mungu!

Tafsiri ya Kibiblia ya zawadi hizo ni kwamba, taifa la Wayahudi ni la kifalme, la kikuhani na la kibi-arusi wa Mungu. Dhahabu inawakilisha mfalme, ubani ni alama ya kuhani na harufu nzuri ya manukato ni bi-arusi wa Mungu. Kwa sasa zawadi hizo zinatuwakilisha sisi wapagani tusiokuwa Waisraeli, lakini tulioipokea nuru ya upendo ya nyota hii yaani Yesu Kristo.

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Seoul- Korea ya Kusini.

Siku moja Kakakuona alitokea kwenye migodi ya madini ya Tanzanite huko Mererani Wilaya ya Simanjiro. Wachimbaji wadogo walipomwona waligombania kumgusa wakitaka baraka na kudai kuwa neema ya madini inakaribia kwenye migodi hiyo. Kakakuona ni mnyama adimu sana kuonekana. Akitokea tu, watu wanajua si bure wala haba, hapa lazima kuna “vijimambo”! Kuna tukio la ajabu litakalotokea. Kuonekana huko kwa kitu cha pekee kama Kakakuona, kunakotanguzana na vituko au vioja fulani, kwa lugha ya Kigiriki kunaitwa epifaino au epifaneia.

Leo Wakristo tunasherehekea Siku kuu ya Epifania au Siku kuu ya Tokeo la Bwana. Lakini hatuoni muujiza au kioja chochote cha pekee kinachotanguzana na mtoko huo wa Bwana. Hali hii inadhihirisha kuwa msafara wa Yesu kutoka mbinguni hadi duniani ni wa kawaida kabisa. Yesu amezaliwa kama wanavyozaliwa watoto wengine wowote wale katika familia maskini. Huu ndiyo mtoko wa upendo wa Mungu usio na vitimbwi wala hekaheka wala patashika nguo kuchanika!. Huu ndiyo ufunuo wa nyota inayong’aa upendo wa Mungu.

Injili ya leo inatuonesha makundi matatu ya mapokezi ya nyota iliyotokea. Hebu nasi tujipange jinsi ya kuipokea.  Kundi la kwanza ni la mamajusi. “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu.” Kuanzia Kanisa la Mwanzo, wakristo wamewahusudu sana Mamajusi na waliofahamika kuwa ni utimilifu wa unabii wa Agano la Kale, Isaya 49 na Zaburi 72 inaposemwa juu ya “Wafalme wa Sheba na Saba wataleta vipaji. Wafalme Tiro na Sidoni watakuja kumwabudu.” Idadi ya Mamajusi ilitokana na aina tatu ya zawadi walizotoa. Aidha iliwakilisha watoto watatu wa Noe, yaani Ham, Shem na Yafeti. Majina, umri na zawadi watoazo zilitofautiana.

Melkior anaoneshwa kuwa Mzee mwenye ndevu nyeupe na anatoa zawadi ya dhahabu. Baltazar ni mtu wa makamo mwenye ngozi nyeusi, anamzawadia Mtoto Yesu manukato. Gaspar ni kijana, anamtolea Yesu zawadi ya ubani. Tofauti ya rangi zao za ngozi zao huwakilisha aina tofauti za mataifa wanaomwendea Yesu. Aidha tofauti ya umri inaonesha kuwa sisi sote wazee kwa vijana tunaitafuta nuru, yaani nyota ya maisha yetu. Mamajusi waliifuata nyota, lakini walipofika Yerusalemu nyota hiyo ikawapotea, ikabidi waulizie: “Yuko wapi Yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Suala la nyota tunalisikia katika kituko cha Balak na Balaam kwenye Biblia kitabu cha Hesabu. Balak mfalme wa Moab alimtaka mamajusi mmoja atabiri dhidi ya Wayahudi.

Balaam badala ya kulaani anatabiri kuhusu kutokea nyota katika Israeli. Unabii wa Balaam Mwana wa Beol, unabii wa binadamu mwenye macho yanayotazama kwa kina sana. Unabii wa yule anayeogopa Neno la Mungu na kuelewa sayansi ya aliye juu, anayeona mwono wa mwenyezi… Mimi naona lakini siyo sasa, ninatafakari lakini siyo karibu juu ya nyota, ambayo ni ufalme unaotokea Uyahudini. Nyota ya mtu atakayeushinda Uyahudi na mmoja wa Yakobo atatawala. Hii nyota ni mfalme wa wayahudi atakayetawala ulimwengu wote.

Mtabiri huyu alifikiria nyota hiyo angekuwa mfalme Yosia, kumbe haikutimilika. Waisraeli wakaendelea kuisubiri. Leo nyota imetokea kwa mamajusi na wanaifuata. Kikundi hiki kinawawakilisha wale wote wanaosisimka wanapoiona nyota mpya yaani Yesu Kristo. Ndivyo alivyosisimka Zakaria na kuimba: “Nuru itokeayo, iliyomvuta yule atokaye juu atufikie… kuwaangazia wakaao gizani na kivuli cha mauti.”  Simeoni alisema: “Nuru ya kuwaangazia wapagani na kuitukuza taifa lako Israeli.” Malaika wanapojionesha kwa wachungaji wanaimba: “Utukufu wa Baba ukawaangaza.” Kwa hiyo Epifania ni nuru aliyoifunua Yesu ulimwenguni kuwa Mungu ni upendo.

Mamajusi hawa wanayo tabia ya kuangalia angani. Yaani, walikuwa wanautafakari uumbaji hadi wakaigundua nuru ya Mungu mwumbaji na wakautangazia. “Ulimwengu kazi ya Mungu na utukufu wa Mungu” (Zaburi 19). Kwa hiyo, kama binadamu anayajali maisha na hatima yake inabidi aangalie na kudhamiria zaidi mambo ya juu ya uumbaji wa Mungu na siyo kuangalia chini kwa mambo ya duniani tu kwani hapo anaweza kutumbukia na hatimaye, kumezwa na mwlimwengu. Tabia ya nyingine ya mamajusi ni kwamba wanapokuwa na dukuduku ya mambo yanayowasumbua rohoni hawatulii, bali wanachukulia hatua. Yaani hawapuyangi tu katika maisha yanayoonekana kuwa tata. Bali daima wanataka kujua maana ya maisha yao. Wanaolingana na mamajusi hawa ni wale wanaosikiliza dukuduku za moyoni mwao na kujiuliza juu ya maana ya maisha yao. Kadhalika mamajusi hawa hawakufunga mawazo ndani mwao, bali waliwasikiliza pia wengine.

Aidha yaonekana hawakuifahamu sawasawa nyota hii, ndiyo maana wanaifuata na wanataka kukutana nayo. Kwa hiyo walisafiri kutafuta ufalme na mwanga mpya. Katika utafiti wao, wanapambana na kikundi kingine ambacho ni kinyume nao ambao ni kundi la pili. Hawa ni wakuu wa ulimwengu huu, ambao hawakutaka kupokea nuru ya nyota iliyotokea katika umbo la mtoto Yesu. Badala yake walitaka kuendeleza ulimwengu wa mambo ya zamani. Wakuu hao walifadhaika au walichafuka vibaya sana kwa hasira wanaposikia kutokea kwa nyota ya mfalme mpya. “Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye.” Neno kufadhaika kwa Kigiriki ni etarachthein yaani, kama kule kuchafuka kwa bahari. Mfalme Herode anawawakilisha wakuu hao waliolewa vyeo. Aidha, “hata Yerusalemu pia pamoja naye (Herode) ilifadhaika.” Hapa mji wa Yerusalemu unawakilisha makao yoyote ya taasisi mbalimbali za dini.

Kwa hiyo Herode “Akakusanya wakuu wa Makuhani wote na waandishi wa watu, akatafuta habari kwao, Kristo amezaliwa wapi?” Wakuu na wataalamu wa taasisi mbalimbali wanafahamu maandiko matakatifu, lakini wanapoteza bahati ya kufungua mioyo yao na kupokea nuru ya Mungu. Ndiyo maana mamajusi wanapoingia Yerusalemu nyota ile iliyowaongoza haionekani tena. Kwa hiyo, ndani ya jiji lenye taasisi mbalimbali, mtu unazibwa macho na giza la taasisi hizo, unachanganyikiwa na huwezi kuiona kirahisi nyota mpya. Mamajusi wanaiona tena nyota kiurahisi wanapotoka nje ya Yerusalemu. “Nao waliposikia maneno ya mfalme, walishika njia; na tazama, ile nyota walioiona mashariki ikawatangulia, hata ikaenda ikasimama juu ya mahali alipokuwa mtoto.”

Makundi haya yote yalipata fursa ya kufunguka akili katika maisha na kuweza kuona nuru hata kama wako gizani. Herode angeweza kubadilika maisha yake kutoka kwenye ukatili na mauaji. Kumbe wanapoteza kirahisi fursa hiyo ya kuona nuru mpya. Mbaya zaidi, Herode anawaita Mamajusi faraghani na anawaambia uwongo kwamba itawabidi wamrudie kumpa habari za mtoto ili naye aende kumwabudu. Hapa unaona dhahiri jinsi watawala wanavyobomoa uwongo ili kutetea maslahi yao. Ni uwongo peke yake unaoweza kutetea ulimwengu wa kale. Pale ufalme, utawala, serikali, siasa kama haiko kwa ajili ya kutumikia taifa na kama inakosa uzalendo wa kuwahudumia raia haina budi kuwalaghai wananchi ili kutetea maslahi yao. Huu ndiyo ufalme wa kale ulio katika giza na unaofanya mambo yake gizani.

Nyota inawaongoza Mamajusi hadi pahala alipolazwa mtoto pembeni wakiwa Maria na Yosefu. Kwa furaha kubwa wanampigia magoti Yesu kumwabudu na kumtolea zawadi. Tafsiri ya kibiblia ya zawadi hizo ni kwamba, taifa la Wayahudi ni la kifalme, la kikuhani na la kibi-arusi wa Mungu. Dhahabu inawakilisha mfalme, ubani ni alama ya kuhani na harufu nzuri ya manukato ni bi-arusi wa Mungu. Kwa sasa zawadi hizo zinatuwakilisha sisi wapagani tusiokuwa Waisraeli, lakini tulioipokea nuru ya upendo ya nyota hii yaani Yesu Kristo. Kama Mungu alitawala taifa la Waisraeli, sasa ufalme wa Mungu unakuwa kwa Wakristo walio taifa jipya la kifalme, la kikuhani na la kibi-arusi wa Bwana.

Kundi la tatu, ambalo halikupewa uzito mkubwa ni lile la wale wachungaji kondeni waliondoka kwa haraka kwenda kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha yao. Ndugu zangu leo imetokea nyota majaabu pekee yanayotanguzana nayo ni kule kung’ara nuru ya upendo wa Mungu usio na mipaka. Tuifuate nyota hiyo na kuiishi. Heri kwa sikukuu ya Epifania.

03 January 2019, 14:30