Ubatizo wa Bwana: Ahadi za Ubatizo: Kumkataa Shetani
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu leo ikiwa ni sherehe ya Ubatizo wa Bwana. Hii ni sherehe ambayo kiliturujia inahitimisha kipindi cha Noeli na inaashiria mwanzo wa kipindi cha kawaida cha Mwaka. Adhimisho la ubatizo wa Bwana, ndani yake, linaendeleza ufunuo wa Kristo. Usiku wa Noeli alijifunua kwa wachungaji na kwa watu masikini, siku ya Epifania akajifunua kwa watu wa Mataifa, leo katika ubatizo wake anajifunua kwa wayahudi kuwa ndiye Masiya aliyetabiriwa na manabii. Ndiye Kristo mwana mpendwa na wa pekee wa Mungu Baba.
Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza (Is 42, 1-4. 6-7) ni kutoka kitabu cha nabii Isaya. Ni kifungu ambacho kinaitwa pia wimbo wa kwanza wa mtumishi wa Bwana. Nabii Isaya anaagua juu ya yule anayeitwa mtumishi wa Bwana. Anaeleza kuwa huyu atakuwa ni mtumishi ambaye Bwana anapendezwa naye, Bwana ataweka Roho yake ndani yake naye ndiye atakayeleta haki kwa mataifa. Atatenda kwa unyenyekevu, hatakuwa mkaidi na atajua namna ya kuwachukulia watu wake hasa wale walio dhaifu kama mwanzi uliopondeka au utambi unaoelekea kuzimika.
Wayahudi wenyewe walipokuwa wakizisoma nyimbo hizi za Mtumishi kwanza walijiona wao kama taifa kuwa ndiye huyu mtumishi anayezungumziwa na nabii Isaya. Walijitambua kuwa taifa lililoundwa na Mungu, taifa linalompendeza Mungu lakini pia taifa lililofunzwa unyenyekevu na upole kupitia matatizo mbalimbali waliyokumbana nayo. Hata hivyo walijiona kuwa hawatoshi katika unabii huo na hapo walianza kutumaini kuwa ipo siku Mungu atamuinua mtumishi wake halisi ambaye atakuwa kweli Mtumishi wa Bwana, atakayejaa Roho wa Bwana, atakayeleta haki kwa mataifa na atakayetenda kwa upole na unyenyekevu. Hatua kwa hatua wakaishi wakimgoja mwokozi huyu na matumaini ya ujio wake yakazidi kuijaza mioyo yao.
Somo la pili (Mate 10, 34-38) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Mtume Petro yupo katika nyumba ya mpagani aliyeitwa Kornelio. Huyu japokuwa hakuwa myahudi, alishukiwa na Roho Mtakatifu kama walivyoshukiwa mitume. Hapo Petro anakiri kuwa Mungu hana upendeleo. Lakini pia anaeleza jambo lingine muhimu kuwa ni pale katika ubatizo wa Yesu ambapo Mungu alimpaka mafuta kwa Roho Mtakatifu na Nguvu ili awe wokovu kwa waisraeli na kwa wote wanaomcha. Kwa kiri hii ya mtume Petro ubatizo wa Yesu ndio uliokuwa mwanzo wake wa kutekeleza kwa hadhara kazi ya ukombozi iliyomleta duniani. Ni baada ya ubatizo wake alipoanza kuzunguka kuhubiri habari njema na kuponya wale waliokuwa na masumbufu mbalimbali na ni kwa njia ya ubatizo wa Yesu, ubatizo umekuwa alama ya ukombozi kwa wote wanaomwamini.
Injili (Lk 3, 15-16, 21-22) inaeleza tendo lenyewe la ubatizo wa Yesu. Ni ubatizo ulioambatana na ushuhuda kumhusu Yesu mwenyewe, kwanza na Yohana Mbatizaji na pili na Mungu. Yohana alianza kumshuhudia Yesu akisema kuwa yeye Yohana siye Kristo. Anamshuhudia kwa watu waliokuwa wamejawa matumaini ya kumsubiria Kristo na walipomwona Yohana na yote aliyokuwa akiyafanya wakadhani kuwa ndiye. Naye Yohana anasema Kristo ni yule ambaye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na moto, ndiye atakayeanzisha ubatizo mpya si ule wa maji na toba bali wa Roho Mtakatifu na moto. Katika injili ya Yohane, anaenda mbele zaidi anamwonesha kwa watu akisema "Tazameni yule ndiye mwanakondoo wa Mungu". Pili Mungu mwenyewe alimshuhudia Kristo akisema kuwa ndiye mwana wake mpendwa anayependezwa naye. Mamlaka ya kimungu yanayotamka yanaoneshwa na kufunguka kwa mbingu na ujio wa Roho Mtakatifu kwa mfano wa njiwa.
Huu ni ufunuo mpya kumhusu Kristo. Sauti ya Mungu inatumia maneno yale yale ya wimbo wa nabii Isaya, wimbo wa Mtumishi wa Bwana kuonesha kuwa yule mtumishi wa Bwana ambaye waisraeli walimngojea alete haki, yaani awaokoe, ndiye huyu Kristo. Kristo ndiye Mtumishi mpendwa wa Bwana aliyetabiriwa na nabii Isaya. Mungu anamfunua pia Kristo kuwa ni mwana wake. Hivyo Kristo anakamilisha unabii mwingine kama wayahudi walivyokuwa wakisali katika Zaburi ya pili "ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa" (Zab 2,7). Ni hapa tunaona kuwa ubatizo wa Yesu ulikuwa ni wasaa muafaka wa kumfunua Kristo kwa wayahudi. Ni hapa anapofunuliwa kuwa ndiye Masiya aliyetabiriwa, ndiye Mtumishi wa Bwana, Ndiye mpakwa mwafuta yaani Kristo na ndiye Mwana wa Mungu.
Tafakari: Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, adhimisho la Ubatizo wa Bwana ni adhimisho ambalo kama jinsi masomo ya leo yanavyotuonesha, linaweka wakati mahususi wa Yesu kujitambulisha kwa wayahudi kuwa ndiye Masiya aliyekuwa akingojewa. Yeye ambaye hakuwa na dhambi hakuhitaji kabisa ubatizo. Pamoja na hayo alijongea kubatizwa na Yohane Mbatizaji ili kuthibitisha ushuhuda na utume mzima wa Yohana Mbatizaji. Na kwa kumwona Yohane Mbatizaji kama Nabii wa mwisho, Yesu kwa kubatizwa naye anathibitisha na anakamilisha unabii wa manabii wote waliomtangulia katika Agano la Kale.
Yesu anapobatizwa na Yohane anaanzisha ubatizo mpya wa maji na Roho Mtakatifu kwa maondoleo ya dhambi na anayatakatifuza maji yote ya ubatizo watakayobatizwa wote wanaomwamini. Anauanzisha ubatizo mpya kama sakramenti itakayokuwa mlango kumpokea yeye, mlango wa imani kwake na mlango wa wokovu kwani "asipozaliwa mtu kwa maji na Roho Mtakatifu hawezi kamwe kuuona ufalme wa Mungu" (Yoh 3,3). Na kwa kuwa Yesu Kristo ndio wokovu wenyewe, ubatizo basi unakuwa ni mlango wa kuuingia wokovu huo, unakuwa ni mwanzo pia wa kuanzisha mahusiano na Kristo anayeokoa, na ndiyo maana kila mbatizwa anaitwa M-Kristo yaani aliye wake Kristo. Ibada ya sakramenti ya ubatizo inayoambatana na kumkataa shetani, kuikataa dhambi na kuikiri imani inatuthibitishia hilo na inatualika tuendelee kulipokea hilo.
Adhimisho la sherehe ya Ubatizo wa Bwana ni adhimisho linalotualika nasi tuukumbuke ubatizo wetu; tukumbuke ahadi zetu za ubatizo; tukumbuke misingi na miiko ya ubatizo wetu na tujizatiti kwa msaada wa neema ya Mungu kuendelea kuishi kadiri ya ahadi zetu za ubatizo kwa furaha ile ile kama siku ile tulipoziweka kwa msaada wa wazazi, wasimamizi na Kanisa zima.