Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili III Mwaka C: Ufunuo wa Neno!
Na Padre Joseph Peter Mosha, - Vatican.
Kristo amekuja duniani kurekebisha ubinadamu uliochakazwa na dhambi. Huu ndiyo muhtasari wa ujumbe wa Neno la Mungu tunaousikia katika Injili ya jumapili hii. Yeye amekuja duniani “kuwahubiri maskini habari njema ... kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa”. Huu ni ufunuo wa upendo wa Mungu kwetu wanadamu. Kama tulivyotafakari katika somo la kwanza la Dominika iliyopita, Mwenyezi Mungu alisema kuwa hatotulia wala kunyamaza kwa ajili ya watu wake. Mungu katika upendo wake usio na mwisho anajifunua katika nafsi ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo katika haiba ya mkombozi. Anakuja kukaa kati yetu na kumkomboa mwanadamu aliyejeruhiwa kwa dhambi.
Kristo anakuja kuturudishia hadhi yetu ambayo tumeipoteza sababu ya dhambi. Baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza mwanadamu alipoteza ile hali ya uwepo wa Mungu kati yake na kuingia katika hali ya huzuni na mahangaiko makubwa. Hii inamaanishwa kwamba, pale mwanadamu alipofanya kiburi na kuamua kutembea peke yake bila kumtegemea mwenyezi Mungu ndipo alipoanza kujifunga katika uovu wa kila aina uliojificha katika ubinafsi, ubadhirifu, chuki na visasi kwa wengine. Matendo haya yanaondoa hali njema kwa mwanadamu na hivyo hubaki kuwa kiumbe mwenye huzuni na unyonge.
Kristo amekuja kuustawisha ufalme wa Mungu kati ya wanadamu: “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk 1:15) ndiyo ujumbe anaotupatia mwanzoni kabisa mwa mahubiri yake. Hii inamaanisha kwamba, ili mwanadamu arejee katika furaha ya kweli na kuwa na mahusiano mema na Mungu anapaswa kutenda mambo haya mawili: Toba, yaani ile hali ya dhati na ya ndani kabisa ya kukiri makosa na kurejea kwa Mungu na pili ni imani kwa Injili, yaani habari njema tunayoipokea kutoka kwa Kristo kupitia mafundisho, miujiza na kwa namna ya pekee maisha yake. Habari hiyo njema ndiyo anayowafunulia watu wa nchi yake ya Nazareth leo hii na pia anaifunua kwetu sisi.
Mwaliko tunaoupata leo hii ni: “mwanadamu tambua cheo chako”. Hadhi tunayoipokea sababu ya fumbo la umwilisho ni kubwa sana. Kwa Sakramenti ya ubatizo tunashirikishwa hadhi hiyo, yaani kuwa wana wapendwa wa Mungu. Hii ndiyo namna njema tunayorudishiwa tena na Kristo baada ya kuipoteza kwa dhambi. Utambuzi huu unapaswa kuambatana na matendo hayo mawili, yaani toba na imani kwa injili. Neema ya Mungu imekwisha kufunuliwa kwetu. Ni wajibu wetu kutenda kadiri tunavyowezeshwa na neema hii ili kuuthibitisha huu mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Mwanadamu hapaswi kuishi tena katika hali ya huzuni, masikitiko na kukata tamaa kwani Mungu yu katikati yetu tena.
Katika somo la kwanza wana wa Israeli wanaipokea Torati au sheria ya Mungu kama habari njema kutoka kwa Mungu. Ezra anaisoma Torati kwa Waisraeli waliokuwa wamerejea toka uhamishoni. Kwa Tendo hili Waisreli wanafanya upya Agano lao na Mungu, kwani Torati ndiyo msingi wa taifa lao jipya. Wana wa Israeli wanaambiwa: “Siku hii ni takatifu kwa Bwana Mungu wenu; msiomboleze wala msilie”. Upendo wa Mungu umefunuliwa kwao kwa njia ya sheria zake. Sheria za Mungu zinamwakilisha Mungu kati yao na kuwa sababu ya furaha na matumaini. Hivyo kwa matumaini na ujasiri mkubwa wanapaswa kuongozwa na zaburi ya leo kwa kusema: “Sheria ya Bwana ni kamilifu huiburudisha nafsi ... maagizo ya Bwana ni adili huufurahisha moyo”.
Mtunga Zaburi anaendelea kutuambia kwamba: “Ushuhuda wa Bwana ni amini, humtia mjinga hekima ... amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru”. Hili linataka kutuhakikishia kwamba uwepo wa Mungu kati ya watu wake ni njia na ufunuo wa kuelewa siri ya utajiri wake mkuu. Mwanadamu aliye katika hali ya dhambi, yaani yeye ambaye anajiweka mbali na huruma na upendo wa Mungu hujifunga katika kuyaona makuu haya ya Mungu. Hivyo, tunaalikwa kutafakari amri na maagizo ya Mungu muumba wetu na kuyatekeleza kwa vitendo yaliyo mapenzi yake. Kwa namna hii tutaendelea kuhisi uwepo wake na kumfanya kiongozi wa maisha yetu.
Mtume Paulo anatuonesha matunda ya kuipokea hali hii ya uwepo wa Mungu. Hili hutupeleka katika umoja na mshikamano katika jamii yetu ya kibinadamu. Kila mmoja kutenda vema kadiri ya nafasi yake na karama aliyojaliwa kwa ajili ya manufaa jamii nzima. Mtume Paulo anatuonya dhidi ya ubinafsi na dharau kwa wengine. Kila mmoja anapaswa kutambua kwamba anamhitaji mwenzake kwa ajili ukamilifu ndani ya jamii. Pia kila mmoja wetu anapaswa kuthamini kazi ya mwenzake bila dharau au ubaguzi. Hakuna kazi iliyo ndogo na ya kudharauliwa.
Katika chumba cha upasuaji uwepo wa wasaidizi wa mtaalamu wa upasuaji ni wenye tija katika kuikamilisha kazi ya daktari mtaalamu. Hiyo huwa ni sababu ya ufanisi katika upasuaji huo na humrejeshea tena afya njema na furaha yeye aliye katika hali ya ugonjwa. Hivyo tunakumbushwa leo, katika Fumbola Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, na sisi viungo vyake, hali ya kutenda kwa umoja na mshikamano ni yenye tija kwa ajili ya kurejesha furaha kwa mwanadamu na huu ndio upendo wa Mungu tunaotumwa kuufunua kwa watu wote. Kristo aonekane kwa wote wanaomhitaji kwa kupitia huduma zetu kwao zilizojaa upendo, bashasha na maneno ya matumaini.
Hivyo ni wajibu wetu katika Dominika hii kutafakari juu ya furaha hii kuu inayotujia, yaani tendo hili la kurudishiwa tena hadhi yetu. Tuione hali hii ndani mwetu na kwa kila mmoja wetu. Tutimize nyajibu zetu tukiongozwa na roho ya umoja kusudi sote katika utendaji wetu tuweze kuujenga mwili wa Kristo, yaani Kanisa.