Sherehe ya Epifania: Ufalme, Ukuhani na Sadaka ya Kristo!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo ni sherehe ya Epifania yaani Tokeo la Bwana. Tunaadhimisha tendo la Yesu kujifunua kama masiya wa Israeli, kama mwana wa Mungu, mwanga kwa mataifa na mwokozi wa ulimwengu mzima.
Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Isa 60, 1-6) ni kutoka kitabu cha nabii Isaya. kwa uvuvio wa Mwenyezi Mungu, manabii walitoa daima unabii uliogusa moja kwa moja matukio na maisha ya watu. Lakini mara nyingi pia manabii walitoa unabii unaovuka yale mambo ya kawaida yanayoonekana, yale ambayo watu walikuwa wakikutana nayo moja kwa moja katika maisha yao. Katika somo hili la leo, nabii isaya anatoa unabii wa namna hiyo. Anauona mji wa Yerusalemu ukiwa umeangazwa kwa mwanga nao ukingàa na kuyaangaza mataifa yote kwa mwanga wake. Anawaona wana wa Yerusalem waliokuwa wametawanyika na wameenda mbali sasa wanaurudia mji wao na sio hao tu hata wana wa mataifa nao wanaujia mji wa Yerusalemu na wanaujaza kwa zawadi mbalimbali. hapo anauambia mji wa Yerusalemu inuka sasa na uangaze pande zote, wote wanakusanyana wanakujia wewe.
Mwanga ni alama ya utukufu. Nabii anaona katika Yerusalemu mahala ambapo patakuwa kitovu cha utukufu utakaowakusanya mataifa na hapo hapo utakaowaangazia mataifa. anatabiri juu ya Epifania ya kweli ambapo katika mji huo Mungu mwenyewe atajifunua katika utukufu wake kuwaunganisha mataifa yote katika mpango wake wa ukombozi aliouanza na taifa la Israeli na hapo hapo atayaangazia kwa mwanga halisi unaotokea Yerusalemu yaani Yesu Kristo Bwana wetu.
Somo la pili (Waef 3, 2-3. 5-6) ni Waraka wa Mtume Paulo kwa waefeso. Mtume Paulo anawafunulia waefeso fumbo la Kristo ambalo anaeleza kuwa lilikuwa limefichwa tangu enzi lakini sasa Mungu mwenyewe amelifunua kwa njia ya Kristo kwa mitume wake na manabii wake. Mtume Paulo anaeleza kuwa katika mpango wa Mungu wa ukombozi mataifa walionekana wamewekwa kando na Mungu kujihusisha tu na taifa la Israeli. Lakini Mungu mwenyewe alikusudia, kama asemavyo katika Waraka kwa Wagalatia, katika utimilifu wa wakati awakusanye mataifa yote. Na sasa wote ni warithi na washiriki wa ahadi zile zile za ukombozi pamoja na Kristo na kwa njia ya Kristo.
Injili (Mt 2, 1-12) Katika Injili tunaona tukio lenyewe la Yesu kujifunua kwa mataifa. kuzaliwa kwake kunaambatana na alama ya nyota isiyokuwa ya kawaida. Nyota hiyo inawaamsha mamajusi kutoka nchi za mbali, kutoka mashariki kujua kuwa kuna mfalme mkuu amezaliwa Bethlehemu nao wanatoka wanaenda kumsujudia. Yesu anazaliwa akitambuliwa kama mfalme na hata mwishoni pale juu Msalabani anakufa pakiwa pameandikwa Mfalme wa Wayahudi. Ufalme huu wa Yesu unaotambuliwa na Mamajusi, wenyeji hawakuutambua. Herode mfalme anaposikia anajawa na hofu na mara moja anaanza mipango ya kumuangamiza. Hata hivyo mamajusi wanaongozwa na nyota na wanafika alipozaliwa Yesu. Wanamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane. Dhahabu kuashiria ufalme wake, uvumba kuashiria ukuhani wake na manemane kuashiria sadaka atakayoitoa kwa kifo chake pale Msalabani, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika mpango wa Mungu wa ukombozi Mungu alipenda kujifunua kwanza kwa njia ya taifa la Israeli. Na ni yeye hasa aliyeliunda kuwa taifa moja pale mlimani Sinai alipoweka nalo Agano. Tangu hapo aliingia kwa namna ya pekee katika historia yao na akasafiri nao katika matukio yote ya maisha yao. Na tunaona Biblia Takatifu hasa Agano la Kale imejaa masimulizi ya mahusiano ya waisraeli na Mungu na namna wao walivyompokea na hatua kwa hatua Mungu alivyozidi kujifunua kwao hadi kumshusha mwanae wa pekee Yesu Kristo.
Adhimisho la leo ni hatua mpya ya ufunuo wa Mwenyezi Mungu, kutoka kuliunda taifa moja la Israeli hadi kuyaunganisha mataifa yote ya ulimwenguni kuwa taifa lake moja. Kristo anajitambulisha kuwa ndio Mwanga wa Mataifa. Ni mwanga kama ule ulioiangazia dunia wakati wa uumbaji ukaipa hadhi, dunia ilipokuwa tupu haina chochote na giza lilipokuwa limetanda juu ya uso wa vilindi vya maji (Rej. Mwanzo 1:3). Leo mataifa yaliyokuwa nje, yakiwakilishwa na mamajusi, wanakuja kumwabudu Kristo Mfalme na Mkombozi wa ulimwengu aliyezaliwa. Zawadi wanazomletea, dhahabu, uvumba na manemane, zinaonesha kuwa wanamkiri kuwa ndiye Mfalme, Kuhani na yule atakayejitoa Sadaka kwa ajili ya ukombozi wa wote kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kuwawezesha kupata maisha ya uzima wa milele!
Ni adhimisho kumbe linalounganisha Noeli na Pasaka - Kristo amezaliwa ili afe Msalabani. Amezaliwa kati ya Wayahudi lakini si kwa ajili ya Wayahudi tu, bali kwa watu wa mataifa yote na kwa ulimwengu mzima. Na kwa kufa kwake Msalabani analeta ukombozi kwa ulimwengu mzima. Kwa adhimisho hili tunaalikwa kumpokea Kristo kama Mwanga na mwokozi wa ulimwengu mzima. Tunaalikwa kuuruhusu Mwanga wake uyaangaze maisha yetu nasi tubebe jukumu la kuwa mabalozi wa mwanga huo wa Kristo kwa ulimwengu.