Sherehe ya Tokeo la Bwana: Yesu ni ufunuo wa Mwanga wa Mataifa!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Epifania ni Siku kuu ya Mwanga na Mwanga huo ni Yesu Kristo, mwanga unaoangaza. Mwangaza huo umewaangaza watu wote na unaendelea kuangaza. Ni sikukuu ya mafumbo ya utoto wa Yesu – KKK 528. Mamajusi kutoka mashariki walithubutu kumtafuta Mtoto Yesu, Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa mjini Bethlehemu kwa kuongozwa na nyota; tabia ya kutojali iliyooneshwa na wakuu wa makuhani na waandishi ya wa watu, waliofahamu fika Maandiko Matakatifu kiasi cha kuonesha mahali alipozaliwa Masiha, lakini wao, hawakujitaabisha kuifuata nyota hiyo! Kundi la tatu ni Mfalme Herode aliyegubikwa na hofu kubwa sanjari na kufadhaika na Yerusalemu pamoja naye. Lakini, alihofia kwamba, Mtoto Yesu aliyezaliwa angempora Ufalme wake.
Mamajusi ni watu wenye busara wa mashariki ambapo baada ya kuiona nyota na kwamba Bwana amezaliwa, walienda Yerusalemu kumwabudu. Zawadi walizochukua zilipatikana huko kwao – Yer 6:20. Mababa wa Kanisa waliona kuwa dhahabu ni mfano wa ufalme wa Kristo, uvumba ulionya umungu wake na manemane ikionya mateso yake. Mamajusi walimsujudia Kristo na ndivyo walivyotumia maneno ya Mungu juu ya Masiya kwamba mataifa watambwabudu Mungu wa Israeli Hes 24, 17.
Ni mwanga kwa watu wote wanaomwendea Mungu wakiongozwa na imani ya huyo Mungu mwenyewe. Katika somo la kwanza leo – Isaya 60: 1-6 - tunapata habari juu ya utukufu wa Bwana unaong’aa Yerusalemu (ambao Neno wa Mungu utatokea) mahali ambapo patakuwa ni makutano ya watu wote ili kumtukuza Mungu na kumtolea ubani na manemane. Leo, somo hili linadhihirisha wazi hilo. Watu kutoka sehemu mbalimbali wakiwa na vitu mbalimbali wakienda kumtukuza Mungu. Tunasikia habari juu ya nuru, mwanga na utukufu wa Bwana: wana na binti kutoka mbali, utukufu wa bahari na utajiri wa mataifa, misafara ya ngamia na watu kutoka Medina wakichukua dhahabu ubani na manemane wakiutangaza ukuu wa Mungu. Hii ndiyo Epifania ya kweli.
Katika somo la Pili - Waefeso 3:2-3,5-6 - tunaona kuwa kwa Waebrania walioteuliwa kwanza na kwa wapagani waliokuja baadaye wote wameitwa katika imani moja kumfuata Kristo na kugawana urithi wa milele pamoja naye. Wokovu wa Mungu ni kwa ajili ya ulimwengu mzima. Somo hili linazungumzia juu ya ufunuo wa siri ya Mungu ambayo Mungu alidhamiria tangu awali. Ni mpango ambao makuhani wa kale waligusia lakini hawakujua maana kamili ya mpango huo. Mpango huo ulikamilika tu kwa njia ya Yesu Kristo. Katika waraka kwa Waefeso 1:3-10, tunasoma juu ya wingi wa neema ya Mungu isiyopimika. Epifania ufunuo wa Mungu kwa njia ya Kristo ndiyo maana kamili ya Maandiko Matakatifu.
Katika somo la Injili leo - Mt. 2:1-12 - tunaona kuwa kutokujali na ujinga wa walimu na wakuu wa sheria, hofu na wasiwasi wa Herode imekuwa maangamizi kwao. Jibu sahihi la mamajusi – tumeona nyota yake mashariki na tumekuja kumwabudu limekuwa wokovu wao. Wanatoka mbali na wanapata wokovu. Ila walio karibu hawatambui kuwa mwokozi amezaliwa na wanaangamia milele. Somo hili latukumbusha kuwa ufunuo haukutokea kama hamu ya Mungu kujitosheleza bali kwa ajili yetu. Mungu anapenda kuwa hata sisi tuuone utukufu huo hivyo tuinuke tumwelekee kama mamajusi walivyofanya. Yahitaji pia bidii yetu. Tujitoe sisi wenyewe kwake kama zawadi. Hakika hatuna budi kumshukuru Mungu siku hii ya leo pamoja na Mtume Paulo kama anavyoandika katika waraka kwa Wakolosai 1:3,12-20 - twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo siku zote tukiwaombea tukimshukuru Baba aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.
Maana nyingine ya Epifania ni kujionyesha au kujifunua kwa maana hiyo ya Kigiriki na katika dini yao, ilikuwa desturi kwa mmoja wa miungu kumtokea mmoja wao. Katika maandiko matakatitifu neno hilo halipo. Bila shaka ni kuepa kuoanishwa na neno hili la kipagani. Kiyunani neno Epifania laelekezwa kwa Yesu na kazi yake ya wokovu mpaka siku ya mwisho. Katika 2Tim 1:10 – tunasoma hivi; lakini sasa kwa tokeo la mwokozi wetu Kristo Yesu neema hiyo imefumbuliwa kwa maana ameshinda mauti na ametangaza uzima wa milele kwa Injili. Katika Tito 2:11 – maana ya neema ya mungu iwaokowayo wanadamu wote imefunguliwa na katika Tito 3:4- lakini wema wake mwokozi wetu Mungu na upendo wake kwa mwanadamu alipofunuliwa alituokoa.
Katika Kanisa jina hili Epifania limeonekana karne ya 3 likitumiwa na kwa Yesu hivyo hatari ya kuhusishwa na upagani ikaisha. Kwa kweli Yesu ndiye ufunuo wa Mungu. Kanisa la mashariki likawa la kwanza kusherehekea sikukuu ya Tokeo laBwana likiunganisha na ubatizo wa Yesu pale Yordani. Itakumbukwa kuwa pale katika tukio hilo sauti toka mbinguni ilisikika ikasema huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu niliyependezwa naye msikilizeni yeye – Mk1:11. Mungu kwa mara ya kwanza anajifunua kuwa yeye ni nani na anajifunua kwa njia ya Yesu Kristo. Mwanae.
Kanisa la Magharibi kwenye karne ya 4 likahusisha hija ya Mamajusi na tokeo la Bwana jinsi ilivyo katika Injili yetu ya leo. Mamajusi siyo Waisraeli hivyo wanawakilisha watu wote. Mungu amejionyesha kwa watu wote hata sisi tuliopo hapa na kwa namna ya pekee ndiyo maana tupo hapa kusherehekea Sikukuu hii ya tokeo la Bwana. Tumshukuru Mungu kwamba hata leo anaendelea kujionyesha kwetu. Mamajusi waliona nyota ambayo kwayo Mugu aliwaelekeza kwenda kwa motto Yesu. Leo tunapenda kuwomba Mwenyezi Mungu ili mimi, wewe na sote tunaoliita jina lake Mungu tuwe kweli ile nyota ambapo watu watuonapo katika maisha yetu ya kumcha Mungu waweze kutamani kumpenda na kumtumikia yeye zaidi ya vitu vingine vyote na watufuate kama Mamajusi ili wafike kwa Kristo.
Matokeo ya ufunuo wake Bwana ni kwamba tunawajibishwa kuweka wazi ushindi na utukufu wake mbele ya dunia yote. Tunamshukuru Mugu kwamba hata leo anaendelea kujionesha kwetu. Mamajusi waliona nyota ambayo kwayo Mungu aliwaelekeza kwenda kwa Mtoto Yesu. Katika 2Tim. 4:1-8 tunasoma – kwa ufunuo wake Kristo tunapata amri ya kuhubiri neno la Mungu ili upate taji la haki. Mwandishi mmoja anatuangalisha kuwa haitoshi tu kuujua ukweli bali zaidi sana ni jinsi gani tulivyojiandaa kutembea na kuishi ukweli huo tulioufahamu. Haitoshi tu kujua bali yahitajika kuishi kwa imani hicho tulichokijua. Tafuteni Mwanga wa Mataifa, upate kuwaangazia katika maisha yenu! Tumsifu Yesu Kristo.