Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili II ya Mwaka: Saa ya Yesu:
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu kwa masomo ya dominika ya 2 ya mwaka C. Kisha kumalizika kipindi cha Noeli, tunaingia katika kipindi cha kawaida cha Mwaka. Kipindi cha kukua na kuchanua katika fadhila, katika imani, matumaini na mapendo na kipindi cha kukuza neema ya Mungu ndani yetu kwa msaada wa Mungu mwenyewe. Ndivyo inavyoashiria pia rangi ya liturujia tunayoitumia kipindi hiki, rangi ya kijani. Maandiko Matakatifu siku ya leo yanatuonesha kuwa Kristo, ufunuo wa kweli wa Mungu, ndiye anayemleta Mungu kwa watu na ndiye anayetambulisha uwepo wake kwa watu wake. Na anawaalika wale wanaompokea kuwa na umoja naye na kuudhihirisha umoja pia kati yao – wao kwa wao.
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Isaya 62:1-5) ni kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Nabii anaitabiria Sayuni mambo mema. Sion ni mlima mtakatifu ndani ya Yerusalemu lilipokuwapo Hekalu la Mungu. Na ni kwa sababu ya Hekalu hili mji mzima wa Yerusalemu ukaitwa mji mtakatifu na ukatwaa alama ya mji wa ukombozi na wokovu na alama ya umoja wa taifa zima la Isreli. Mji huu sasa ulikuwa ukiwa, ulikuwa umeachwa kwa sababu wanawe walikuwa wamechukuliwa mateka na fahari yake yote ilikuwa imepotea. Nabii Isaya anautabiria kuundwa upya na kuwa Bwana hatausahau wala kuuacha milele. Utukufu wake utarejea na mataifa yote watauona, wanawe wataurudia na hautakuwa tena ukiwa na Bwana ataufurahia.
Unabii huu wa Nabii Isaya hauzungumzii mji pekee kama mji bali hasa unawagusa watu wa Mungu. Watu ambao wamepita katika kipindi kigumu cha maisha katika wakati fulani wa historia yao lakini hawakuyapoteza matumaini yao kwa Bwana. Bwana anawaambia hawezi kuwaacha milele. Yeye mwenyewe atawaijia, atakutana nao na ujio wake utawarudishia fahari na furaha yao. Huu ni mmojawapo wa unabii wa kimasiya unaomwona masiya kama ndiye ajaye kufungulia enzi mpya ya Bwana kuwaijia watu wake.
Somo la pili (1Kor 12:4-11) ni waraka kwa kwanza wa mtume Paulo kwa wakorinto. Mtume Paulo anaiandikia jumuiya ya wakristo wa Korinto, jumuiya iliyokuwa na tatizo la mgawanyiko. Tangu mwanzo kabisa wa waraka wake huu, sura ya 1:10 anawaasa “nawasihi…mnene mamoja, wala pasiwe kwenu faraka bali mhitimu katika nia moja na shauri moja”. Na akaendelea, s. 12, “kusema mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo, mimi ni wa Kefa” ni sawa na kumgawanya Kristo. Katika somo la leo anawaonesha kuwa kutokuulewa utendaji wa Roho Mtakatifu na kutokuelewa makusudi ya Mungu kugawa huduma nakarama mbalimbali kwa watu wake kunaweza kuwa chanzo kingine kikubwa cha kuleta mgawanyiko na mpasuko katika jumuiya. Anawaambia kuwa Roho Mtakatifu amegawa karama mbalimbali kwa watu na karama hizo kwa kweli ni tofauti tofauti.
Utofauti huo sio kosa na hauna ubaya wowote kwa sababu ni Mungu yuleyule azitendaye kwa wote na tena kila mmoja amepewa ili kuwa faida kwa mwingine asiye na karama hiyo. Ubaya unakuja pale ambapo aliye na huduma au karama fulani anaitumia vibaya: au kwa kuwadharau wasiyo nayo, au kwa kujinufaisha mwenyewe na kuisahau jumuiya ama kwa kujiona amekuwa bora kuliko wengine. Ni hapo ndipo utofauti wa karama unapoleta mgawanyiko na mpasuko katika jumuiya. Somo hili linatufundisha kutumia vema karama, huduma na nafasi mbalimbali tulizojaliwa. Linatufundisha pia umuhimu wa kuhimiza na kujenga umoja katika utofauti na kutokuruhusu kamwe tofauti za kibinadamu ziwe ndio sababu ya migawanyiko au mipasuko katika jamii.
Injili (Yn 2:1-11) Injili ya leo inaelezea muujiza wa kwanza wa Yesu kadiri ya mwinjili Yohane arusini Kana. Wakiwa arusini Yesu anaambiwa na mama yake kuwa “hawana divai” na moja kwa moja Mama yake anawaambia watumishi “lolote atakalowaambia fanyeni”. Ni maneno yale yale Farao aliyowaambia wamisri wote wakati wa njaa “enendeni kwa Yusufu, atakalowaambia fanyeni” (Mwanzo 41:55). Farao aliamini ni Yusefu tu anayeweza kuliokoa taifa la Misri na baa la njaa, na hapa Maria anaamini moja kwa moja katika uwezo wa Yesu. Yesu anawaambia wajaze mabalasi maji na kisha anawaambia wampelekee mkuu wa sherehe. Nayo yalikuwa yamekwisha geuzwa kuwa divai.
Mwinjili Yohane hauiti huu muujiza, bali anauita ishara. Na ndivyo anavyoona katika miujiza yote ishara na alama za kimasiya za Yesu. Alama ya kwanza katika muujiza huu ni ile ya mabalasi. Haya yalitumiwa na wayahudi katika ibada zao za kujitakasa. Yalipaswa kuwa na maji muda wote lakini haya hayakuwa na maji. Yanajazwa maji kwa amri yake kuonesha utakaso mpya utakapatikana kwa jina lake tu. Alama ya pili ni “saa yake”. Anasema “saa yangu haijawadia”. Saa ya Yesu ni ule wakati muafaka ambao atatukuzwa kwa kuinuliwa msalabani na kuukamilisha ukombozi wa ulimwengu mzima. Ni saa inayotambulisha lengo la ujio wake na makusudi ya yote anayoyafanya katika utume wake. Yote yanamsogeza katika saa hiyo na yote yanapata maana katika saa hiyo. Kwa alama hii Yesu anajitambulisha waziwazi kuwa ndiye Masiha atakayekamilisha ukombozi wa waisraeli na wa ulimwengu mzima.
Alama ya tatu ni wingi wa divai. Katika muujiza huu Yesu alitoa divai nyingi na tamu. Mabalasi sita ni ujazo mkubwa sana kupita mahitaji ya sherehe yoyote ile. Katika agano la kale, uwingi wa divai tamu ni alama ya kieskatolojia ya ujio wa siku ya Bwana. Rej Amos 9:13, Yoeli 3:18 – “siku ile milima itadondosha divai tamu”. Yesu anapofanya muujiza wake wa kwanza na kuleta divai nyingi na tamu anaashiria kuwa umefika sasa wakati ule uliotabiriwa, wakati wa Bwana kuwaijia watu wake na kuwaletea wingi wa neema zake zisizo na kipimo.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo ya dominika ya leo yanatuonesha kwa namna iliyo wazi sana mahusiano yaliyopo kati ya imani yetu ya kikristo na maisha tunayoishi kila siku. Imani ni chachu ya maisha yote ya mwanadamu. Inamsaidia kuyaelewa maisha na kuyaishi vema kama yalivyokusudiwa na Mungu mwenyewe mtoaji wa maisha hayo. Ni kwa njia ya imani tunauona bayana uwepo wa Mungu katika maisha yetu: Mungu asiyetusahau milele, Mungu anayeturudishia furaha na fahari ya kuumbwa kwetu na Mungu anayetujulisha alama za ukombozi wetu kwa njia ya Kristo.
Haya yote, yanahitaji kutafsiriwa katika maisha ya kila siku vinginevyo imani inabaki kuwa kitu cha nadharia na kilicho mbali na uhalisia wa maisha yetu. Ndiyo maana masomo ya leo yametuwekea ufunuo huu sambamba na mwaliko wa kupambana na changamoto ya utengano na mipasuko katika jamii zetu. Hakuna jamii ambayo haijaonja adha ya mipasuko au utengano. Iwe ni jamii ndogo kama familia au iwe ni jamii kubwa kama jumuiya au taasisi. Leo tunaalikwa kurudi nyuma kidogo na kujiuliza nini hasa chanzo cha utengano na mipasuko hii?
Sio kweli kama asemavyo Mtume Paulo kuwa ni kutokana na matumizi mabaya ya karama alizotujalia Roho Mtakatifu? Ni wazi katika jumuiya patakuwa na utofauti: utofauti wa mawazo,utofauti wa upeo, utofauti wa itikadi, utofauti wa kipato na kadhalika. Je hizi ni sababu za kujenga chuki, visasi na mipasuko? Je hatuwezi pamoja na tofauti hizi kujenga jumuiya inayoridhiana, inayoheshimiana na kuthaminiana katika tofauti tulizonazo? Ni hapa nguvu ya imani yetu inapoweza kutuhakikishia kuwa tunaweza kuzishinda tofauti zetu na kuunda jamii iliyoungana. Tuamini katika ukubwa uleule wa imani kama aliyokuwa nayo Maria Mama wa Yesu kwa mwanae na imani hiyo ituangazie kumweka Kristo kama mhimili wa umoja katika familia na jumuiya zetu.