Tafuta

Sherehe ya Ubatizo wa Bwana ni kielelezo cha mshikamano na unyenyekevu wa Kristo Yesu kwa binadamu mdhambi! Sherehe ya Ubatizo wa Bwana ni kielelezo cha mshikamano na unyenyekevu wa Kristo Yesu kwa binadamu mdhambi! 

Ubatizo wa Bwana: Maisha na utu mpya katika Roho Mtakatifu!

Naye Yesu akiwa ametundikwa pale Msalabani alitobolewa ubavuni kwa mkuki na mara ikatoka Damu na Maji. Maji hayo ndiyo ilikuwa ishara ya sakramenti ya ubatizo, ambayo kwayo tunapata kuondolewa dhambi ya asili na dhambi zetu binafsi pamoja na adhabu zake. Kwa njia na mastahili ya Mwana wa pekee wa Mungu, kwa ubatizo nasi tunapokea hadhi ya kuwa wana wa Mungu.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. – Vatican.

Ndugu mpendwa, leo tunasherehekea Dominika ya Ubatizo wa Bwana. Tunakifunga rasmi kipindi cha Noeli na kuanza Dominika ya kwanza ya mwaka mpya wa Liturujia, Mwaka C. Tunaposherehekea sikukuu hii tujiulize maswali matatu ya msingi. Je, ubatizo wa toba ulikuwa na maana gani kwa Waisraeli? Je, Yesu alihitaji kweli kubatizwa? Je, sherehe hii ya Ubatizo wa Bwana ina maana gani kwetu sisi Wakristo?

Tukio la kubatizwa Bwana wetu Yesu Kristo kama jinsi tunavyosimuliwa na Waenjili, lilitokea katika mwaka wa 15 wa utawala wa mfalme Tiberio. Yohane Mbatizaji ambaye ndiye alikuwa Nabii wa mwisho wa Agano la Kale aliyekuja kumtayarishia Bwana njia, alikuwa akihubiri jangwani katika maeneo ya kusini ya Yuda karibu na kingo za mto Yordani. Alikuwa akiwahubiria watu juu ya ujio wa Ufalme wa Mungu na hivyo kuwaalika waongoke na kubatizwa. Baada ya kumwasi Mungu kwa matendo yao yasiyofaa, waisraeli walihitaji kusafishwa. Ubatizo wa Yohana unakamilisha utabiri wa nabii Ezekieli kwa taifa la Israeli unaosema, “Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya,.. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu…“ (Ez. 36: 25-27).

Watu toka sehemu mbalimbali za Yerusalemu, Yudea na sehemu zote zinazozunguka Yordani walimiminika kumwendea Yohane ili waweze kubatizwa na kutakaswa. Cha ajabu ni kwamba hata Yesu, wakati huo akiwa na umri wa takribani miaka 30 naye aliondoka toka Nazareti, sehemu aliyokuwa akiishi na aliyokulia, akafika mahali ambapo Yohane alikuwa akihubiri na kubatiza. Yesu akaunga mstari akisubiri zamu yake ya kushuka mtoni ili naye abatizwe. Kimsingi, kama Mwana wa Mungu, yeye hakuhitaji ubatizo wa toba kwakuwa hakuwa na dhambi. Hakuna namna ambayo twaweza kuelezea tendo hili la Yesu zaidi ya kutambua moyo wake wa mshikamano pamoja na wanadamu katika udhaifu, magumu na mahangaiko yao.

Hii ndiyo maana ya Fumbo la Umwilisho ambalo tumekuwa tukisherehekea siku hizi. Yesu anakubali kuchukua mwili na damu yetu ya kibinadamu, anakubali kuwa masikini ili atutajirishe ili atutajirishe kwa umasikini wake. (Rej. 2 Kor 8: 9). Tendo la kubatizwa ni ishara ya tunu ya unyenyekevu aliokuwa nayo katika maisha yake yote. Hapa anakubali Roho Mtakatifu amshukie kupitia ubatizo wa Yohana. Kama tulivyosikia katika Injili ya leo, baada ya Yesu kubatizwa mbingu zilifunguka, Roho Mtakatifu akashuka juu yake kama hua na sauti ikatoka mbinguni ikisema, “Wewe ndiwe mwanangu, nimependezwa nawe.” Hii ilikuwa ni sauti ya Mungu Baba ikimtambulisha mwanae wa pekee kwa watu. Baada ya kubatizwa Yesu akiwa amejazwa Roho Mtakatifu, aliondoka Yordani na kwenda jangwani kwa siku arobaini akitafakari na kufunga kabla ya kuanza maisha yake ya hadharani ya kuuhubiri Ufalme wa Mungu.

Kwetu sisi wakristo sherehe ya Ubatizo wa Bwana inatukumbusha ubatizo wetu, ule ubatizo ambao Yohana Mbatizaji aliuongelea akisema kwamba yeye alikuwa akibatiza kwa maji bali yule anayekuja, yaani Yesu,  atawabatiza watu kwa Roho Mtakatifu. Naye Yesu akiwa ametundikwa pale Msalabani alitobolewa ubavuni kwa mkuki na mara ikatoka Damu na Maji. Maji hayo ndiyo ilikuwa ishara ya sakramenti ya ubatizo, ambayo kwayo tunapata kuondolewa dhambi ya asili na dhambi zetu binafsi pamoja na adhabu zake. Kwa njia na mastahili ya Mwana wa pekee wa Mungu, kwa ubatizo nasi tunapokea hadhi ya kuwa wana wa Mungu na warithi wa Ufalme wa Mungu. Zaidi sana tukumbuke kwamba kwa ubatizo sisi tunampokea Roho Mtakatifu, Roho wa Kristo mwenyewe. Hii ndiyo sababu ya msingi ya sisi kuitwa wakristo.

Ubatizo pekee au majina pekee ya kikristo hayatoshi. Endapo tunataka kuwa wakristo wa kweli tumpe Roho Mtakatifu nafasi katika mioyo na maisha yetu ili apate kuongoza mawazo, mitazamo na matendo yetu. Ndiyo maana Mtakatifu Paulo katika barua yake kwa Warumi anasema kwamba mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake.(Rej. Rm 8:9b). Mtu mwenye Roho wa Kristo ndani yake ni yule anayekubali kuongozwa na roho ya Injili yaani mafundisho ya Yesu mwenye. Roho ya Injili inapatikana katika Heri za Mlimani anazotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo na  kama tunavyozisoma katika Injili ya Mathayo sura ya 5:3-10 au katika ufupisho wa heri hizi katika Injili ya Luka sura ya 6: 20-22 pamoja na Sala ya Baba Yetu.

Ndugu yangu, hiki ndicho kiini cha maisha ya ukristo. Tumwombe Mungu ili Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yetu na Neno hili lipate kuzaa matunda katika familiya zetu, katika jumuiya zetu na katika jamii na dunia nzima kwa jumla. Tumsifu Yesu Kristo.

Ubatizo wa Bwana 2019
10 January 2019, 16:59